Nchi ya Myanmar ina jamii kubwa ya waumini wa dini ya Bhudda na Waislamu wachache wa Rohingya. Takriban mwezi sasa zaidi ya Warohingya laki tano wamekimbilia Bangladesh, jirani na nchi hiyo, kukwepa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Serikali ya Myanmar.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo ni Aung San Suu Kyi ambaye alipiganiwa na dunia kama Nelson Mandela, kutokana na madhila aliyoyapata mintarafu harakati zake za kupata demokrasia nchini mwake.
Kutambua mchango wake huo alitunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1991 kama ile aliyotunukiwa Rais Nelson Mandela miaka michache baadaye. Cha ajabu ni kuwa kiongozi huyo amekaa kimya wakati kadhia ya mateso ya raia wake inatokota. Jambo hili lilimfanya mshindi mwingine wa tuzo ya Amani ya Nobel, Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini, kumwandikia barua kumtaka achukue hatua madhubuti kuzuia mateso ya raia wake.
Izingatiwe kuwa waathirika wakubwa wa wakimbizi hao ni wazee, wanawake na watoto. Aung San Suu Kyi mwenyewe ni mwanamke na ana watoto aliowazaa na raia wa Uingereza. Na huwa anajinadi kuzungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha.
Kwa fedheha kubwa Aung San Suu Kyi alishindwa hata kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichomalizika New York nchini Marekani, majuma mawili yaliyopita yumkini kukwepa shutuma kali dhidi yake. Kutokana na hali hii Madaraka Nyerere anasema “... sasa zipo sauti zinapazwa tena kumshutumu na kujenga hoja kuwa anapaswa kunyang’anywa tuzo hiyo.” Lakini anasita kuwa, “Hilo sidhani kama litatokea, labda Suu Kyi angekuwa Robert Mugabe.”
Jumuiya za kimataifa
Ikumbukwe kuwa juma lililopita Shirika la Afya Duniani lilimteua Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kama Balozi wake wa Heshima. Uteuzi huo ulipingwa na mataifa yote makubwa na kushinikiza uteuzi huo ufutwe. Na kweli mapema wiki hii Rais Mugabe akavuliwa ubalozi wake wa heshima.
Kwa bahati mbaya mno dunia yote sasa imezingwa na ubaguzi wa rangi na dini. Hata mateso ya Warohingya yanaelezwa vyema zaidi na Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, nchi yenye Waislamu wengi, kuliko nyingine yoyote duniani. Tarehe 19 Oktoba 2017, Televisheni ya Al Jazeera, katika kipindi mashuhuri “The Stream” kilimwonyesha mwanahabari wake nguli Mohamed Jamjoon akitoa ushuhuda wa madhila ya Warohingya.
Yeye na mpiga picha wake walikuwa wanafuta machozi wakielezea namna mtoto wa miezi sita alivyochomwa moto na wanajeshi wa Myanmar na kumuacha na jeraha kubwa kichwani likizingirwa na nzi. Kwa kukosa dawa mama yake alibaki kumpepea mwanaye kichwani kusaka nzi na kumpunguzia maumivu.
Kaifa mbaya zaidi ni ile ya mwanamke wa miaka ishirini ambaye aliteswa na kubakwa, mama yake aliuawa na mtoto wake akafa baada ya kutupwa motoni na wanajeshi wa Myanmar. Ni jahili tu ambaye hawezi kulengwa na machozi kusikia kahati kama hii. Inakuwaje Aung Sun Suu Kyi anakosa utu kiasi hiki!
Hadi leo, Umoja wa Mataifa, hasa Baraza la Usalama hawajachukua hatua zozote madhubuti kuwahami Warohingya. Hivi karibuni tu ndio Katibu Mkuu wa umoja huo pamoja na mashirika ya kimataifa machache yameamua kuamka.
Juzi tu kulifanyika Mkutano wa Wahisani, Paris, Ufaransa katika jitihada za kuwasaidia Warohingya. Na hivi karibuni Serikali ya Bangladesh ilifikia makubaliano na Myanmar kuwarejesha wakimbizi hao Myanmar.
Yumkin Bangladesh ambayo ni nchi maskini inaelemewa na mzigo wa hali na mali wa wakimbizi hao na inapenda warejee makwao haraka iwezekanavyo. Lakini, masharti ambayo Myanmar imeyaweka hayatekelezeki na hali ya usalama nchini Myanmar ni mbaya kiasi kwamba idadi ya wakimbizi inaongezeka kila uchao.
Unafiki wa jumuiya ya kimataifa umeonekana mara nyingi. Kwa mfano, pale majeshi yalipotumwa kuisaidia East Timor kwa madai ya kuvamiwa na Indonesia miongo miwili iliyopita. Takriban wakazi wote wa East Timor ni Wakristo na wale wa Indonesia ni Waislamu.
Majanga mengine
Katika majanga makubwa hoja sio kutoa msaada, bali msaada huo lazima utolewe haraka. Mauaji yaliyofanywa na Israel katika kijiji cha Shatila, Lebanon miaka ya themanini; au yale yaliyofanywa Bosnia Hecegovina hususan katika mji wa Szebrenitza na Serikali ya Slobodan Milosovic wa Serbia mwaka 1995 ; au yale ya Rwanda na hata Gaza, Palestina yaliyofanywa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, mwaka 2014 yangeweza kuzuilika au kupunguzwa mapema na jumuiya ya kimataifa.
Jumuiya ya kimataifa inachagua kuchukua hatua za dharura kusaidia kutokana na silka ya waathirika wenyewe. Aidha inatoa shutuma nzito mapema kutokana na silka ya wahusika wenyewe. Mathalan ni mazoea kulaumu “Magaidi wa Kisilamu.” Hatujui magaidi walioua watu katika tamasha la muziki jijini Manchester, Uingereza au pale Miami, Florida, Marekani watapewa lakabu gani!
Katika muktadha huu naungana na Madaraka Nyerere kuwa sio rahisi kumnyang’anya Aung San Suu Kyi tuzo yake ya Amani ya Nobel kama ambavyo ingekuwa kwa Rais Robert Mugabe.
Profesa Abdallah Saffari
Dar es Salaam
0754- 262623
No comments:
Post a Comment