Thursday, September 28

Changamoto wachimbaji wadogo wa dhahabu zishughulikiwe kuimarisha uchumi


Wakati serikali ikiweka mazingira ya kulinda rasilimali za taifa hasa madini, wananchi wanapaswa kujiandaa kunufaika na fursa kede zilizopo kwenye sekta hiyo kwa kuondoa changamoto zilizopo.
Tanzania immebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali maeneo mengi nchini lakini teknolojia ya kuyachimba, kuyachenjua mpaka kuyasafisha na kuyauza yamekuwa ni mambo yanakwaza kushamiri kwa sekta hiyo.
Wachimbaji wakubwa, wengi wakitoka nje ya nchi wamekuwa ndiyo wanufaikaji wakubwa wa madini yaliyopo nchini. Tangu uwekezaji ulipoanza mwanzoni mwa miaka ya 1990, kampuni zilizokaribishwa hazijalipa kodi kama ilivyotakiwa ili kuiongezea serikali mapato.
Licha ya migogoro kadhaa iliyoripotiwa kati ya wachimbaji hao wakubwa na wananchi au halmashauri za maeneo ilipo migodi yao, hakuna la kujivunia ambalo Tanzania linalo kutokana na udanganyifu na wizi unaofanywa na wahusika kwa kushirikiana na maofisa wa umma wasio waaminifu.
Walau kwenye migodi midogo ambako wachimbaji wadogo wameshamiri, manufaa yanaonekana kutokana na kuimarika kwa kipato cha wananchi na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha.
Kutokana na kupotea kwa rasirimali zinazowanufaisha wageni, Bunge la Bajeti mwaka huu lilifanya mabadiliko ya sheria tatu huku rai ikitolewa kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kuendeleza uchimbaji endapo wachimbaji wakubwa wataamua kuondoka.
Yapo mambo kadhaa yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini ili kupunguza athari za kimaadili, kiuchumi na kijamii kwenye maeneo yenye wachimbaji wadogo kama ilivyoshuhudiwa wilayani Chunya.
Halmashauri hii iliyopo mkoani Mbeya ni miongoni mwa wilaya zenye hazina ya madini ya dhahabu ambayo takwimu za mwaka 2016/2017 zinaonyesha kilo 546.59 zilizalishwa.
Watoto
Katika machimbo yaliyopo kwenye Kitongoji cha Itumbi Kata ya Matundas wilayani humo, makundi ya watoto kati ya watano mpaka 15 wenye na umri wa kuanzia miaka 7 hadi 17 wanajihusisha na uchimbaji wa dhahabu migodini kinyume na kifungu cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
Sheria hiyo inasema ni makosa kumuajiri mtoto mwenye chini ya miaka 18 kwenye kazi za baharini, kwenye, kubeba mizigo mizito au kufanya kazi zinazotumia tumia kemikali au mitambo na kwenye vilabu vya pombe.
Licha ya faida za machimbo yaliyopo ndani ya Mamlaka ya Mji mdogo Makongolosi wenye wakazi 4,000, watoto wadogo wanahusishwa kwenye shughuli zote hivyo kuwaathiri kwa namna moja au nyingine.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini watoto hao wanatumia nyundo na vipande vya chuma kuponda, kupunguza ukubwa wa mawe mpaka inchi moja kabla ya kutumbukizwa kwenye karasha kuyasaga ili kupata vumbi au unga wake.
Watoto hao hufanya shughuli hizo bila kuvaa glovu mikononi, kofia ngumu wala viatu vya kujikinga na madhira ya kujikwaa au kudondokewa na vitu vizito. Hawana miwani ya kukinga macho dhidi ya vipande vya mawe vinavyoruka yanapopondwa pia.
Mazingira haya huwasababishia majeraha, ulemavu hata vifo kukichangiwa na kukosekana huduma ya kwanza kwa kuzingatia ukweli kwamba kituo cha afya kipo kilomita 13 kutoka Itumbi.
Ukiacha kuhatarisha afya zao, watoto hawa wanabeba viroba vya mawe vye kati ya kilo 50 mpaka 60 na kuyasogeza kwenye mashine za kuyasaga hivyo kujiweka kwenye hatari ya kutokua vizuri kwa misuli na mifupa yao.
Watoto hao wanachanganyika na watu wazima wanaojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu pasipo jamii inayozunguka maeneo hayo kuchukua hatua zozote kudhibiti hali hiyo inayoweza kusababisha athari za kiafya, kisaikolojia huku wakikosa haki zao za msingi ikiwamo elimu.
Mratibu Elimu Kata ya Matundas (MEK), Ayubu Mwangosi anasema watoto wengi kuhusika kwenye machimbo ya dhahabu kunarudisha nyuma maendeleo ya elimu kiasi cha kuathiri matokeo ya shule za msingi na sekondari. Anasema kwa miaka mitatu mfululizo, tangu mwaka 204, wastani wa matokeo kwa kwa shule za msingi Itumbi na Matundasi si wa kuridhisha.
