Wednesday, November 1

PITIA VICHWA VYA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO NOVEMBA MOSI,2017

WAKILI MWALE NA WENZAKE WAZUA TAHARUKI MAHAKAMANI

 

WAKILI Median Mwale na wenzake watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka 44, jana waliibua taharuki mahakamani baada ya kuachiwa huru na kutimua mbio kabla ya kukamatwa na polisi.

Wakili Mwale na wenzake, Don Bosco Gichana raia wa Kenya, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi, waliachiwa huru baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kukubaliana na ombi la Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), la kuondoa shauri la mahakamani.

Baada ya kuachiwa huru, Wakili Mwale na mwenzake walibaini kuwepo kwa polisi waliokuwa wakisubili kuwakamata tena, hivyo waliamua kuwakwepa kwa kutimua mbio tukio ambalo lilizua taharuki katika viunga vya mahakama.
Akisoma uamuzi wa kuwaachia huru Wakili Mwale na wenzake katika kesi ya Jinai namba 61 ya mwaka 2015, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, David Mrango alikubaliana na ombi la DPP lililowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali na kumtaka asiwakamate tena.
Hata hivyo, baada ya Wakili Mwale na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka 44 yakiwamo ya utakatishaji fedha, kughushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu, polisi na askari kanzu waliokuwa mahakamani walianza kuwafuata.
Wakili Mwale na wenzake waliokuwa wameambatana na familia zao na mawakili wanaowatetea baada ya kubaini wanafuatwa walitimua mbio huku polisi wakiwafuata.
Polisi walimkamata kwanza Ndejembi aliyekuwa akishuka ngazi na mkewe ambaye alianza kupiga picha tukio hilo kwa simu yake ya mkononi kabla naye ya kutiwa nguvuni.
Mwale na wenzake wawili walijaribu kuwakimbia polisi kwa kuruka uzio wa jengo la Don Bosco lakini walikamatwa kabla hawajatokomea.
Tukio hilo la askari kanzu, polisi na watuhumiwa kufukuza, lilivuta hisia za mawakili, mahakimu na watu waliokuwa mahakamani hapo na wakati likiendelea polisi waliwaondoa washtakiwa eneo hilo kwa kutumia magari ya polisi yaliyokuwa na namba za usajili T 770 CWT, T 953 CZS aina ya TDI na PT 3766.
Wakili Mwale na wenzake walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mwaka 2011.
NDANI YA MAHAKAMA
Awali, mahakama iliwaachia huru washtakiwa huku ikikubaliana na ombi lililowasilishwa juzi na  mawakili wa utetezi kuwa wasikamatwe tena kwa vile maombi ya DPP yamelenga kuwatesa wateja wao na siyo  mara ya kwanza kwa kesi hiyo kuomba iondolewe.
Jaji Mrango alisema mahakama haina mamlaka ya kukataa maombi ya DDP lakini alisisitiza kuwa endapo wameyawasilisha kwa nia njema shauri hilo liondolewa na washtakiwa wasikamatwe.
Wakili wa utetezi, Albert Msando juzi akiwasilisha pingamizi hilo aliieleza Mahakama kuwa DPP alitakiwa kutoa sababu za kutokuendelea na kesi kwa sababu alikuwa na muda wa miaka miwili kufanya hivyo.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyekomya akisaidiana na mawakili waandamizi, Shadrack Kimaro na Pius Hilla na upande wa utetezi uliongozwa na Wakili Albert Msando akisaidiwa na mawakili Omary Omary, Mosses Mahuna, Innocent Mwanga na Buheri Ngoseki.
Akiwasilisha ombi la DPP mahakamani, Wakili Tibabyekomya alieleza kuwa DPP anaomba chini ya Kifungu cha 91(1) cha mwenendo wa makosa ya jinai kuondoa shauri hilo na kwamba ombi hilo liingizwe kwenye kumbukumbu za mahakama.
Hii ni mara ya pili kwa DPP kuondoa shauri hilo mahakamani, mara ya kwanza ilikuwa Novemba 23, mwaka 2015, ambapo liliondolewa kisha washitakiwa hao walikamatwa na kufunguliwa kesi upya.

