Thursday, September 28

PROF. MAGHEMBE AONGOZA MAADHIMISHO YA 87 YA SIKU YA TAIFA LA SAUDI ARABIA JIJINI DAR ES SALAAM



Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Tanzania wakati wa maadhimisho ya siku ya 87 ya Taifa la Kifalme la Saudi Arabia yaliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam. Prof. Maghembe alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo. Kulia ni Balozi wa taifa hilo nchini Tanzania, Balozi Mohammed Bin Mansour Al Malik.



 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (katikati), Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mohammed Bin Mansour Al Malik (wa pili kulia) na viongozi wengine wa ubalozi huo wakijiandaa kukata keki ya maadhimisho hayo.



 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto), Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mohammed Bin Mansour Al Malik (katikati) na viongozi wengine wa ubalozi huo wakikata keki ya maadhimisho hayo.



Baadhi ya watoto wa Taifa la Kifalme la Saudi Arabia wakiinua bendera ya nchi hiyo kuashiria maadhimisho ya siku ya 87 ya Taifa hilo yaliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI AWAOMBA WANANCHI WANAOISHI MIPAKANI KUTOA TAARIFA ZA WAHAMIAJI HARAMU KWENYE VYOMBO VYA DOLA


 Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Dk. Anna P. Makakala wa kwanza kutoka kushoto  akikagua vichochoro  vinavyotumiwa na wahamiaji haramu kuingia nchini katika kijiji cha  Mugulika  Kata ya Bwerenyange  wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera. Kamishna Jenerali yuko mkoa wa Kagera kujionea shughuli zinazotekelezwa na Idara yake mkoani humo.



 Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Dk. Anna P. Makakala wa kwanza kutoka kushoto  akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera  Godfrey Mheluka watatu kutoka kulia  katika kijiji cha Muguluka  Kata ya  Bwerenyange  wilaya ya Karagwe  Mkoa wa Kagera.Kamishna Jenerali huyo amefanya ziara katika Vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji haramu kutoka nchini nyingine kuingia Tanzania.



 Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Dk. Anna P. Makakala wa nne kutoka kulia akiwa katika Mkutano wa Hadhara na baadhi ya Wananchi (hawapo pichani) wa Kijiji cha Muguluka Kata ya Bwerenyange wilaya ya Karagwe  Mkoa wa  Kagera.Kamishna Jenerali huyo amefanya ziara katika Vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji haramu kutoka nchini nyingine kuingia Tanzania.



Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Muguluka Kata ya Bwerenyange wilaya ya Karagwe  Mkoa wa  Kagera wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Dk. Anna P. Makakala katika Mkutano wa Hadhara baina ya wanakijiji hao na Ujumbe huo wa Idara ya Uhamiaji kutoka Makao Makuu ambapo katika Mkutano huo Dk. Makakala  alitoa wito  kwa  wanakijiji hao  kutowahifadhi wahamiaji haramu  kwenye makazi yao sambamba na kuwataka kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola pale wanapogundua kuna mgeni asiyeeleweka na wanamtilia mashaka kwenye makazi yao.(Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)

Jared Kushner 'amesajiliwa kama mpiga kura mwanamke'

Jared KushnerHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionJared Kushner ametajwa kuwa mtu mwenye umri wa miaka 36 mwenye ushawishi mkubwa duniani
Mkwe wa Donald Trump amesajiliwa kupiga kura kama mwanamke kwa miaka 8, inadaiwa.
Jinsia yake imesajiliwa kama "mwanamke" katika rekodi kutoka bodi ya uchaguzi jimboni New York, kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye mtandao wa Wired.
Picha za usajili wake zinaashiria kuwa Kushner, ambaye ni mshauri mkuu wa rais alijisajili kupiga kura Novemba 2009.
Mpaka sasa hajatoa tamko lolote kuhusu hilo, kwahivyo haijulikani wazi ni vipi makosa hayo yalitokea .
Huenda makosa hayo hayawezi kuchukuliwa kuwa ya udanganyifu, kwasababu hilo linahitaji mshukiwa kutoa kwa makusudi taarifa za uongo.
Rais Trump alizungumza kwa mbwembwe kuhusu suala hilo baada ya uchaguzi mkuu 2016 akituma ujumbe kwenye Twitter kwamba "mamilioni ya watu walipiga kura kiharamu", pasi kutoa ushahidi wowote.