“Ufaulu katika Shule ya Msingi Matindasi mwaka 2014 ulikuwa asilimia 46 ambao ulishuka mpaka asilimia 43 mwaka 2015. Ingawa uliongezeka mpaka asilimia 45 mwaka 2016 bado ni chini ya asilimia 50,” anasema.
Kemikali
Pamoja na kazi ya uchimbaji madini kuwa na misukosuko mingi na hatarishi kiafya na kisaikolojia, bado watoto hao wanashirikishwa kwenye kuchimba mawe kwa kutumua sululu, kuyaponda kwa nyundo na kuyasaga kwenye makarasha kisha kutenganisha udongo na dhahabu kwa kutumia kemikali ya zebaki na cynate bila kuvaa vifaa ya usalama.
Katika uchorongaji, wachimbaji wadogo hutumia baruti kulipua miamba kabla hawajaingia ndani ya mashimo kukusanya mawe mashimoni ambako huvuta hewa inayoweza kuathiri afya zao hasa mapafu na figo.
Zebaki hutumika kutenganisha dhahabu na mchanga ila kutokana na ukosefu wa ufahamu juu ya madhara yake, hakuna tahadhari inayochukuliwa na wachimbaji hawa hivyo kujiweka kwenye hatari ya kuvuta vumbi au mvuke wake au kuila baada ya kushika chakula na kukiweka mdomoni kabla ya kunawa kwa sabuni na maji safi.
Ofisa Afya na Mazingira Wilaya ya Chunya, Yohana Ngulukia anasema kemikali hiyo huweza kusababisha magonjwa ya ini, figo, matatizo ya moyo, mapafu, macho, ngozi hata kuathiri mfumo wa fahamu na kuchangia mtindio wa ubongo.
“Vumbi la mawe huweza kusababisha kifua kikuu wakati zebaki huchangia ugonjwa ini. Hii ni hatari zaidi kwa watoto kutokana na shughuli hiyo,” anasema Ngulukia.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo, Reuben Mwakilima anasema machimbo hayo yamechangia ongezeko la magonjwa. Mwaka jana, anasema kulikuwa na wagonjwa 567 wa kifua kikuu na kati yao, 29 pamoja na watoto wawili walitoka Kata ya Matundasi.
“Hao ni waliofika hospitali na kugundulika na matatizo hayo lakini kuna idadi kubwa zaidi maeneo ya vijijini kutokana na uchimbaji madini usiozingatia afya na usalama mahala pa kazi,” anasema Mwakilima.
Elimu
Shule zilizopo maeneo ya machimbo hayo zinaelezwa kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi ambao mahudhurio yao si mazuri kutokana na watoto wengi kujihusisha na shughuli za huko na kuipa kisogo elimu ambayo ni msingi wa maisha yao.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Itumbi, Apolinary Mwankumbi anasema shule yake ina wanafunzi 684 lakini kuna mahudhurio duni kwani watoto wengi hushinda kwenye uchimbaji wa dhahabu.
Anasema kwa kiasi kikubwa mazingira yanachangia watoto kujiingiza katika machimbo na wananchi wanaamini kila eneo kuna dhahabu hivyo wakati mwingine kuingia hadi eneo la shule na kusababisha mashimo.
Kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani, kukua kwa uchumi unategemea matumizi ya zana za kisasa zinazohitaji watu wenye elimu ya kutosha kuweza kuzitumia. Kwa mwenendo uliopo, utafanya kusiwe na uwezekano wa kutumia teknolojia ya kisasa katika uzalishaji hivyo tija itakosekana hatimaye kuzorotesha ukuaji wa uchumi na kuwafanya watoto hawa kuendelea kubaki masikini.
Maadili
Machimbo yana mkusanyiko wa watu kutoka sehemu mbalimbali na rika zote. Kutokana na matendo yanayofanywa na wachimbaji hawa yakiwamo ugomvi wa hadharani, unywaji wa pombe, uvutaji sigara na ngono zembe huathiri maadili ya watoto waliomo maeneo hayo.
Kutokana na wengi kuishi bila wenza wao, hali hiyo huchochea vitendo vya ubakaji pia huku wasichana wadogo wakianza kujiuza katika umri mdogo kutokana na kukosa shughuli zaidi ya hiyo.
Ofisa maendeleo ya jamii, Tekesia Mwendapolea anasema kutokana na usalama mdogo uliopo maeneo hayo, mwaka 2015/2016 watoto 20 walibakwa na wawli kulawitiwa.
Wakati majadiliano baina ya serikali na Acacia, kampuni inayoongoza kwa uchimbaji wa dhahabu nchini, ipo haja kwa mamlaka husika kuweka mazingira rafiki yatakayohakikisha uendelevu kwa wachimbaji wadogo.

No comments:

Post a Comment