Saturday, September 2

Kenyatta aonyesha ukomavu kisiasa

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amezungumza kwa mara ya kwanza tangu Mahakama ya Juu itengue ushindi wake akisema yuko tayari kurejea kwenye mapambano kuwania madaraka.Uchaguzi wa marudio unapaswa kufanyika katika kipindi cha siku 60.
Akiwa ameambatana na makamu wake, William Ruto, Kenyatta amesema amekubali uamuzi wa Mahakama licha ya kwamba hauafiki.
Amesema raia zaidi ya 40 milioni wa Kenya waliamua kukiunga mkono chama chake cha Jubilee lakini uamuzi wa aliowaita watu sita umebadilisha mambo.
“Hawa watu sijui watano ...sijui sita wameamua kubadilisha uamuzi uliofanywa na Wakenya... naomba msife moyo, mimi na mwenzangu tuko tayari kurejea tena kwenye uchaguzi na tutarudi na ajenda yetu ileile,” amesema Kenyatta katika hotuba yake kwa Taifa.
Amewataka wananchi wa Kenya kuendelea kuwa wamoja na kutokaribisha tofauti zao, akisema umoja ndiyo nguzo muhimu kwa Wakenya.
“ Naomba tuendelee kuwa wamoja, jirani yako ni ndugu yako,” amesema Kenyatta huku akisisitiza kwa kusema, “amani, amani, amani.
Mahakama ya Juu imetengua matokeo ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8 ambao ulimpa ushindi Rais Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.

Odinga ataka mabadiliko IEBC kabla ya uchaguzi


Mgombea urais wa Kenya kupitia Muungano wa Nasa, Raila Odinga amesema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni lazima ifanyiwe mabadiliko ili kurudia  uchaguzi.
Mahakama ya Juu ya Kenya leo Septemba Mosi imefuta matokeo ya urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.
Kwa uamuzi uliotolewa na mahakama, uchaguzi mwingine unapaswa kufanyika katika kipindi cha siku 60. Iwapo ushindi wa Kenyatta ungeidhinishwa angeapishwa Septemba 12.
Odinga amesema ni lazima waliosababisha dosari kwenye uchaguzi wa Agosti 8 waondolewe.
“Tume ya uchaguzi ni lazima isafishwe ili turejee kwenye uchaguzi mwingine na nina uhakika tutashinda,” amesema Odinga katika mkutano na waandishi wa habari ambao pia uliwashirikisha viongozi wengine wakuu wa Nasa.
Amesema ni lazima viongozi waliohusika wawajibishwe akisisitiza mitambo ya Tume ya Uchaguzi ni lazima iwe wazi kwa ukaguzi.
Odinga amesema hawana imani na IEBC inayoongozwa na Wafula Chebukati kwa kuwa haikuwatendea haki kwenye uchaguzi huo.
“Leo tunasherehekea sikukuu ya Eid lakini tuna sherehe nyingine ambayo Mahakama imetupatia tunaisherehekea,” amesema.
Amesema uamuzi wa Mahakama umeipa heshima Kenya katika ujenzi wa demokrasia. Ameipongeza kwa umakini uliozingatia uamuzi wa Wakenya wa kutaka uchaguzi huru na wa haki.
 “Uamuzi wa Mahakama umetoa sura mpya na umetuma ujumbe kwa Afrika namna demokrasia yetu ilivyokomaa. Kulikuwa hakuna haja ya kurudia uchaguzi kama tume ingeonyesha matokeo katika mitambo yake,” amesema.
Odinga amesema majaji wameonyesha Mahakama zinaweza kuwa na uhuru na kusimama dhidi ya nguvu za marais Afrika.
“Mahakama imeashiria mwanzo wa Kenya mpya na daima ni kwamba, ukweli ndiyo msingi wa yote na jina na Jaji Maranga litaendelea kukumbukwa katika historia ya Kenya,” amesema. David Maranga ndiye Jaji Mkuu wa Kenya.