LISSU: NYALANDU KARIBU CHADEMA


SIKU moja baada ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, kujivua uanachama wa CCM na nyadhifa zote ndani ya chama hicho, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amemkaribisha ndani ya Chadema.

Lissu ambaye alipigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Dodoma, Septemba 7 mwaka huu, alitoa kauli hiyo jana akiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakotibiwa.

Akizungumza kwa sauti ya kukwaruza akiwa kitandani, Lissu alisema bado Watanzania wanahitaji kufanya uamuzi mgumu kwa kuikataa CCM kupitia uchaguzi wa madiwani unaotarajiwa kufanyika Novemba 26.

“Nimepokea kwa faraja kubwa taarifa ya kujiuzulu kwa Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa jimbo la jirani kwangu Singida Kaskazini, kutoka CCM na maombi yake ya kujiunga na Chadema.

“Nyalandu ameitumikia CCM kama Mbunge wa Singida Kaskazini kwa karibu miaka 20, lakini pamoja na muda wote huo, bado ana mawazo ya ujana, bado ni kijana katika fikra zake, ndiyo maana akapata ujasiri na uthubutu wa kuchukua hatua hii kubwa, ambayo watu wengi wasiopenda kuwa CCM wanashindwa kuchukua, naomba nimpongeze kwa hili,” alisema Lissu.

Pamoja na mambo mengine, Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), aliwataka Watanzania kuwapigia kura wagombea wa udiwani kutoka Chadema na vyama vingine vya Ukawa.

“Naongea nikiwa katika kitanda cha Hospitali ya Nairobi ambapo kama mnavyofahamu, naendelea na matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na wale ambao wamezoea kututesa.

“Ndugu zangu nina ujumbe leo, unaohusu uchaguzi wa marudio wa madiwani, kuna kata 40 zinagombaniwa.

“Kuwapa kura CCM ni sawa kuendelea kuhangaika wakati watu wachache wananufaika. Kwahiyo, ndugu zangu naomba tufanye maamuzi magumu katika uchaguzi huu katika hizi kata 40… Ni kuikataa CCM na kukubali kupiga kura kwa ajili ya wagombea watakaowekwa na Chadema pamoja vyama vingine vya Ukawa.

“Ujumbe huu ni ‘special’ kwa ajili ya wananchi wa Kata ya Siuyu, nawasalimu nyote nikiwa katika Hospitali ya Nairobi, ambako naendelea na matibabu baada ya kupigwa risasi…

“Ujumbe wangu leo kwenu, naomba sana mfahamu hili kwamba nguvu zilezile zilizotumika kumfunga Mahami (aliyekuwa Diwani wa Siuyu Mahami Gerald) na baadaye kumzuia asiendelee na kazi ya udiwani, kazi ambayo mmempa ninyi kwa ushindi mkubwa 2015, ni nguvu hizo hizo ambazo zimenifungulia mashtaka mara nyingi.

“…Naomba wananchi wa Siuyu mchukue hatua bila woga, wala kusitasita, nchi huwa haikombolewi na waoga, bali inakombolewa na wajasiri.

“Naombeni wananchi wa Siuyu mimi ninawafahamu, tumeshinda mara mbili pamoja kwa sababu mmekuwa wajasiri sana, katika uchaguzi huu wa diwani ambaye tumenyang’anywa bila sababu, aliondolewa madarakani bila sababu kwenye hili waonyesheni watu Siuyu wakoje.

“Naomba siku ya uchaguzi kila mzee, kila mama, kila baba, kaka, dada ajitokeze kuhakikisha Mahami Gerald anabaki kuwa diwani wa Siuyu.

“Badala ya mimi kuja kuzungumza nanyi moja kwa moja, nazungumzia kitandani, naomba tuwape fundisho watesi wetu na vilevile tuwape Watanzania fundisho kuwa Siuyu huwa hatuchezewi.