Mwanzilishi wa jarida la Playboy aaga dunia

Muanzilishi wa jarida la Playboy Hugh HefnerHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionHugh Hefner alifariki kwa amani nyumbani kwake
Hugh Hefner, mwanzilishi wa jarida la kimataifa la watu wazima - Playboy, amefariki akiwa na umri wa miaka 91.
Playboy Enterprises Inc imesema alifariki kwa amani nyumbani .
Hefner alianza kuchapisha jarida hilo jikoni nyumbani mwake mnamo 1953. Likawa jarida linalo uzika zaidi la wanaume duniani.
Cooper Hefner, mwanawe amesema "atakumbukwa kwa ukubwa na wengi".
Alimtaja babake kama "Mojawapo ya watu wa kwanza kujitosa katika uandishi na aliishi maisha ya aina yake na yenye utofuati," na amemuita mtu anayetetea uhuru wa kuzungumza, haki za kiraia na uhuru wa kijinsia.
Mnamo 2012, akiwa na umri wa 86, alimuoa mke wake wa tatu Crystal Harris - ambaye alikuwa mdogo wake kwa miaka 60.
Hugh Hefner Crystal Harris, 2011Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionMkewe wa wa tatu Crystal Harris anamrithi
Jarida la Hefner lilichangia kile kinachoonekana kuwa kuheshimiwa kwa picha za utupu katika vyombo vya habari na hilo lilimtajirisha na kumfanya kuwa milionea.
Ufanisi wake ukamuezesha kufungua maenoe ya kucheza kamari na vilabu vya burudani.
Tajiri huyo aliyeonekana mara nyingi akivaa nguo za hariri, aliishi maisha ya starehe, akiwachumbia na kuwaoa wanamitindo wanaopigwa picha katika jarida hilo .
Katika miaka yake ya baadaye alifurahikia kuandaa tamasha kubwa na mikusanyiko ya starehe katika majumba yake ya kifaharai.
Anadai kulala na zaidi ya wanawake 1000 na amesifia nguvu zake kwa dawa za kuongeza nguvu za kiume Viagra.

Myanmar yafutilia mbali ziara ya Umoja wa mataifa Rakhine

Jimbo la Rakhine limedhibitiwa vikaliHaki miliki ya pichaEPA
Image captionJimbo la Rakhine limedhibitiwa vikali
Umoja wa mataifa unasema kuwa, utawala wa Burma umefutilia mbali mipango ya Umoja huo kuzuru jimbo la Rakhine nchini Myanmar.
Hilo ni eneo ambalo kulishuhudiwa idadi kubwa zaidi ya watu wa jamii ndogo ya waislamu Wa- Rohingya, waliotoroka makaazi yao kuepuka mapigano.
Msemaji wa Umoja wa mataifa huko Yangon, Stanislav Saling, ameiambia BBC kuwa hakuna sababu zozote ambazo zilitolewa kuhusiana na hatua ya kuwazuia maafisa wa Umoja wa mataifa kuzuru maeneo hayo.
Umoja wa mataifa umekuwa ukishinikiza kuruhusiwa kulizuru jimbo hilo la Rakhine, ili kupeleleza kiini cha Warohingya hao kuhama kwa wingi kutoka maeneo hayo, kuanzia mapema mwezi uliopita.
Makumi kwa maelfu ya waislamu, Wabudha na Wahindu wanaishi katika majengo ya muda katika jimbo hilo la Rakhine tangu kuanza kwa mashambulio yaliyokuwa yakitekelezwa na warohingya wenye itikadi kali.
Hatua iliyosababisha Jeshi la Myanmar kuanza kuwashambulia Warohingya.

NATO imekiri shambulio la Marekani Kabul liliwadhuru raia

NATO imekiri kwamba shambulio la anga la majeshi ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Kabul
Image captionNATO imekiri kwamba shambulio la anga la majeshi ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Kabul
NATO imekiri kwamba shambulio la anga la majeshi ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Kabul, wakati wa ziara ya waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis ulisababisha madhara kwa raia.
NATO wanasema kuwa kombora lilishindwa kulipuka,jambo wanalosema lilisababisha usumbufu mkubwa kwa watu wasio wanajeshi.
Serikali ya Afghanistan inasema kuwa mtu mmoja alikufa na wengine saba kujeruhiwa.Shambulio hilo lilifanyika katika kuwakabili washambuliaji wa kujitoa muhanga waliokuwa katika uwanja wa ndege wakiwa wamevalia vifaa vya kujilipua.