Mahakama Kenya yaandika historia

Historia imeandikwa nchini Kenya. Mahakama ya Juu imefuta matokeo ya urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.
Mgombea wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga alifungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8, akisema ulitawaliwa na udanganyifu ikiwemo kuchezewa mitambo ya kujumlishia matokeo.
Katika uamuzi wake, Mahakama imesema uchaguzi huo ulikuwa na dosari nyingi, hivyo kukiuka misingi ya uchaguzi huru na wa haki kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya nchi hiyo.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Taifa hilo kwa Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi na inaweka rekodi mpya katika historia ya uchaguzi barani Afrika ndani ya mfumo wa vyama vingi.
Katika uchaguzi uliopita, Odinga alienda mahakamani kupinga matokeo lakini Mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja zake na kuridhia matokeo yaliyompa ushindi Rais Kenyatta.
Katika uchaguzi wa Agosti 8, Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27, huku mpinzani wake Odinga akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74.
Kwa uamuzi uliotolewa na mahakama, uchaguzi mwingine unapaswa kufanyika katika kipindi cha siku 60. Iwapo ushindi wa Kenyatta ungeidhinishwa angepaswa kuapishwa Septemba 12.
Kumekuwa na shamrashamra katika mitaa mbalimbali ya Nairobi na Mombasa kushangilia uamuzi huo, huku Odinga akiwa na wanasiasa wenzake wamepongeza wakisema watatoa taarifa zaidi baadaye.

