Monday, August 21

Serikali yabanwa sakata la Bombardier kuzuiwa Canada




Serikali inazidi kubanwa kuhusu ndege aina ya Bombardier Q400 Dash 8, ambayo imezuiwa nchini Canada kutokana na kushindwa kutekeleza amri ya mahakama ya kimataifa ya kulipa fidia.
Hukumu ya Mahakama ya Kimataifra ya Usuluhishi (ICSD) iliyotolewa mwaka 2010 iliitaka Serikali kuilipa kampuni ya ujenzi ya Stirling Civil Engineering Ltd dola 25 milioni za Kimarekani na riba ya asilimia nane, lakini hadi sasa haijalipwa na hivyo deni kufikia dola 38.7 milioni (sawa na Sh87 bilioni).
Fidia hiyo inatokana na Serikali ya Awamu ya Nne kuvunja mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Tegeta Wazo-Bagamoyo bila ya kufuata mkataba.
Habari za kuzuiwa kwa ndege hiyo ziliwekwa bayana na Mwanasheria wa Chadema Tundu Lissu na baadaye Serikali kuzithibitisha, huku ikitupia lawama wanasiasa.
Jana, kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye alihoji kuhusu kutowasili kwa ndege hiyo siku chache kabla ya Lissu kuibuka, alionekana kuchukukizwa na majibu ya Serikali, akitaka iache kugeuza suala hilo kuwa la kisiasa au ushabiki wa mpira.
Wakati Zitto akisema hayo, wachambuzi wengine wamesema Serikali ina wajibu wa kutoa taarifa kuhusu mali za nchi na kuacha kulaumu wanasiasa wa upinzani.
Zitto, ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini, alisema suala la ndege hiyo linagusa nchi na mjadala wake ni lazima uwe na hadhi hiyo badala ya kuufanya wa kisiasa.
Jumatano iliyopita, Zitto alihoji katika akaunti yake ya Twitter sababu za ndege hiyo kutowasili Julai kama Serikali ilivyoahidi na mchangiaji mmoja mwenye jina la Mbarawa alijibu kuwa kulikuwa na matatizo kidogo na kuahidi kuwa yakiisha itakuja.
Juhudi za Mwananchi kuthibitisha kama mwenye jina lililotoa majibu hayo ni Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa hazikufanikiwa, lakini juzi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Zamaradi Kawawa alithibitisha kuwapo kwa deni hilo na kusema matatizo yaliyojitokeza yamesababishwa na wanasiasa walioweka masilahi yao mbele kukwamisha jitihanda za maendeleo zinazofanywa na Rais John Magufuli.
Akizungumza na Mwananchi jana, Zitto alisema majibu hayo yanataka kuligeuza suala hilo kuwa la kisiasa.
“Tusikubali kuingia kwenye huu ushabiki. Hili ni suala la kisheria, na ni suala la nchi ambayo sisi wote tuna maslahi ya kuona inakwenda mbele,” alisema Zitto.
Alisema si dhambi nchi kuwa na deni na kwamba mataifa makubwa duniani yanadaiwa.
“Mimi binafsi ninadaiwa madeni ya uchaguzi mpaka sasa na wengine kati ya wanaonidai wamenipeleka mahakamani. Si dhambi kudaiwa,” alisema.
Alisema ni muhimu wananchi kuelewa deni linatokana na nini kama ni uamuzi mbaya wa kisiasa au mikakati gani inawekwa ili kulilipa.
Zitto alisema maneno yanayosambazwa kuwa ameshiriki kuwezesha kukamatwa ndege ya Bombardier iliyonunuliwa na Serikali, ni propaganda na hazina ukweli.
“Serikali lazima ifahamu kuwa ni lazima ihojiwe na iwe tayari kutoa majibu, sisi kama vyama vilivyo nje ya Serikali ni wajibu wetu kuhoji jambo lolote,” alisema.
“Pia, ni haki yetu kupata taarifa zozote kutoka mahali popote zitakazosaidia kuisimamia Serikali. wajibu wa Serikali ni kujibu hoja zinazoibuliwa nasi.
“Suala la ndege yetu kuzuiwa nchini Canada lisifanywe la ushabiki kama wa mpira.
“Kitendo cha Kaimu Msemaji wa Serikali kulaumu wanasiasa kwa jambo la kisheria kama hili, ni utoto.”
Alisema historia inaonyesha kuwa hakuna mwanasiasa, hasa wa upinzani, anayeweza kushirikiana na kampuni za kigeni kuhujumu nchi.
“Falsafa ya chama ninachokiongoza, ACT Wazalendo, ni Taifa Kwanza, Leo na Kesho na filosofia yangu ni my country first, right or wrong (nchi yangu kwanza kwa usahihi au kwa makosa),” alisema.
Alisema Serikali ifahamu kuwa nchi ina madeni mengi na miongoni mwa madeni hayo yapo ambayo yameshaamuliwa na Mahakama.
“Kinachopaswa ni kuwa na maarifa ya kuzuia mali zetu nje ya nchi kuzuiwa kama ilivyo kwa ndege hii,” alisema.
“Hii ni nchi ni yetu sote, hakuna mwenye hatimiliki ya ukweli. Ukweli pia haupendi kupindwapindwa. Serikali itoke kueleza nini kimetokea mpaka ndege kuzuiwa.”
Maoni kama hayo alikuwa nayoProfesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu).
“Kazi za vyama vya upinzani ni kuikosoa Serikali. Wanapopata taarifa za Bombardier kuzuiwa Canada, unataka wakae kimya?” alihoji.
“Wakikaa kimya hawatakuwa wapinzani.”
Alisema Serikali itoe taarifa zinazojitosheleza kuhusu ndege hiyo badala ya kuwalaumu wanasiasa kuwa ndiyo wamesababisha mgogoro huo.
Alisema Serikali ilishaahidi kwamba ndege hiyo ingewasili Julai, hivyo kutowasili katika muda uliotangazwa kunasababisha wapinzani watafute taarifa.
Profesa Mpangala alisema sasa ni muhimu Serikali itoe taarifa kwa wananchi ni kwa nini ndege hiyo imezuiwa Canada badala ya kusubiri taarifa zitolewe na vyama vya upinzani.
“Vyama vya upinzani visilaumiwe kutoa taarifa hizo kwa kuwa wao pia ni sehemu ya jamii,” alisema.
“Tusiwalaumu wapinzani kuwa wanachochea migogoro. Kuikosoa Serikali ni moja ya kazi zao.”
Lakini, Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alikuwa na mawazo tofauti.
“Si kila jambo la Serikali linatakiwa liwekwe hadharani. Kuna mambo mengine hayawezi kuwekwa hadharani kwa sababu bado hajayaiva kuwaeleza wananchi,” alisema.
Hata hivyo, alisema si vibaya kwa Serikali kuweka bayana kilichotokea badala ya kuendelea kusikia taarifa hizo kutoka kwa wapinzani.
Alisema taarifa zilizotolewa na Msemaji wa Serikali haikujitosheleza na akashauri suala hilo lizungumzwe kwa kina na Waziri Mbarawa.     







No comments:

Post a Comment