Punguzo la kodi litaleta nafuu: Donald Trump

TrumpHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionRais Donald Trump has ametangaza kile anachokiita punguzo kubwa la kodi
Rais Donald Trump ametangaza kile anachokiita punguzo kubwa la kodi kuwahi kutokea katika historia ya taifa hilo. Amesema anahitaji mfumo rahisi na wa wazi wa kodi ili kurejesha ajira na utajiri ndani ya taifa hilo.
Trump ametangaza kupunguza kodi kwenye biashara na amesisitiza kuwa ataondoa kodi ya urithi. Amesema wafanyakazi wanawake kwa wanaume ndiyo watakao nufaika na hatua yake hiyo na si wale wenye mapato makubwa.
"Mfumo wetu mpya unalenga mabadiliko ambayo,yatamlinda mtu wa kipato cha chini , cha kati na katika ngazi ya kaya siyo kwa matajiri.
Wataniita kwa majina yoyote wapendayo, lakini haitasaidia. Ninafanya mambo ya haki na si kwa manufaa yangu mwenyewe.Naomba mniamini."
Hatua hii ni kutekeleza mapendekezo ya chama chake cha Republicans, huku Democrats wakiwa na maoni tofauti kwamba mabadiliko hayo yataziumiza familia zenye kipato cha kati na kupunguza kipato chao hasa wajane na watoto.

Wabunge watwangana makonde Uganda

UgandaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWabunge nchini Uganda wamepigana ndani ya ukumbi wa bunge
Wabunge nchini Uganda wamepigana ndani ya ukumbi wa bunge wakiwa katika siku ya pili ya kikao cha kujadili wa muswada wa kuondoa ukomo wa miaka ya kugombea nafasi ya urais kwa mjibu wa katiba ya taifa hilo.
Katika ugomvi huo wabunge hao walirushiana viti, kuharibu vipaza sauti na katika kikao hicho kilichoongozwa na Spika wa bunge, Bi.Rebecca Kadaga.
UgandaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWabunge watwangana makonde ukumbini
UgandaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWabunge wapambana
Ugomvi huo ulianza pale Spika alipochukua hatua ya kuwafukuza wabunge wapatao 25 wengi wao wakiwa ni wale wa upinzani kwa madai ya utovu wa nidhamu pamoja na waziri wa serikali aliyeshtakiwa kwa kufyatua risasi bungeni siku ya jumanne.
Wabunge hawa wanadai kuwa kama kikomo cha umri wa miaka 75 kitaondolewa basi rais aliyepo kwa sasa atapata mwanya wa kugombea tena mwaka 2021.

KUZA FURSA : Ukiisimamia vyema, biashara itakua kila mwaka



Ally  Mbuyu
Ally  Mbuyu 
Wengi wanapenda kumiliki biashara. wachache wanathubutu kuanzisha na kuziendeleza. Wachache zaidi wanavumilia changamoto zilizopo kwenye biashara walizozianzisha.
Muda wote biashara inatakiwa kukua nakushikiria kasi ya ukuaji kwa kutatua vikwazo vilivyopo na kuangalia mwenendo huo kwa siku zijazo.
Ili kuendelea kukua, mjasiriamali anatakiwa kutafakari mwenendo wa biashara yake na kuweka dira kwa miaka kadhaa ijayo. Namna ya kutafakari ni kama vile unapokuwa juu ya ndege angani na ukaangalia chini, utaona ardhi na vilivyo jinsi vilivyokaa. Muonekano huo hutaweza kuuona ukiwa umesimama ardhini.