Bomoabomoa ni pasua kichwa


Sakata la bomoabomoa katika maeneo mbalimbali ya wakazi wa Toangoma, Bonde la Msimbazi na Kimara mkoani Dar es Salaam limeonekana kuwagonganisha viongozi wa Serikali.
Wachambuzi wameelezea hali hiyo kuwa inatokana na sheria kutofuatwa na baadhi ya viongozi serikalini.
Mgongano huo umetokana na uongozi wa juu serikalini kutengua uamuzi wa ngazi ya chini kwa kile ambacho wachambuzi wamedai ni kukosekana kwa mawasiliano ya operesheni hizo.
Bomoabomoa iliyoanza Agosti 16 mwaka huu, katika eneo la Kimara hadi Kiluvya kwa zaidi ya nyumba 1,000 yakiwamo mahekalu ya vigogo, nyumba za ibada na vituo vya mafuta, imesitishwa juzi kwa baadhi ya nyumba ambazo zina kinga ya Mahakama.
Bomoabomoa nyingine ya nyumba zipatazo 300 zilizokuwa zimeshawekwa alama ya X katika Bonde la Makamba lililopo Kata ya Toangoma, ilizuiwa juzi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kusema ameagizwa na Rais John Magufuli kufanya hivyo.
Siku hiyo alitoa agizo kama hilo kwa nyumba zaidi ya 17,000 za Bonde la Msimbazi ambazo zilikuwa katika mpango wa kubomolewa huku nyingine zikiwa zimewekwa alama ya X tangu mwaka jana.
Makonda alisema Rais Magufuli ameshangazwa na bomoabomoa hizo huku akidai kuwa hata ofisi ya mkuu wa mkoa nayo haikuwa na taarifa.
Katika ufafanuzi wake, Rais aliagiza kusitishwa kwa ubomoaji wa nyumba za baadhi ya wakazi wa Kata ya Toangoma, Temeke ambao ungezikumba zaidi ya nyumba 300 kutokana na madai ya kujengwa katika eneo tengefu la Serikali kwa ajili ya kuendeleza ukanda wa kijani maarufu kama “Bonde la Makamba.”
Lakini utata umeibuka katika utaratibu uliotumika kwenye ushirikishwaji wa ngazi za uamuzi kabla ya operesheni hizo kufanyika.
Hali hiyo imeonekana kuyumbisha mamlaka ya viongozi wa Serikali katika uanzishaji wa opeshereni hizo kabla ya kutenguliwa.
Makonda alisema kutokana na utapeli na uuzaji holela wa viwanja katika eneo hilo la Toangoma, hakuna atakayebomolewa nyumba, wakati Agosti 29, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva aliwataka waliojenga nyumba kwenye bonde la hifadhi lililotengwa kwa ajili ya kuendeleza ukanda huo wa kijani kuondoka kwani si sehemu salama kwa makazi.
“Mimi nimekuja kuwaambieni ukweli kwamba maeneo mliyojenga si halali na hamstahili kujenga, pia mmeharibu mazingira kitu ambacho hakikubaliki,” alisema Lyaviva alipozungumza na wakazi wa eneo hilo huku mkurugenzi wa manispaa hiyo akitoa notisi ya wiki moja waondoke.
Lakini juzi, Makonda aliwaambia wananchi hao, “Inawezekana kuna baadhi ya watu wanafanya zoezi hili ili kumchonganisha Rais na wananchi, wamechelewa. Hakuna nyumba itakayobomolewa kwenye mkoa wangu, nasitisha zoezi la ubomoaji kuanzia sasa.”
Alipoulizwa kuhusu kusitishwa kwa ubomoaji wa nyumba 17,000, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nemc, Dk Vedast Makota alisema hakuwa na taarifa rasmi, lakini akaahidi kutoa ufafanuzi baada ya kujiridhisha. “Jambo la msingi ni kwamba sisi kama Serikali tunawasiliana lakini ngoja nipate taarifa ili tusikie anasema nini, ndiyo nitaweza kutoa majibu,” alisema juzi.
Maoni ya wadau
Wakizungumzia mgongano huo baadhi ya watetezi wa haki za binadamu na wanazuoni nchini walisema mkanganyiko huo wa maagizo ya bomoabomoa unaonyesha namna ambavyo baadhi ya mambo yanafanywa bila kufuata utawala wa kisheria.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema mkanganyiko unaojitokeza kuhusu bomoabomoa hiyo unaonyesha namna ambavyo baadhi ya viongozi wasivyofuata utawala wa kisheria.
Dk Bisimba alisema kama sauti ya Rais kuhusu kusitishwa kwa bomoabomoa Msimbazi imesikiliwa, uamuzi wa mahakama ulipaswa pia kusikilizwa mapema kwa sababu upo kwa mujibu wa sheria.
“Mfano ni kule Kimara, watu walikimbilia mahakamani na maamuzi yakatoka kwamba bomoabomoa isitishwe, lakini iliendelea. Sasa hii inaonyesha kwamba hakuna utaratibu wa kisheria na hii hali ni hatari zaidi,” alisema.
Hata hivyo, bomoabomoa hiyo ilisitishwa na Tanroads baada ya kupokea amri hiyo ya Mahakama huku ikisema kwamba iliendelea na operesheni hiyo kutokana na kuchelewa kuipokea.
Dk Bisimba hakuwa peke yake katika hilo. Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kwa sababu katika eneo la Kimara, ilishatolewa amri ya Mahakama ya kusitishwa ubomoaji Serikali ilipaswa kutii mara moja.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga alisema ni sheria kufuata sheria na kwamba kama Mahakama ilitoa oda ya kusitishwa kwa bomoabomoa lakini Tanroads hawakutii wanapaswa kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema ipo hatari wananchi wanapogundua kuwa hata kama wakikimbilia mahakamani kupata haki hawasikilizwi.
“Unapowaumiza wananchi kwa ajili ya kuwanufaisha wengine kwa maana ya kuwaletea maendeleo, ni lazima kuangalia pia mustakabali wa wale uliowaumiza. Kama Rais Magufuli anavyoeleza kila siku, wananchi wanyonge wanapaswa kuhurumiwa,” alisema.
CCM yazuia bomoabomoa Tanga
Wakati hayo yakiendelea jijini Dar es Salaam, sakata la uwekaji alama za X katika nyumba zinazotakiwa kubomolewa jijini Tanga kupisha upanuzi wa reli limeingia sura mpya baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kuingilia kati na kusema hazitabomolewa kwa sababu hakikushirikishwa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu alisema jana kuwa kamati ya siasa imeketi na kufikia uamuzi wa kuamuru ubomoaji huo usitishwe hadi wafahamishwe na wananchi washirikishwe.
Akizungumza na wanahabari jana, Shekifu alisema kamati ya siasa iliketi juzi na kujiridhisha kuwa uwekaji wa alama za X haukufanyika kwa kufuata taratibu hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.
“Tumezungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela na ametuhakikishia kuwa kuna dosari katika zoezi zima la uwekaji wa alama za X hivyo nachukua nafasi hii kuwaomba radhi waliokumbwa na zoezi hili,” alisema Shekifu.
Uwekaji wa alama za X ulianza mwezi uliopita kwa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) kutoa notisi ya mwezi mmoja kwa wamiliki wa nyumba zilizopo mitaa ya Usagara, Chuda na baadaye mjini Muheza, Korogwe na Mombo.
Majengo mbalimbali yakiwamo makazi, hoteli za kifahari, maghala na viwanda viliwekewa X ikiwa na kupewa siku 30 kuhakikisha zimevunjwa.
Kitendo hicho kilizusha malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walieleza kushangazwa kwao na hatua hiyo kwa sababu walimilikishwa na mamlaka zenye kuhusika na masuala ya ardhi na wanalipia kodi kila mwaka.
Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Tumaini Msowoya, Cledo Michael, Hidaya Nyanga na Burhan Yakubu     