“Nawashukuruni, nawatakia kila la kheri, Mwenyezi Mungu atawalinda na atawapa ushindi wa nguvu,” alisema Lissu.

Mbali na hilo katika ujumbe wake huo wa sauti wa dakika 7, pia alizungumzia bomoabomoa inayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini.

MVUA KUBWA ZATARAJIWA UKANDA YA PWANI


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi wanaoishi maeneo ya ukanda wa pwani kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha kuanzia Octoba 31 hadi Novemba 3, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, maeneo yatakayoathiriwa zaidi na mvua hizo ni mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na visiwa vya Pemba na Unguja.
Taarifa hiyo ilisema kuwa vipindi vya mvua kubwa zinazozidi milimita 50 zinatarajiwa kunyesha ndani ya saa 24. Kiwango cha juu kinakadiliwa kufikia asilimia 80.
“Baadhi ya maeneo ambayo yataathirika ni ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani pamoja visiwa vya Unguja na Pemba.
“Mvua hiyo inatarajiwa kusambaa katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Lindi kuelekea siku ya Ijumaa Novemba 3, mwaka huu,” ilisomeka taarifa hiyo.
Taarifa ilisomeka zaidi kuwa hali hiyo inatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua (Inter Tropical Convergency Zone –ITCZ) katika maeneo hayo.

Kiongozi wa jimbo la Catalonia akubali uchaguzi mpya

 Kiongozi wa jimbo la Catalonia aliyeondolewa madarakani Carles Puigdemont amesema kuwa amekubaliana na hatua ya serikali kuu ya Uhispania kuitisha uchaguzi wa mapema.

Pressekonferenz Puigdemont Brüssel (Reuters/Y. Herman
)
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels Puigdemont amesema alikuwa hatafuti hifadhi ya kisiasa nchini Ubelgiji baada ya mwendesha mashitaka mkuu wa serikali ya Uhispania  kutaka afunguliwe mashitaka ya uasi na uchochezi.
Alipoulizwa na waandishi wa habari ni muda gani anatarajia kusalia Ubeligiji Puigdemont amesema hali inabadilika kila mara nchini Uhispania na kuwa kwa sasa nchini Ubeligiji wamehakikishiwa juu ya haki zao za msingi na kuwa wanatekeleza mipango yao vizuri kutokea nchini humo na kusisitiza kuwa hakwenda Ubeligiji kutafuta hifadhi ya kisiasa  bali ni kwa ajili ya usalama wake na kwa vile Brussels ni makao makuu ya Umoja wa Ulaya na kuongeza kuwa pamoja na kuwa  atarejea nchini mwake baada ya kuhakikishiwa usalama na mazingira huru yeye binafsi pamoja na viongozi wenzake.
Puigdemont amesema pia kuwa atakubaliana  kwa nguvu zote na changamoto  zitakazotokana na uchaguzi wa mapema ulioitishwa Desemba 21 na kusema wananchi wa Catalonia watashiriki uchaguzi huo na kusisitiza kuwa hatua ya serikali ya Uhispania kujaribu kuzuia mchakato wao wa kisiasa haitafanikiwa.
Hatua ya Puigdemont kusema kwamba atakubaliana na  uchaguzi huo wa mapema katika jimbo la Catalonia mnamo Desemba 21 inathibitisha kuwa serikali kuu ya mjini Madrid imepata mafanikio katika juhudi za kukwamisha mchakato wa jimbo hilo kutaka kujitenga.
 Jitihada za jimbo la Catalonia kujaribu kuzuia serikali ya mjini Madrid kutawala moja kwa moja jimbo hilo zimeonekana kugonga mwamba tangu mwanzoni mwa wiki hii na kuifanya iliyokuwa serikali ya jimbo hilo kuwa katika wakati mgumu.
Mahakama ya katiba yazuia tangazo la uhuru wa jimbo la Catalonia
Spanien PK Ministerpräsident Mariano Rajoy in Madrid (Reuters/S. Vera)
Waziri Mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy
Mahakama ya katiba ya Uhispania hii leo imezuia tangazo la uhuru wa jimbo la Catalonia lililotolewa na bunge la jimbo hilo Ijumaa iliyopita hatua ambayo haikudumu na kufutiliwa mbali katika muda usio zidi nusu saa.
" Ninatoa mwito kwa watu wa jimbo la Catalonia kujiandaa kwa mchakato mrefu kufikia demokrasia ambao ndio utakao kuwa msingi wa ushindi wetu" amesema Puidemont.
Serikali ya Uhispania tayari imekwishatamka kuwa Puigdemont anakaribishwa kushiriki katika uchaguzi wa Desemba 21 ulioitishwa na waziri mkuu Mariano Rajoy kama njia moja wapo ya kutatua mkwamo uliopo.
Mgogoro huo wa kisiasa mbaya zaidi kutokea nchini humo katika kipindi cha miongo minne  tangu nchi hiyo irejee katika utawala wa kidemokrasia mwishoni mwa miaka ya 1970 umesababishwa na kura ya maoni iliyofanyika katika jimbo hilo la Catalonia Oktoba 1.
Licha ya kura hiyo ya maoni iliyoitikiwa na watu wasio zidi nusu ya wanaostahili kupiga kura na  kutangazwa na  mahakama ya Uhispania kuwa ni batili  bado iliyokuwa serikali ya jimbo hilo inasisitiza kuwa inalipa mamlaka ya kutangaza uhuru wa jimbo hilo.
Mataifa ya ulaya ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ujerumani na Ufaransa yameungana na waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy na kukataa hatua ya jimbo la Catalonia kujitangazia uhuru ingawa baadhi wametoa mwito wa kufanyika majadiliano kati ya pande hizo mbili.

