Monday, August 21

Balozi Mwapachu ampata mbwa wake




Mwanadiplomasia wa siku nyingi nchini, Juma Mwapachu sasa atakuwa amejaa tabasamu baada ya mbwa wake aliyekuwa amepotea, kupatikana.
Mwapachu alitoa tangazo la aina yake katika gazeti hili Agosti 15, akieleza kuwa mbwa wake amepotea na kuomba msaada kwa atakayemuona.
Akizungumza na gazeti hili, Mwapachu alisema kuna mtu ambaye alisoma tangazo hilo na kwenda nyumbani kwake na kueleza nia yake ya kumsaidia kumtafuta.
Mwapachu alisema mtu huyo alianza kumsaka mbwa huyo kwenye nyumba za jirani, maeneo ya Mikocheni hadi alipofanikiwa kumkuta Mbezi Beach jijini hapa.
“Alimkuta kwa mtu ambaye alidai ameuziwa na baada ya kumrudisha hapa tulimpa zawadi ya Sh200,000 kama tulivyoahidi kuwa zawadi nono itatolewa,” alisema Mwapachu.
Mwapachu alisema kuna uwezekano mbwa huyo alitoroka nyumbani kupitia matundu yaliyopo katika geti la nyumba yake.
Alisema mbwa huyo alipewa na rafiki yake wa karibu kutoka familia ya marehemu Sir George Kahama, miezi sita iliyopita.
Mwapachu alisema tangu atoe taarifa ya kupotelewa na mbwa huyo, amepokea simu za watu mbalimbali wakionyesha nia ya kumsaidia kumtafuta.
“Rafiki yangu Anna Kahama aliniletea mbwa huyo na alinipa kama zawadi tu. Aliletwa hapa akiwa na miezi mitatu na picha kwenye gazeti ilipigwa akiwa mdogo. Sasa amekua,” alisema Mwapachu.
Tangu kuanza zoezi la kumtafuta mbwa huyo hakikuwekwa wazi kiasi ambacho kingetolewa kwa mtu ambaye angefanikisha kumpata mbwa huyo.   

No comments:

Post a Comment