Waliomkata albino wafungwa miaka 20


Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela, washtakiwa sita kwa makosa ya kula njama na jaribio la kuua mtoto mlemavu wa ngozi (albino).
Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Adam Mambi alisema Mahakama imeridhishwa na ushahidi wa kiungo uliotolewa na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi 12 wakiwamo daktari na mkemia.
Kiungo hicho kilipelekwa kuchunguzwa vinasaba (DNA) kwa lengo la kuthibitisha iwapo kilikuwa cha mtoto huyo aliyeuawa.
Jaji Mambi alisema washtakiwa hao walithibitika kutenda kosa hilo katika Kijiji cha Msia, wilayani Sumbawanga Februari 15, 2013 kwa kumvamia mtoto Mwigulu Matomange alipokuwa akichunga ng’ombe na kumkata kiungo cha mkono na kutoweka nacho.
Alisema baada ya watuhumiwa hao kutoweka na kiungo hicho, walikamatwa na polisi Aprili 20, 2013 mkoani Tabora wakiwa katika harakati za kutafuta mnunuzi.
Washtakiwa sita kati ya kumi waliofikishwa mahakamani hapo, ambao walikutwa na hatia ni Ignas Sungura, James Paschal, Ibrahim Tela, Faraja Jailos, Weda Mashilingi na Nickson Ngalamila. Walioachiwa ni Kulwa Mashilingi, Peter Said, Hamis Rashid na James Ngalamila waliokuwa wakitetewa na mawakili wanne ambao ni Bartazar Chambi, Charles Kasuku, Peter Kamyalile na Mathias Budodi.
Jaji Mambi alisema Mahakama imejielekeza katika mambo kadhaa ya msingi ili kuthibitisha makosa hayo; iliangalia ushahidi wa mazingira; kitendo cha washitakiwa kukutwa na kiungo cha binadamu wakitafuta soko; na nia ovu ya kutenda kosa na kusababisha maumivu makali au kifo.
Alisema kosa la kula njama ya kuua, adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela kwa kuzingatia kifungu cha Sheria Namba 215 ya kanuni ya adhabu sura 16, huku kosa la kufanya jaribio la kutaka kuua adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.
Hata hivyo, Jaji Mambi alisema Mahakama kwa kuangalia mazingira ya kesi na hoja za upande wa utetezi imewapunguzia adhabu kutoka kifungo cha maisha kwa kosa la pili kuwa kifungo cha miaka 20 huku kosa la kwanza wakitumikia kifungo cha miaka 14 hivyo watatakiwa kutumikia vifungo vyote kwa pamoja.
Awali, Wakili wa Serikali Fadhili Mwandoloma aliitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotenda makosa kama hayo.
Nao, mawakili wa upande wa utetezi waliiomba mahakama kupunguza adhabu kwa wateja wao kwa kuwa tayari wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka minne kitu ambacho ni funzo tosha kwao hivyo hawawezi kurudia kutenda tena makosa hayo.    