Mshambuliaji awaua watu 8 kwa kuwagonga kwa gari New York

Marekani
Image captionShambulizi nchini Marekani baisikeli na miili ya watu ilitapakaa ardhini
Meya wa mji wa New York, Bill De Blasio, amearifu kwamba watu 8 wamefariki dunia na zaidi ya 12 wamejeruhiwa na gari iliyowagonga waendesha baiskeli mjini humo.
Bill amelielezea tukio hilo kuwa la ugaidi lililosababisha hofu mjini humo.
Kamishna wa polisi la jiji wa New York, James O'Neill, amemuelezea mtu aliyetekeleza tukio hilo kuwa ni kijana wa miaka 29 aliyekuwa anaendesha gari dogo la kubebea mizigo alilokuwa amelikodisha.
Alisema gari hilo liliwagonga wanaotembea kwa miguu na waendeshaji baiskeli kabla ya kugongana na basi la shule.
Kwa upande wake bwana O'Neill, amesema kuwa dereva wa gari hilo alitoka ndani ya gari lake na kuanza kuandaa silaha mbili kwa ajili ya shambulizi na kabla ya hilo, polisi walimpata na kumpiga risasi zilizomjeruhii.
Marekani
Image captionGari lililosababisha tukio hilo
Polisi mjini humo wametoa tamko kwamba wanalichukulia tukio hilo kama shambulizi la kigaidi . Mtuhumiwa wa tukio hilo alichukuliwa na polisi kwa mahojiano zaidi ambao walithibitisha taarifa hizo katika kituo cha Lower Manhattan.
Vyombo vya habari nchini Marekani vimenukuu taarifa za polisi kuwa kijana huyo aliamua kuendesha gari hilo katika njia ya waendesha baisikeli iliyoko karibu na mto Hudson eneo la Lower Manhattan ya chini ,kabla ya kupigwa risasi na maafisa wa polisi ili kuzuia shambulio alilolipanga.