Hivyo dira na mipango itawekwa kwa jinsi mjasiriamali anavyoiona biashara yake itakavyokuwa miaka, mfano mitano ijayo. Hivyo kuweka mikakati itakayowezesha kufikia malengo hayo inajumuisha kuwafunza wafanyakazi mbinu mpya za kuhudumia wateja, kushirikiana katika kazi na kutatua changamoto kwa usahihi na umakini bila kuathiri biashara na wateja.
Dira na mikakati itasaidia kukabiliana na mabadiliko, kuwa imara katika kipindi cha mpito kabla ya kufikia malengo na kufanyia kazi fursa mpya zitakazojitokeza.
Katika kutafakari na kuandaa dira ya biashara inashauriwa kuzingatia mambo kadhaa ili kuwa na uhakika wa kufikia malengo yaliyokusudiwa. Muundo wa kampuni kwa siku zijazo ni miongoni mwa vitu hivyo.
Mipango, dira na mikakati ya kukuza biashara lazima iangalie muundo wa biashara yako kwa maana ya idadi ya wafanyakazi waliopo na watakaohitajika ili kuongeza nguvu ya fikra na utaalam kwa siku zijazo. Kuupanga upya muundo wa uongozi ambao utawezesha mafanikio yajayo na kwa muda mahsusi.
Kufikia malengo mazingira rafiki ya kila idara katika kampuni ama biashara yanahitajika. Wafanyakazi wanatakiwa kujituma kwa kufanya kazi bila uzembe wala kutegea. Hii itasaidia kupata matokeo yaliyokusudiwa kwa urahisi.
Mazingira hayo yanaweza kuhusisha kuwazawadia wafanyakazi, kuweka malengo kwa kila idara, kupanga semina na mafunzo ya kukabili mabadiliko ya kampuni, biashara, masoko na utandawazi utakaowawezesha wafanyakazi kujua mwelekeo wa kampuni yao kikamilifu.
Matumizi ya teknolojia ni suala lisiloepukika kwa biashara za zama hizi. Mjasiriamali anapaswa kujua matumizi mbalimbali ya teknolojia kwa kuongeza tija na kupanua uendeshaji wa biashara yake.
Teknolojia hutumika kwenye program za hesabu ambazo zinazosaidia kuokoa muda. Zipo pia program za kusimamia kalenda ya kazi ya kampuni na wafanyakazi pamoja na za kupokea na kupangilia baruapepe za kampuni.
Ni muhimu kuangalia, kupanga na kuamua ni aina gani ya teknolojia inatakiwa katika biashara na utaalamu wa wafanyakazi ili kuleta ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mkakati mwingine wa kukuza biashara ni kufungua matawi katika maeneo mengine kama vile wilaya, mikoa, kanda na nchi jirani kutegemea ukubwa na nguvu ya kampuni na biashara husika. Njia hii inatakiwa kuwa na uhakika wa soko unakotarajia kufungua matawi ili kuepuka hasara. Masoko yakiwa ya uhakika yatasaidia kampuni kukua kwa kuwa na soko pana na kuuza zaidi.
Kunapokuwa na haja iliyojadiliwa kwa kina, unaweza kuchukua mkopo kutoka katika taasisi za fedha zinazo aminika.Wataalamu wa fedha wanahitajika kufanya upembuzi sahihi ili kuona uhitaji wa mkopo, uwezo wa kuusimamia, kiasi na uwezo wa kulipa bila kusahau faida ya mkopo katika uzalishaji.
Mjasiriamali anatakiwa kupiga hatua ya maendeleo kwa kukuza biashara yake mwaka hadi mwaka. Biashara inayokaa muda mrefu bila kukua ina tatizo katika uendeshaji na usimamizi. Ni muhimu kuonana na wataalam na kupata ushauri utakaosaidia kukabiliana na changamoto ulizonazo.

