Monday, August 21

Askofu Malasusa awataka waumini kuhudumia jamii




Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Dk Alex Malasusa amehimiza waumini kujihusisha na huduma za jamii.
Dk Malasusa alitoa wito huo jana wakati wa ibada ya ufunguzi wa Kanisa la KKKT Mtaa wa Misugusugu Usharika wa Mlandizi, Jimbo la Magharibi.
“Tuache utamaduni wa kukaa ndani, tutoke nje na kufanya huduma za jamii kama shule na hospitali kama sehemu ya utume wetu kwa watu wengine,” alisema Dk Malasusa.
Akizungumzia mfuko wa elimu uliozinduliwa hivi karibuni, Katibu Mkuu wa DMP, Geophrey Nkini alisema kanisa limeuanzisha kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia, miundombinu na kukuza viwango vya ufundishaji ili kuibua vipaji maalumu.
Pia, Nkini alisema taasisi za kanisa zinazotoa elimu ambazo zimelengwa kuhudumiwa na mfuko huo ni Sekondari ya Wasichana Mkuza, Kisarawe Junior Seminary, Mbwawa na Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudaco).
Kuhusu utunishaji wa mfuko, Nkini alisema wanatarajia kukusanya Sh1.6 bilioni ifikapo Desemba.
Awali akisoma risala, Mzee wa kanisa hilo, Meja Jenerali mstaafu Samwel Kitundu alisema kazi ya ujenzi wa kanisa hilo umegharimu Sh135 milioni, tofauti na makadirio ya awali ya Sh128 milioni, huku akitaja sababu ya ongezeko hilo kuwa ni kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi.
“Tnashukuru watu mbalimbali waliojitoa kufanikisha kukamilika kwa kazi hii na kufikia hapa,” alisema.
Naye Mtumishi wa kanisa hilo, Edward Mwakalomo aliwashukuru washarika kwa kujitolea kwa kuwa kazi hiyo haikuwa nyepesi, lakini jitihada zao zimeifanya ifanikiwe. Ufunguzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa majimbo, wachungaji, wainjilisti.     

No comments:

Post a Comment