Mdee apigania haki za mtoto wa kike


Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee amesema jamii ina wajibu wa kupigania haki za watoto wa kike dhidi ya mifumo isiyokubali mabadiliko kwa kuhakikisha wanapata fursa ya kupata elimu na kushika nafasi za uongozi.
Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, amepinga jitihada za kuwakwamisha wasichana wanaopata mimba wakiwa masomoni kutoendelea na masomo.
Amesema kikwazo hicho ni mojawapo ya vinavyopaswa kupewa jukwaa na wadau kutoa ufumbuzi badala ya kuwahukumu na kuwanyima nafasi ya pili.
Mdee amesema hayo katika kituo cha watoto yatima cha Samaritan Village eneo la Moshono jijini hapa alipokabidhi msaada ikiwa ni hatua ya kuunga mkono taasisi zilizojitolea kulinda haki za watoto waliokosa fursa baada ya wazazi wao kufariki dunia.
Mdee aliye jijini hapa kuongoza maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chadema amesema kumekuwa na ukatili ndani ya jamii ambao wakati mwingine umesababisha baadhi ya wa watoto kujikuta kwenye vituo hivyo.
Amesema katika maadhimisho hayo wameamua kujishughulisha na mambo ya kijamii kwa sababu ndipo misingi ya chama chao ilipo na kimeweza kupiga hatua kisiasa kutokana na kutetea masilahi ya wanyonge na haki kwa jumla.
Mdee amesema hatatishwa wala kukata tamaa kuzungumzia mambo anayoona yanapaswa kukemewa kwa sababu ya kuogopa kukamatwa kwa kuwa yeye ni kiongozi na atatimiza wajibu wake wa kuwasemea wasioweza kusimama hadharani.
Mratibu wa kituo cha Samaritan Village, Josephat Mmanyi amesema wanalea watoto  50 wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 21 ambao wapo katika ngazi mbalimbali za masomo.

Korti yakataa kupokea bangi kesi ya Wema Sepetu


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa kupokea msokoto na vipisi viwili vya bangi vilivyotolewa na upande wa mashtaka kama sehemu ya ushahidi katika kesi inayomkabili Wema Sepetu na wenzake wawili.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula na wakili wa utetezi, Tundu Lissu.
Awali, akiongozwa na Kakula kutoa ushahidi, akiwa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Elias Mulima kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali alidai alipima msokoto na vipisi viwili vinavyodaiwa kukutwa nyumbani kwa Wema na kugundua kuwa ni bangi.
Mulima kupitia kwa wakili Kakula aliiomba Mahakama kupokea bahasha iliyokuwa imefungwa yenye namba ya maabara 291/2017 ikiwa na muhuri na saini yake kama kielelezo cha ushahidi wake kuhusu bangi hiyo. Baada ya bahasha kupokewa na Mahakama, Kakula alimuuliza shahidi iwapo anakumbuka kuna vitu gani ndani ya bahasha hiyo?
Mulima alidai ndani ya bahasha hiyo kuna msokoto mmoja na vipisi viwili ambavyo ndani vina majani ya bangi.
Kakula alimtaka shahidi aifungue bahasha hiyo. Baada ya kuifungua alitoa vitu hivyo na kuiomba Mahakama kuvipokea kama kielelezo, ombi lililopingwa na wakili Lissu akidai ndani ya bahasha hiyo kuna vitu zaidi ya msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kuwa ni bangi.
Alidai kuwa kwa kuviangalia kwa makini vitu hivyo, ni vipisi vya sigara ya kienyeji ambayo imetumika kwa kuwa vina alama ya kuungua ambayo kwao vinaitwa twagooso.
Lissu alibainisha kuwa, kitu kinachoitwa msokoto wa bangi hakijulikani kwa kuwa kimefungwafungwa tu kwenye karatasi.
Alidai haiwezekani vitu vilivyotolewa kwenye bahasha kuwa ndivyo shahidi alivyovielezea, hivyo kuiomba Mahakama isikubali kuvipokea kama kielelezo.
Wakili Kakula alidai kuwa pingamizi za upande wa utetezi hazina msingi kisheria kwa kuwa wakati shahidi anatoa ushahidi, alieleza vitu vilivyokuwamo ndani ya bahasha kuwa ni msokoto mmoja na vipisi viwili vya bangi. Aliiomba Mahakama kuvipokea kama kielelezo.
Lissu alisisitiza kuwa, kila kilichomo kwenye bahasha hiyo iliyofungwa kilipaswa kutajwa kwa kuwa wateja wake wanakabiliwa na shtaka ambalo wakibainika wana hatia watafungwa.
Hakimu Simba alitoa uamuzi wa kukataa kupokea vitu hiyo kama kielelezo na aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 12 na 13 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Wema na wenzake Angelina Msigwa na Matrida Abbas wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na dawa za kulevya na kutumia dawa hizo.
Inadaiwa kuwa Februari 4, katika makazi ya Wema yaliyoko Kunduchi Ununio, washtakiwa walikamatwa wakiwa na msokoto mmoja na vipisi viwili vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Wema pia anadaiwa kuwa Februari Mosi katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, alitumia bangi.
Watatu kumtetea Masogange
Katika kesi nyingine inayomkabili msanii, Agnes Gerald maarufu Masogange mahakamani hapo, mashahidi watatu watamtetea.
Jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alitoa uamuzi wa kumuona Masogange ana kesi ya kujibu ya kutumia dawa za kulevya hivyo kusema anapaswa kujitetea baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake.
Baada ya uamuzi huo, mshtakiwa huyo alieleza kuwa atajitetea kwa njia ya kiapo na anatarajia kuwaita mashahidi watatu. Anatetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Ruben Simwanza.
Upande wa mashtaka unaowakilishwa na Wakili wa Serikali, Kakula uliwaita mashahidi watatu.
Masogange (28) anayekabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin na oxazepam ataanza kujitetea Oktoba 12.     