Changamoto wachimbaji wadogo wa dhahabu zishughulikiwe kuimarisha uchumi


Wakati serikali ikiweka mazingira ya kulinda rasilimali za taifa hasa madini, wananchi wanapaswa kujiandaa kunufaika na fursa kede zilizopo kwenye sekta hiyo kwa kuondoa changamoto zilizopo.
Tanzania immebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali maeneo mengi nchini lakini teknolojia ya kuyachimba, kuyachenjua mpaka kuyasafisha na kuyauza yamekuwa ni mambo yanakwaza kushamiri kwa sekta hiyo.
Wachimbaji wakubwa, wengi wakitoka nje ya nchi wamekuwa ndiyo wanufaikaji wakubwa wa madini yaliyopo nchini. Tangu uwekezaji ulipoanza mwanzoni mwa miaka ya 1990, kampuni zilizokaribishwa hazijalipa kodi kama ilivyotakiwa ili kuiongezea serikali mapato.
Licha ya migogoro kadhaa iliyoripotiwa kati ya wachimbaji hao wakubwa na wananchi au halmashauri za maeneo ilipo migodi yao, hakuna la kujivunia ambalo Tanzania linalo kutokana na udanganyifu na wizi unaofanywa na wahusika kwa kushirikiana na maofisa wa umma wasio waaminifu.
Walau kwenye migodi midogo ambako wachimbaji wadogo wameshamiri, manufaa yanaonekana kutokana na kuimarika kwa kipato cha wananchi na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha.
Kutokana na kupotea kwa rasirimali zinazowanufaisha wageni, Bunge la Bajeti mwaka huu lilifanya mabadiliko ya sheria tatu huku rai ikitolewa kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kuendeleza uchimbaji endapo wachimbaji wakubwa wataamua kuondoka.
Yapo mambo kadhaa yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini ili kupunguza athari za kimaadili, kiuchumi na kijamii kwenye maeneo yenye wachimbaji wadogo kama ilivyoshuhudiwa wilayani Chunya.
Halmashauri hii iliyopo mkoani Mbeya ni miongoni mwa wilaya zenye hazina ya madini ya dhahabu ambayo takwimu za mwaka 2016/2017 zinaonyesha kilo 546.59 zilizalishwa.
Watoto
Katika machimbo yaliyopo kwenye Kitongoji cha Itumbi Kata ya Matundas wilayani humo, makundi ya watoto kati ya watano mpaka 15 wenye na umri wa kuanzia miaka 7 hadi 17 wanajihusisha na uchimbaji wa dhahabu migodini kinyume na kifungu cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
Sheria hiyo inasema ni makosa kumuajiri mtoto mwenye chini ya miaka 18 kwenye kazi za baharini, kwenye, kubeba mizigo mizito au kufanya kazi zinazotumia tumia kemikali au mitambo na kwenye vilabu vya pombe.
Licha ya faida za machimbo yaliyopo ndani ya Mamlaka ya Mji mdogo Makongolosi wenye wakazi 4,000, watoto wadogo wanahusishwa kwenye shughuli zote hivyo kuwaathiri kwa namna moja au nyingine.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini watoto hao wanatumia nyundo na vipande vya chuma kuponda, kupunguza ukubwa wa mawe mpaka inchi moja kabla ya kutumbukizwa kwenye karasha kuyasaga ili kupata vumbi au unga wake.
Watoto hao hufanya shughuli hizo bila kuvaa glovu mikononi, kofia ngumu wala viatu vya kujikinga na madhira ya kujikwaa au kudondokewa na vitu vizito. Hawana miwani ya kukinga macho dhidi ya vipande vya mawe vinavyoruka yanapopondwa pia.
Mazingira haya huwasababishia majeraha, ulemavu hata vifo kukichangiwa na kukosekana huduma ya kwanza kwa kuzingatia ukweli kwamba kituo cha afya kipo kilomita 13 kutoka Itumbi.
Ukiacha kuhatarisha afya zao, watoto hawa wanabeba viroba vya mawe vye kati ya kilo 50 mpaka 60 na kuyasogeza kwenye mashine za kuyasaga hivyo kujiweka kwenye hatari ya kutokua vizuri kwa misuli na mifupa yao.
Watoto hao wanachanganyika na watu wazima wanaojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu pasipo jamii inayozunguka maeneo hayo kuchukua hatua zozote kudhibiti hali hiyo inayoweza kusababisha athari za kiafya, kisaikolojia huku wakikosa haki zao za msingi ikiwamo elimu.
Mratibu Elimu Kata ya Matundas (MEK), Ayubu Mwangosi anasema watoto wengi kuhusika kwenye machimbo ya dhahabu kunarudisha nyuma maendeleo ya elimu kiasi cha kuathiri matokeo ya shule za msingi na sekondari. Anasema kwa miaka mitatu mfululizo, tangu mwaka 204, wastani wa matokeo kwa kwa shule za msingi Itumbi na Matundasi si wa kuridhisha.