Mlango wa ndege iliyokuwa angani waangukia nyumba India

The door weighed more than 20kgsHaki miliki ya pichaTELANGANA POLICE
Image captionThe door weighed more than 20kgs
Familia moja nchini India imepigwa na mshangao baada ya mlango wa ndege kuangukia nyumba yao katika mji ulio kusini mwa India wa Hyderabad.
Mwanamume ambaye alikuwa akipaka paa la nyumba rangi aliponea baada ya kwenda kupata chakula cha mchana wakati kisa hicho kilipotokea,
Polisi aliiambia BBC kuwa ndege hiyo ya kubeba abiria wanne ambayo ni ya kutoa mafunzo ilikuwa ikiruka chini chini.
Aliongoza kuwa rabani na mwanafunzi wake wako salama na uchunguzi umeanza kubaini ni vipi kisa hicho kilitokea.
Insepkta wa Polisi Karan Kumar Singh alisema kuwa ni kawaida kuona ndege zikiruka chini chini eneo hilo.
Rubani na mwanafuzi wake waliponea mwezi Septemba wakati ndege kama hiyo ilipoanguka katika eneo hio.

Muuguzi alipwa $0.5m katika kisa cha kukataa mgonjwa kutolewa damu

Nurse Alex Wubbels is shown during an incident at University of Utah Hospital in Salt Lake City, Utah, U.S., in this still photo taken from police body-worn camera video taken July 26, 2017Haki miliki ya pichaPRESS EYE
Muuguzi mmoja ambaye alikamatwa baada ya kukataa kumruhusu polisi kuchukua sampuli ya damu kutoka kwa mgonjwa ambaye alikuwa amepoteza fahamu amekubali kulipwa fidia ya dola 500,000.
Alex Wubbels aliafikia makubaliano hayo na Manisapaa ya mji wa Salt Lake na chuu kikuu cha Utah, kwa mujibu wa wakili wake.
Kukamata kwake na polisi mwezi Julai kulizua ghadhabu baada ya video ya kisa hicho kuibuka baadaye. Anaonekana kuwa na pingu mikononi huku akilazimishwa kuingia katika gari la polisi .
Baadaye aliachiliwa bila ya kushtakiwa. Polisi aliyemkamata alifutwa kazi mwezi uliopita huku mkubwa wake akishushwa madaraka.
Polisi Jeff Payne alitumwa kwenda hospitali ya chuo cha Utah tarehe 26 mwezi Julai kuchukua sampuli ya damu kutoka kwa dereva ambaye alikuwa amehusika kwenye ajali ya barabarani na ambaye alikuwa amepoteza fahamu.
Afisa wa polisi Jeff Payne (kushoto) alifutwa kazi huku mkubwa wake James Tracy, akishushwa madarakaHaki miliki ya pichaSALT LAKE CITY POLICE
Image captionAfisa wa polisi Jeff Payne (kushoto) alifutwa kazi huku mkubwa wake James Tracy, akishushwa madaraka
Mgonjwa hakuwa ameshukiwa kufanya lolote baya.
Bi Wabbels ambaye alikuwa katika zamu wakati huo alimuambia polisi Payne kuwa hakuwa na waranti ya kuchukua sampuli ya damu jinsi inavyohitajika na sera za hospitali na sheria za jimbo.
Pia alisema kuwa damu haingechukuliwa bila ya idhini ya mgonjwa.
Bi Wubbels alikataa kumuambia polisi alikokuwa mgonjwa au kumruhusu kuchukua damu.
Luteni James Tracy kisha akamuamrisha Det Payne kumkamata Bi Wubbels.
Hospitali ya chuo cha Utah baadaye ilisema kwa ilikuwa imeleta sera mpya zinazowazuia polisi kuingia hospitalini wenyewe kuchukua sampuli ya damu.