Mufti atumia baraza la Eid el Hajj kusisitiza amani


Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewataka waumini kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Akizungumza leo Septemba Mosi wakati wa baraza la Eid el Hajj lililofanyika katika Msikiti wa Taqwa, Ilala Bungoni jijini Dar es Salaam, Mufti wa Tanzania Sheikh Mkuu, Abubakar Zubeir amesema ni jukumu la kila muumini kudumisha amani kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo.
Mufti amesema hakuna kinachoweza kufanyika bila kuwepo amani na kwamba, Mtume Muhammad (S.A.W), ilisisitiza amani.
Amewataka walimu wa madrasa na maimamu kusimamia miongozo inayojenga amani, umoja na kupendana miongoni mwao kwa kuwa hakuna neema wala baraka zilizowahi kutokea popote duniani kama wananchi hawasimamii misingi hiyo.
“Mtume Muhammad (S.A.W) alikataa kufarakana kwa sababu ndani yake kuna mabaya, haijawahi kutokea baraka na neema ndani ya kufarakana,” amesema.
Amewataka waumini kila mmoja kuwa mlinzi wa amani popote alipo kwa kuwa hakuna mbadala wake, wala shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanyika bila amani.
Pia, ameeleza kusikitishwa na baadhi ya taasisi zilizochukua fedha za waumini kwa ajili ya kuwasafirisha kwenda hija lakini ikashindwa kufanya hivyo.
Mufti amesema wametoa miezi sita kwa taasisi hizo, zikiwemo Twaiba na Jamarat kurejesha fedha za waumini waliokwama kusafiri ili mwakani waweze kwenda hija.
Mgeni rasmi katika baraza hilo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amewataka waumini kuendelea kuliombea Taifa. Pia amesisitiza suala la amani.
Dk Mwinyi amesema maendeleo ya nchi yanategemea ustawi wa amani, hivyo ikikosekana hata ibada zinazoendelea kufanyika hazitawezekana.

Friday, September 1

BANDARI KAVU YA KWALA –VIGWAZA KUANZA KUTUMIKA JANUARI MWAKANI




Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto), akifafanua jambo wakati akikagua mchoro wa Bandari kavu ya Kwala –Vigwaza Mkoani Pwani.
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Eng. Charles Salu Ogare anayesimamia ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza Mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Eng. Deusdedit Kakoko akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi wa bandari kavu ya Kwala –Vigwaza Mkoani Pwani.
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa mwenye kofia ya njano akiwa katika majukumu ya ukaguzi wa ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza inayojengwa mkoani Pwani.
Muonekano wa bandari kavu inayojengwa na mkandarasi Suma-KJT katika eneo la Kwala-Vigwaza inayotarajiwa kuanza kutumika Januari mwakani ikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini , Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Kwala Vigwaza Mkoani Pwani na kumtaka mkandarasi Suma JKT kuongeza kasi na kuzingatia ubora.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo ameiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha wanaunganisha kwa haraka ili reli na barabara zinazoingia katika bandari kavu hiyo zinakamilika na hivyo kuiwezesha bandari kavu hiyo kuanza kutumika ifikapo Januari mwakani.