“Ufaulu katika Shule ya Msingi Matindasi mwaka 2014 ulikuwa asilimia 46 ambao ulishuka mpaka asilimia 43 mwaka 2015. Ingawa uliongezeka mpaka asilimia 45 mwaka 2016 bado ni chini ya asilimia 50,” anasema.
Kemikali
Pamoja na kazi ya uchimbaji madini kuwa na misukosuko mingi na hatarishi kiafya na kisaikolojia, bado watoto hao wanashirikishwa kwenye kuchimba mawe kwa kutumua sululu, kuyaponda kwa nyundo na kuyasaga kwenye makarasha kisha kutenganisha udongo na dhahabu kwa kutumia kemikali ya zebaki na cynate bila kuvaa vifaa ya usalama.
Katika uchorongaji, wachimbaji wadogo hutumia baruti kulipua miamba kabla hawajaingia ndani ya mashimo kukusanya mawe mashimoni ambako huvuta hewa inayoweza kuathiri afya zao hasa mapafu na figo.
Zebaki hutumika kutenganisha dhahabu na mchanga ila kutokana na ukosefu wa ufahamu juu ya madhara yake, hakuna tahadhari inayochukuliwa na wachimbaji hawa hivyo kujiweka kwenye hatari ya kuvuta vumbi au mvuke wake au kuila baada ya kushika chakula na kukiweka mdomoni kabla ya kunawa kwa sabuni na maji safi.
Ofisa Afya na Mazingira Wilaya ya Chunya, Yohana Ngulukia anasema kemikali hiyo huweza kusababisha magonjwa ya ini, figo, matatizo ya moyo, mapafu, macho, ngozi hata kuathiri mfumo wa fahamu na kuchangia mtindio wa ubongo.
“Vumbi la mawe huweza kusababisha kifua kikuu wakati zebaki huchangia ugonjwa ini. Hii ni hatari zaidi kwa watoto kutokana na shughuli hiyo,” anasema Ngulukia.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo, Reuben Mwakilima anasema machimbo hayo yamechangia ongezeko la magonjwa. Mwaka jana, anasema kulikuwa na wagonjwa 567 wa kifua kikuu na kati yao, 29 pamoja na watoto wawili walitoka Kata ya Matundasi.
“Hao ni waliofika hospitali na kugundulika na matatizo hayo lakini kuna idadi kubwa zaidi maeneo ya vijijini kutokana na uchimbaji madini usiozingatia afya na usalama mahala pa kazi,” anasema Mwakilima.
Elimu
Shule zilizopo maeneo ya machimbo hayo zinaelezwa kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi ambao mahudhurio yao si mazuri kutokana na watoto wengi kujihusisha na shughuli za huko na kuipa kisogo elimu ambayo ni msingi wa maisha yao.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Itumbi, Apolinary Mwankumbi anasema shule yake ina wanafunzi 684 lakini kuna mahudhurio duni kwani watoto wengi hushinda kwenye uchimbaji wa dhahabu.
Anasema kwa kiasi kikubwa mazingira yanachangia watoto kujiingiza katika machimbo na wananchi wanaamini kila eneo kuna dhahabu hivyo wakati mwingine kuingia hadi eneo la shule na kusababisha mashimo.
Kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani, kukua kwa uchumi unategemea matumizi ya zana za kisasa zinazohitaji watu wenye elimu ya kutosha kuweza kuzitumia. Kwa mwenendo uliopo, utafanya kusiwe na uwezekano wa kutumia teknolojia ya kisasa katika uzalishaji hivyo tija itakosekana hatimaye kuzorotesha ukuaji wa uchumi na kuwafanya watoto hawa kuendelea kubaki masikini.
Maadili
Machimbo yana mkusanyiko wa watu kutoka sehemu mbalimbali na rika zote. Kutokana na matendo yanayofanywa na wachimbaji hawa yakiwamo ugomvi wa hadharani, unywaji wa pombe, uvutaji sigara na ngono zembe huathiri maadili ya watoto waliomo maeneo hayo.
Kutokana na wengi kuishi bila wenza wao, hali hiyo huchochea vitendo vya ubakaji pia huku wasichana wadogo wakianza kujiuza katika umri mdogo kutokana na kukosa shughuli zaidi ya hiyo.
Ofisa maendeleo ya jamii, Tekesia Mwendapolea anasema kutokana na usalama mdogo uliopo maeneo hayo, mwaka 2015/2016 watoto 20 walibakwa na wawli kulawitiwa.
Wakati majadiliano baina ya serikali na Acacia, kampuni inayoongoza kwa uchimbaji wa dhahabu nchini, ipo haja kwa mamlaka husika kuweka mazingira rafiki yatakayohakikisha uendelevu kwa wachimbaji wadogo.