Odinga apuuza ushindi wa Kenyatta


 Kiongozi wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa) kwa mara ya kwanza tangu Uhuru Kenyatta atangazwe kuwa rais mteule, amepuuza uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26.
Odinga akiwa ameongozana na viongozi wenzake wa muungano huo amesema kura hiyo ni “udanganyifu” na ameapa kutomtambua Kenyatta na serikali yake.
Badala yake amesema Nasa itaweka shinikizo liundwe Baraza la Wananchi kuongoza Kenya hadi uongozi halali utakapochaguliwa na kuundwa.
“Leo hii tunaanzisha Baraza la Wananchi ili lifanye kazi ya kurejesha demokrasia katika nchi hii,” alisema Odinga alipozungumza na wanahabari katika jengo la Okoa Kenya yalipo makao makuu ya chama.
“Baraza la Watu litajumuisha vijana, viongozi wa dini, wachumi na asasi za kiraia.”
Nasa, alisema, itawasilisha mapendekezo yake ya kuundwa kwa Baraza la Wananchi kwenye mabaraza ya kaunti kwa ajili ya kujadili na kuridhia.
“Ratiba ya kuundwa kwa baraza hilo itatolewa hivi karibuni,” alisema.
Katika hatua nyingine, Odinga alisema tawi la Nasa la kuendesha harakati za kukaidi serikali (NRM) litaanzisha kampeni kali za kudai demokrasia kwa kufanya migomo ya kiuchumi na kuweka vigingi.
Odinga alisingizia maandalizi na uendeshaji wa uchaguzi wa marudio akisema kwamba haukukidhi viwango vilivyowekwa kisheria, Katiba na Mahakama ya Juu.
Alisema ni kweli uchaguzi ulisimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kama ilivyoamliwa na Mahakama ya Juu.
Badala yake, alidai serikali kupitia makamanda wa polisi wa kwenye kaunti na wanasiasa wa Jubilee ndio walioteka shughuli yote.