“TPA, TRL na TANROADS uzuri wote mko kwenye wizara moja shirikianeni na hakikisheni kilomita 15 za barabara inayoingia kwenye bandari kavu hii na kilomita moja ya reli zinajengwa haraka,” Amesema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko kuhakikisha ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza unazingatia ubora na viwango vilivyopo katika mkataba ili kuiwezesha kuhudumia zaidi ya makontena milioni moja kwa mwaka na hivyo kupunguza msongamano katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

“Hakikisheni eneo la bandari kavu linakuwa na maegesho ya kutosha, taa, maji ya uhakika, gari la zimamoto, uzio na mashine ya ukaguzi wa mizigo scanner itakayowezesha kupima kila mzigo unaopandishwa na kushushwa katika eneo hili,” amesisitiza Profesa Mbarawa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Kakoko amesema TPA imejipanga kuhakikisha ujenzi huo unatumia gharama nafuu na mifumo yote ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA inakuwepo katika bandari hiyo ili kuiwezesaha kufanya kazi kisasa na kwa ufanisi zaidi.

“Tukifanikiwa kuhamia hapa mzigo uliokuwa unasafirishwa kwa siku saba sasa utatumia siku tatu kufika Mwanza hali itakayovutia wasafirishaji wengi kutumia bandari ya Dar es Salaam na hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuibua fursa za ajira,” amesema Eng. Kakoko.

Bandari Kavu ya Kwala –Vigwaza inayojengwa na Mkandarasi SUMA JKT ambapo takribani kiasi cha shilingi bilioni 9 kinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ili kuboresha huduma za usafirishaji katika bandari ya Dar es Saalaam ambapo zaidi ya hekta 500 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo ambapo kwa kuanza hekta 120 sawa asilimia 24 zinajengwa katika awamu ya kwanza.

WANANCHI WAONDOLEWA WASIWASI KUHUSU FIDIA YA MALI ZAO ZITAKAZOPITIWA NA BOMBA LA MAFUTA


Wananchi Mkoani Singida wameondolewa wasiwasi kuhusu fidia ya mali au ardhi yao ambayo itapitiwa na mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga kwakuwa hawatapunjwa bali itazingatia vigezo vya kimataifa na kitaifa.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo amesema hayo mapema leo wakati wa kikao na wataalamu wanaofanya uthamini wa mali na ardhi ambayo itapitiwa na mradi huo.

Tarimo amesema wananchi na taasisi zote wanapaswa kutoa ushirikiano kwa kutaja gharama kulingana na thamani halisi ya mali zao na sio kuongeza gharama za juu kwakuwa vigezo vya kitaifa na kimataifa vitazingatiwa.

“wananchi wengine wasio waaminifu wananweza wakataja pesa kubwa au hata kuvamia maeneo ambayo siyo yao ilimradi wapate tu pesa, nawasihi wasifanye hivyo kwakua watakuwa wanakwamisha mradi huu muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu na majirani zetu Uganda”, amesema na kuongeza kuwa
Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo akizungumza katika kikao na wataalamu watakaofanya uthamini wa mali na ardhi kwa ajili ya fidia katika mradi wa bomba la mafuta la Kutoka Uganda hadi Tanga.


Mthamini wa ardhi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Chiku Mkina (aliyevaa miwani) na wataalaamu wengine wakisikiliza kwa makini mada katika kikao kilichohusu uthamini wa mali na ardhi kwa ajili ya fidia katika mradi wa bomba la mafuta la Kutoka Uganda hadi Tanga.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi akichangia mada katika kikao kilichohusu uthamini wa mali na ardhi kwa ajili ya fidia katika mradi wa bomba la mafuta la Kutoka Uganda hadi Tanga.
Mkurugenzi wa kampuni ya Dighy Welly Dkt Jan Perold akiwasilisha mada katika kikao kilichohusu uthamini wa mali na ardhi kwa ajili ya fidia katika mradi wa bomba la mafuta la Kutoka Uganda hadi Tanga.


Mwakilishi wa Serikali katika zoezi la Uthamini kutoka Wizara ya Nishati na Madini Linus Kinyondo akizungumza na wataalamu wa mkoa wa Singida katika kikao kilichohusu uthamini wa mali na ardhi kwa ajili ya fidia katika mradi wa bomba la mafuta la Kutoka Uganda hadi Tanga.
Mhandisi wa Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Simwela Nuru Martin akifuatilia kwa makini kikao kilichohusu uthamini wa mali na ardhi kwa ajili ya fidia katika mradi wa bomba la mafuta la Kutoka Uganda hadi Tanga.

BOT YAKANUSHA TAARIFA KUHUSU KUBADILISHA FEDHA

Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutaarifu umma kupuuza taarifa zinazozunguka katika mitandao ya kijamii kwamba kutakuwa na ‘mabadilisho ya fedha zote za zamani kuanzia tarehe 04/09/2017 hadi tarehe 01/12/2017’. 