Safi Kingi ajitolea kunyanyua elimu kwenye Kisiwa cha Ziwa Tanganyika


Katika kisiwa cha Mvuna kilichopo wilayani Nkasi ambacho kina wakazi zaidi ya 400 lakini kisicho na shule yoyote, kuna shujaa mmoja; Safi Kingi, mwanamke aliyeamua kuanzisha darasa kusaidia watoto wasiokwenda shule.
Safi si tajiri wala kigogo ndani ya Serikali na hajawahi kuwa ofisa katika asasi za kiraia kiasi kwamba akashawishika au kushawishiwa kufanya kazi hiyo.
Lakini upendo wake wa maendeleo ya kijiji hicho ndio ulimfanya aanzishe masomo ili kuwaandaa watoto kwa ajili ya kusaidia visiwa hivyo siku zijazo.
Mvuna, kisiwa anachoishi Safi, ni miongoni mwa visiwa vitano katika Ziwa Tanganyika na ni kitongoji cha Kijiji cha Mandakerenge chenye changamoto lukuki za huduma za kijamii kama elimu na afya.
Kijiji cha Mandakerenge, ambacho kipo Kata ya Kipili, kina vitongoji 13 vinavyotegemea shule moja ya msingi. Kutokana na umbali na changamoto za usafiri, watoto wa Mvuna hawawezi kuvuka maji ya Ziwa Tanganyika kuifikia shule hiyo kupata elimu.
Akieleza sababu iliyomsukuma kuanzisha shule hiyo mwaka 2014 hivi karibuni kisiwani humo, Safi ambaye elimu yake ni ya msingi, anasema aliona uchungu kuona watoto wengi wakiishi bila kupata elimu.
“Kilichonisukuma mimi ni kuona watoto wanakaa nyumbani bila kuwa na kazi yoyote na bila kuwa na elimu. Niliwakusanya watoto wapatao 120 na kuanza kuwafundisha nikiungwa mkono na kanisa langu la Agape,” anasema.
Anasema alipeleka wazo lake kwa uongozi wa kitongoji na baadaye Halmashauri ya Wilaya ya Namanyere ikapata taarifa na ndipo alipopewa jengo linalotumiwa kama zahanati ya dharura alitumie kama darasa lake.
Katika safari hiyo, Safi anasema kanisa analosali lilimsaidia kumpa posho ya kujikimu kwa kuwa hakuwa na muda mwingine wa kufanya shughuli za kiuchumi kama ilivyokuwa awali kabla ya kuanzisha shule.
Katika shule hiyo ya darasa moja, Safi anafundisha watoto hao kusoma, kuandika na kuhesabu na tayari wameshaanza kuonyesha mwamko wa masomo.
“Ndoto yangu ni kuhakikisha shule hii inakuwa kubwa,” anasema Safi huku sura yake ikibadilika na kuonyesha masikitiko.
Hata hivyo, kama wahenga wasemavyo “ng’ombe wa maskini hazai”, baada ya miezi mitatu ya kufundisha, Safi alianza kuugua ugonjwa ambao hakuufahamu na akawa akipoteza fahamu na baadaye akawa haoni.
“Hali hiyo iliendelea kwa miezi kadhaa, hivyo nikashindwa kutimiza ndoto yangu ya kutoa elimu kwa watoto walioikosa,” anasema Safi.
Kukatishwa kwa ndoto ya Safi ndiyo kumesababisha watoto wapatao 200 kukosa elimu na kuendelea kuishi katika ujinga uliotopea.
Safi anasema anajisikia vibaya kuwaona watoto hao wakiishi bila elimu lakini anashindwa kufufua ndoto yake kwa sababu bado hali yake haijawa nzuri.
Kuzimika kwa ndoto hizo kumewagusa wazazi ambao walishakuwa wameanza kuona nuru ya maisha mapya ya watoto wao.
Miongoni mwa wazazi wanaoathirika kwa kukosekana kwa shule kisiwani humo ni Juma Kakozi, ambaye kazi yake kuu ni uvuvi katika ziwa hilo lenye kina kirefu kuliko yote barani Afrika.
Kakozi, mwenye mke mmoja na watoto wanane, ameshindwa kuwapeleka watoto wake shule kwa sababu ya uwezo mdogo wa kifedha na shule ya Safi ndiyo ilikuwa mkombozi pekee.
Mtoto wake wa kwanza ana umri wa miaka 15, lakini hadi sasa hajaandikishwa shule kwa sababu huduma hiyo muhimu haipo kisiwani hapo.
“Unawaona watoto wote hawa, nimeshindwa kuwasomesha kwa sababu hapa hakuna shule,” anasema Kakozi ambaye anafanya biashara ya samaki lakini fedha apatazo haziwezi kumudu gharama za usafiri wa watoto wake kwenda shule.
Kutokana na ukosefu wa shule katika Kisiwa cha
Kutokana na ukosefu wa shule katika Kisiwa cha Mvuna wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa, watoto hulazimika kukaa nyumbani na jamaa zao muda wa masomo. Picha na Elias Msuya
“Hata nikiamua kuwapeleka shule huko Kirando, nitalazimika kuwa na fedha za kuwalipia nyumba ya kupanga. Wenye nyumba wenyewe wanataka kodi ya kuanzia miezi mitatu hadi minne, nitapata wapi?”
Kakozi anawalaumu wanasiasa akisema wakati wa kampeni hutoa ahadi za kujenga shule kisiwani hapo, lakini uchaguzi ukiisha wanawatelekeza.
“Wagombea udiwani huja wakisema watatujengea shule, lakini uchaguzi ukiisha hawatujali tena. Watoto wote hawa mimi nitawapeleka wapi?” alihoji.
Mtoto wa kwanza wa kakozi, Asha Juma anaonekana kukata tamaa ya kupata elimu, akisema ameshasubiri kwa muda mrefu, lakini baba yake ameshindwa na hivyo ndoto yake kuyeyuka.
