Kiongozi wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa) kwa mara ya kwanza tangu Uhuru Kenyatta atangazwe kuwa rais mteule, amepuuza uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26.
Odinga akiwa ameongozana na viongozi wenzake wa muungano huo amesema kura hiyo ni “udanganyifu” na ameapa kutomtambua Kenyatta na serikali yake.
Badala yake amesema Nasa itaweka shinikizo liundwe Baraza la Wananchi kuongoza Kenya hadi uongozi halali utakapochaguliwa na kuundwa.
“Leo hii tunaanzisha Baraza la Wananchi ili lifanye kazi ya kurejesha demokrasia katika nchi hii,” alisema Odinga alipozungumza na wanahabari katika jengo la Okoa Kenya yalipo makao makuu ya chama.
“Baraza la Watu litajumuisha vijana, viongozi wa dini, wachumi na asasi za kiraia.”
Nasa, alisema, itawasilisha mapendekezo yake ya kuundwa kwa Baraza la Wananchi kwenye mabaraza ya kaunti kwa ajili ya kujadili na kuridhia.
“Ratiba ya kuundwa kwa baraza hilo itatolewa hivi karibuni,” alisema.
Katika hatua nyingine, Odinga alisema tawi la Nasa la kuendesha harakati za kukaidi serikali (NRM) litaanzisha kampeni kali za kudai demokrasia kwa kufanya migomo ya kiuchumi na kuweka vigingi.
Odinga alisingizia maandalizi na uendeshaji wa uchaguzi wa marudio akisema kwamba haukukidhi viwango vilivyowekwa kisheria, Katiba na Mahakama ya Juu.
Alisema ni kweli uchaguzi ulisimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kama ilivyoamliwa na Mahakama ya Juu.
Badala yake, alidai serikali kupitia makamanda wa polisi wa kwenye kaunti na wanasiasa wa Jubilee ndio walioteka shughuli yote.
No comments:
Post a Comment