Kiongozi wa Myanmar si kama Robert Mugabe


Nimepata mshawasha wa kuandika maoni haya mafupi baada ya kusoma makala ya sahibu yangu Madaraka Nyerere aliyoiita “Aung San Suu Kyi sio Robert Mugabe” iliyochapishwa ukurasa wa 21 wa gazeti la Jamhuri la Oktoba 24-30 2017 kuhusiana na nchi ya Myanmar.
Nchi ya Myanmar ina jamii kubwa ya waumini wa dini ya Bhudda na Waislamu wachache wa Rohingya. Takriban mwezi sasa zaidi ya Warohingya laki tano wamekimbilia Bangladesh, jirani na nchi hiyo, kukwepa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Serikali ya Myanmar.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo ni Aung San Suu Kyi ambaye alipiganiwa na dunia kama Nelson Mandela, kutokana na madhila aliyoyapata mintarafu harakati zake za kupata demokrasia nchini mwake.
Kutambua mchango wake huo alitunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1991 kama ile aliyotunukiwa Rais Nelson Mandela miaka michache baadaye. Cha ajabu ni kuwa kiongozi huyo amekaa kimya wakati kadhia ya mateso ya raia wake inatokota. Jambo hili lilimfanya mshindi mwingine wa tuzo ya Amani ya Nobel, Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini, kumwandikia barua kumtaka achukue hatua madhubuti kuzuia mateso ya raia wake.
Izingatiwe kuwa waathirika wakubwa wa wakimbizi hao ni wazee, wanawake na watoto. Aung San Suu Kyi mwenyewe ni mwanamke na ana watoto aliowazaa na raia wa Uingereza. Na huwa anajinadi kuzungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha.
Kwa fedheha kubwa Aung San Suu Kyi alishindwa hata kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichomalizika New York nchini Marekani, majuma mawili yaliyopita yumkini kukwepa shutuma kali dhidi yake. Kutokana na hali hii Madaraka Nyerere anasema “... sasa zipo sauti zinapazwa tena kumshutumu na kujenga hoja kuwa anapaswa kunyang’anywa tuzo hiyo.” Lakini anasita kuwa, “Hilo sidhani kama litatokea, labda Suu Kyi angekuwa Robert Mugabe.”
Jumuiya za kimataifa
Ikumbukwe kuwa juma lililopita Shirika la Afya Duniani lilimteua Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kama Balozi wake wa Heshima. Uteuzi huo ulipingwa na mataifa yote makubwa na kushinikiza uteuzi huo ufutwe. Na kweli mapema wiki hii Rais Mugabe akavuliwa ubalozi wake wa heshima.
Kwa bahati mbaya mno dunia yote sasa imezingwa na ubaguzi wa rangi na dini. Hata mateso ya Warohingya yanaelezwa vyema zaidi na Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, nchi yenye Waislamu wengi, kuliko nyingine yoyote duniani. Tarehe 19 Oktoba 2017, Televisheni ya Al Jazeera, katika kipindi mashuhuri “The Stream” kilimwonyesha mwanahabari wake nguli Mohamed Jamjoon akitoa ushuhuda wa madhila ya Warohingya.
Yeye na mpiga picha wake walikuwa wanafuta machozi wakielezea namna mtoto wa miezi sita alivyochomwa moto na wanajeshi wa Myanmar na kumuacha na jeraha kubwa kichwani likizingirwa na nzi. Kwa kukosa dawa mama yake alibaki kumpepea mwanaye kichwani kusaka nzi na kumpunguzia maumivu.
Kaifa mbaya zaidi ni ile ya mwanamke wa miaka ishirini ambaye aliteswa na kubakwa, mama yake aliuawa na mtoto wake akafa baada ya kutupwa motoni na wanajeshi wa Myanmar. Ni jahili tu ambaye hawezi kulengwa na machozi kusikia kahati kama hii. Inakuwaje Aung Sun Suu Kyi anakosa utu kiasi hiki!
Hadi leo, Umoja wa Mataifa, hasa Baraza la Usalama hawajachukua hatua zozote madhubuti kuwahami Warohingya. Hivi karibuni tu ndio Katibu Mkuu wa umoja huo pamoja na mashirika ya kimataifa machache yameamua kuamka.
Juzi tu kulifanyika Mkutano wa Wahisani, Paris, Ufaransa katika jitihada za kuwasaidia Warohingya. Na hivi karibuni Serikali ya Bangladesh ilifikia makubaliano na Myanmar kuwarejesha wakimbizi hao Myanmar.
Yumkin Bangladesh ambayo ni nchi maskini inaelemewa na mzigo wa hali na mali wa wakimbizi hao na inapenda warejee makwao haraka iwezekanavyo. Lakini, masharti ambayo Myanmar imeyaweka hayatekelezeki na hali ya usalama nchini Myanmar ni mbaya kiasi kwamba idadi ya wakimbizi inaongezeka kila uchao.
Unafiki wa jumuiya ya kimataifa umeonekana mara nyingi. Kwa mfano, pale majeshi yalipotumwa kuisaidia East Timor kwa madai ya kuvamiwa na Indonesia miongo miwili iliyopita. Takriban wakazi wote wa East Timor ni Wakristo na wale wa Indonesia ni Waislamu.
Majanga mengine
Katika majanga makubwa hoja sio kutoa msaada, bali msaada huo lazima utolewe haraka. Mauaji yaliyofanywa na Israel katika kijiji cha Shatila, Lebanon miaka ya themanini; au yale yaliyofanywa Bosnia Hecegovina hususan katika mji wa Szebrenitza na Serikali ya Slobodan Milosovic wa Serbia mwaka 1995 ; au yale ya Rwanda na hata Gaza, Palestina yaliyofanywa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, mwaka 2014 yangeweza kuzuilika au kupunguzwa mapema na jumuiya ya kimataifa.
Jumuiya ya kimataifa inachagua kuchukua hatua za dharura kusaidia kutokana na silka ya waathirika wenyewe. Aidha inatoa shutuma nzito mapema kutokana na silka ya wahusika wenyewe. Mathalan ni mazoea kulaumu “Magaidi wa Kisilamu.” Hatujui magaidi walioua watu katika tamasha la muziki jijini Manchester, Uingereza au pale Miami, Florida, Marekani watapewa lakabu gani!
Katika muktadha huu naungana na Madaraka Nyerere kuwa sio rahisi kumnyang’anya Aung San Suu Kyi tuzo yake ya Amani ya Nobel kama ambavyo ingekuwa kwa Rais Robert Mugabe.
Profesa Abdallah Saffari
Dar es Salaam
0754- 262623