Baadhi ya wazazi wenye uwezo kidogo wa kifedha kisiwani hapo wamelazimika kuwapeleka watoto wao vijiji vya mbali ili wakapate elimu huku wao wakisalia kisiwani hapo kwa ajili ya uvuvi.
Ephraim Pondamali, mwenye watoto tisa, anasema amelazimika kuwapeleka Kijiji cha Kalungu ambako wanasoma shule ya Msingi ya Mkinga.
“Kazi yangu ni uvuvi wa kujikimu tu. Tusingeweza kukaa na watoto wote hapa kwa sababu hakuna shule, hivyo tuliamua kuwapeleka Kalungu angalau wapate elimu watusaidie baadaye,” anasema Pondamili.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Elias Mlea anasema kuna watoto zaidi ya 200 waliokosa fursa ya elimu kwa sababu ya kutokuwa na shule.
“Tumeshapeleka kero hii kwa mbunge wetu, Ally Keissy lakini nilimsikia kwa masikio yangu mwenyewe akisema kwa kuwa tumechagua viongozi wa Chadema, hatatusaidia,” anasema Mlea.
“Hiki kisiwa kimekuwepo enzi na enzi. Mimi nimezaliwa hapa na nimemkuta babu yangu akiishi hapa. Isitoshe, kisiwa hiki kinatambulika kisheria na ndiyo maana kuna uongozi na kila uchaguzi ukifika wanakuja hapa kupiga kampeni.
“Lakini sasa tunashangaa wanapotutaka tuondoke.”
Mwenyekiti wa tawi la CCM la Mvuna, King Mwaliwa anadai chama hicho kimeshindwa kutekeleza ilani yake ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kutoa fursa ya elimu kwa wote.
“Utekelezaji wa ilani ya CCM hapa kisiwani haujafikia kiwango cha kuridhisha, kama unavyoona,” anasema.
“Hapa hatuna shule na tunao watoto wanaohitaji kusoma, hili ni tatizo na tulijaribu kuzungumza na uongozi wa wilaya na wa chama akiwemo Mwenyekiti wa Mkoa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, lakini hadi sana hakuna mafanikio.”
Diwani wa Kipili, Wilbrod Chakukila ndioo anafuta kabisa matumaini ya wakazi hao kuwa na shule baada ya kueleza kuwa kisiwa hicho cha Mvuna si makazi ya kudumu.
“Kile ni kisiwa cha wavuvi. Mwaka 1974 wakati Mwalimu Nyerere akiwa Rais, aliwaondoa pale kwa sababu walikuwa wachache na waliishi kama wavuvi kwa sababu hawatapata huduma za jamii,” anasema Chakukila.
Pamoja na kuondolewa wakati huo, anasema watu wamerudi na kuweka makazi ya kudumu na wengine kuishi kwa msimu wa uvuvi.
“Ni kweli kwa sasa watu wapo wengi, lakini ni hao wanaoishi kwa uvuvi tu. Kwa hiyo pale si makazi, hata mbunge alishawaambia waondoke,” anasema.
Alipoulizwa sababu za kwenda kisiwani hapo kufanya kampeni wakati si makazi yanayotambulika kisheria, Chakukila anajibu:
“Ni kweli wakati wa kampeni tunakwenda kwa sababu kuna watu. Kampeni haijali idadi ya watu, hata pakiwa na nyumba mbili, mnakwenda tunatoa ahadi.
“Sasa utakwenda pale mtu atakuuliza ‘utatusaidiaje?’ Utafanyaje sasa? Siyo ahadi za uongo kwa sababu ukiishauri Serikali nayo inakupa mipango yake.”
Akizungumza kwa njia ya simu, mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy amesisitiza kuwa hakuna mpango wa kujenga shule wala zahanati katika kisiwa hicho kwa sababu si makazi rasmi ya binadamu.
“Mvuna ni kijiji cha wavuvi na hakina eneo la kujenga shule, ni makambi ya wavuvi,” anasema.
“Wewe si umefika pale? umeona hata sehemu ya kujenga choo pale? hakuna hata nusu ekari ya kujenga shule. Mimi nimezaliwa kule, ni kambi ya wavuvi.
“Kama wanataka huduma za jamii waende Kisiwa cha Mandakerenge kuna shule na zahanati. Nimeshawaambia wahame, hawasikii. Wengi wanatoka Congo DR, Burundi sijui na wapi,” anasema Keissy.
Hali ya elimu
Wananchi wa kijiji hicho wanataabika licha ya elimu kuwa ni haki ya msingi ya binadamu iliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 11(2).
“Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake,” kinasomeka kifungu hicho cha Katiba ya mwaka 1977.
Haki hiyo pia iko kwenye lengo namba nne la Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs) linalozizitiza kufanikisha Elimu ya Shule ya msingi kwa wote, kuandikisha watoto waliofikisha umri wa kwenda shule na na kuwawezesha wafaulu na kuendelea na elimu ya sekondari.
Kauli ya Mkurugenzi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo anakiri kuwepo kwa changamoto nyingi za huduma ya jamii katika wilaya hiyo kuliko uwezo wa kuzitatua.
“Tunazijua changamoto za upatikanaji wa huduma za jamii katika visiwa vya Ziwa Tanganyika, lakini uwezo wetu ni mdogo, hivyo tunazitatua hatua kwa hatua.
“Tuliwaelekeza wanaokaa kwenye maeneo ambayo hayana huduma ya elimu, wajenge ‘satellite schools’ (shule za mfano) madarasa ya awali halafu sisi tutaunga mkono.
Maeneo mengine wameshafanya, kwa mfano Kata ya Kala, kuna Kata ya Wampembe wamefanya, tukafanya harambee tukapata fedha ya kuwaunga mkono na bado tunaendelea,” anasema Kaondo.