Taarifa hizo ni za uongo na hazijatolewa na Benki Kuu ya Tanzania. Wananchi mnaombwa kuendelea na taratibu zenu za kawaida za kufanya miamala yenu mbalimbali kwa kutumia fedha zetu kama kawaida. 

Aidha, Benki Kuu ya Tanzania inawaasa watumiaji wa mitandao ya kijamii kutumia vizuri nyenzo hiyo ya kupashana habari na kuacha kuzusha uongo ambao unaleta usumbufu usio wa lazima kwa wananchi.

Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
Barua pepe: info@bot.go.tz

Simu: +255 22 2233167

MKEMIA MKUU WA SERIKALI: HUDUMA ZETU ZINAPATIKANA KOTE NCHINI

Na. Georgina Misama – MAELEZO

Serikali kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inafanya maboresho katika maabara zake za kanda zilizopo kote nchini ili kusogeza huduma hiyo kwa wananchi.

Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, Kaimu Meneja Masoko, Mawasiliano na Huduma kwa Wateja kutoka Mamlaka hiyo Cletus Mnzava alisema kwamba Mamlaka inafanya maboresho katika Ofisi zake za kanda kwa kuboresha miundombinu na kuzipatia vifaa vya maabara vya kisasa.“Lengo kuu la kuimarisha Maabara zetu za kanda ni kusogeza huduma karibu na wananchi kote nchini ili kuwaondolea ulazima wa kuja kufuata baadhi ya huduma kwenye ofisi zetu za Dar es salaam”. Alisema Mnzava

Mnzava amesema sehemu ya maboresho hayo ni pamoja na kujenga majengo ya kudumu ya Ofisi za Mamlaka katika kanda ili kuwekeza katika mitambo ya kisasa na ya kudumu. Aidha, ujenzi wa jengo la Ofisi za Kanda za Nyanda za Juu Kusini unatarajiwa kukamilika mwaka huu wa fedha.

Akizitaja Ofisi hizo za kanda Mnzava anasema kuna kanda ya Ziwa ambayo inahudumia mikoa ya Mwanza, Bukoba, Simiyu, Mara, Shinyanga, Geita na Kigoma, na kanda ya Kaskazini kwa ajili ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. Kwa mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro, Tabora na Iringa inahudumiwa na ofisi za Kanda ya Kati, wakati Kanda ya Mashariki ni kwa ajili ya Mikoa ya Dar es salaam na Pwani.

Vilevile kuna Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya Mikoa ya Mbeya, Katavi, Songwe, na Rukwa na Kanda ya Kusini kwa ajili ya kuhudumia mikoa ya Lindi, Mtwara na Songea.Mamlaka pia imejipanga kuanzisha Maabara yenye vifaa vya kisasa kwa kanda ambazo bado hazina maabara hizo ili kutoa huduma kwa weledi na ufanisi kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Mzava anasema ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano, Mamlaka imeimarisha shughuli zake za ukaguzi kwa mipaka yote nchini, ambapo kwa mipaka mikubwa kama vile Namanga na Tunduma huduma hizo za ukaguzi hutolewa kwa masaa 24.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inawaasa watanzania kujenga utamaduni wa kuzitumia Ofisi zake za Kanda kwa lengo la kufanya kazi zinazoweza kufanyika kwa haraka kwenye Kanda husika badala ya kutegemea zaidi Maabara zilizoko Ofisi za Dar es salaam.

Kaimu Meneja Masoko, Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemi Mkuu wa Serikali Bw.Cletus Mnzava akiwasomea Waandishi wa Habari (hawapo pichani) baadhi ya mikakati ya mamlaka ya hiyo kuhusu uimarishwaji wa ofisi zao hapa nchini, kulia ni Afisa Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Bw. Silvester Omary katika mkutano uliofanyika katika ukumbI wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar es Salaam leo.
Kaimu Meneja Masoko, Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemi Mkuu wa Serikali Bw.Cletus Mnzava akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari( hawapo pichani) katika mkutano wa mamlaka hiyo katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam .
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Kaimu Meneja Masoko, Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemi Mkuu wa Serikali Bw.Cletus Mnzava katika mkutano wa Mamlaka hiyo ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na: Paschal Dotto(31.08.2017