Thursday, September 28

KUZA FURSA : Ukiisimamia vyema, biashara itakua kila mwaka



Ally  Mbuyu
Ally  Mbuyu 
Wengi wanapenda kumiliki biashara. wachache wanathubutu kuanzisha na kuziendeleza. Wachache zaidi wanavumilia changamoto zilizopo kwenye biashara walizozianzisha.
Muda wote biashara inatakiwa kukua nakushikiria kasi ya ukuaji kwa kutatua vikwazo vilivyopo na kuangalia mwenendo huo kwa siku zijazo.
Ili kuendelea kukua, mjasiriamali anatakiwa kutafakari mwenendo wa biashara yake na kuweka dira kwa miaka kadhaa ijayo. Namna ya kutafakari ni kama vile unapokuwa juu ya ndege angani na ukaangalia chini, utaona ardhi na vilivyo jinsi vilivyokaa. Muonekano huo hutaweza kuuona ukiwa umesimama ardhini.
Hivyo dira na mipango itawekwa kwa jinsi mjasiriamali anavyoiona biashara yake itakavyokuwa miaka, mfano mitano ijayo. Hivyo kuweka mikakati itakayowezesha kufikia malengo hayo inajumuisha kuwafunza wafanyakazi mbinu mpya za kuhudumia wateja, kushirikiana katika kazi na kutatua changamoto kwa usahihi na umakini bila kuathiri biashara na wateja.
Dira na mikakati itasaidia kukabiliana na mabadiliko, kuwa imara katika kipindi cha mpito kabla ya kufikia malengo na kufanyia kazi fursa mpya zitakazojitokeza.
Katika kutafakari na kuandaa dira ya biashara inashauriwa kuzingatia mambo kadhaa ili kuwa na uhakika wa kufikia malengo yaliyokusudiwa. Muundo wa kampuni kwa siku zijazo ni miongoni mwa vitu hivyo.
Mipango, dira na mikakati ya kukuza biashara lazima iangalie muundo wa biashara yako kwa maana ya idadi ya wafanyakazi waliopo na watakaohitajika ili kuongeza nguvu ya fikra na utaalam kwa siku zijazo. Kuupanga upya muundo wa uongozi ambao utawezesha mafanikio yajayo na kwa muda mahsusi.
Kufikia malengo mazingira rafiki ya kila idara katika kampuni ama biashara yanahitajika. Wafanyakazi wanatakiwa kujituma kwa kufanya kazi bila uzembe wala kutegea. Hii itasaidia kupata matokeo yaliyokusudiwa kwa urahisi.
Mazingira hayo yanaweza kuhusisha kuwazawadia wafanyakazi, kuweka malengo kwa kila idara, kupanga semina na mafunzo ya kukabili mabadiliko ya kampuni, biashara, masoko na utandawazi utakaowawezesha wafanyakazi kujua mwelekeo wa kampuni yao kikamilifu.
Matumizi ya teknolojia ni suala lisiloepukika kwa biashara za zama hizi. Mjasiriamali anapaswa kujua matumizi mbalimbali ya teknolojia kwa kuongeza tija na kupanua uendeshaji wa biashara yake.
Teknolojia hutumika kwenye program za hesabu ambazo zinazosaidia kuokoa muda. Zipo pia program za kusimamia kalenda ya kazi ya kampuni na wafanyakazi pamoja na za kupokea na kupangilia baruapepe za kampuni.
Ni muhimu kuangalia, kupanga na kuamua ni aina gani ya teknolojia inatakiwa katika biashara na utaalamu wa wafanyakazi ili kuleta ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mkakati mwingine wa kukuza biashara ni kufungua matawi katika maeneo mengine kama vile wilaya, mikoa, kanda na nchi jirani kutegemea ukubwa na nguvu ya kampuni na biashara husika. Njia hii inatakiwa kuwa na uhakika wa soko unakotarajia kufungua matawi ili kuepuka hasara. Masoko yakiwa ya uhakika yatasaidia kampuni kukua kwa kuwa na soko pana na kuuza zaidi.
Kunapokuwa na haja iliyojadiliwa kwa kina, unaweza kuchukua mkopo kutoka katika taasisi za fedha zinazo aminika.Wataalamu wa fedha wanahitajika kufanya upembuzi sahihi ili kuona uhitaji wa mkopo, uwezo wa kuusimamia, kiasi na uwezo wa kulipa bila kusahau faida ya mkopo katika uzalishaji.
Mjasiriamali anatakiwa kupiga hatua ya maendeleo kwa kukuza biashara yake mwaka hadi mwaka. Biashara inayokaa muda mrefu bila kukua ina tatizo katika uendeshaji na usimamizi. Ni muhimu kuonana na wataalam na kupata ushauri utakaosaidia kukabiliana na changamoto ulizonazo.

No comments:

Post a Comment