Saturday, September 2

Kenyatta aonyesha ukomavu kisiasa

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amezungumza kwa mara ya kwanza tangu Mahakama ya Juu itengue ushindi wake akisema yuko tayari kurejea kwenye mapambano kuwania madaraka.Uchaguzi wa marudio unapaswa kufanyika katika kipindi cha siku 60.
Akiwa ameambatana na makamu wake, William Ruto, Kenyatta amesema amekubali uamuzi wa Mahakama licha ya kwamba hauafiki.
Amesema raia zaidi ya 40 milioni wa Kenya waliamua kukiunga mkono chama chake cha Jubilee lakini uamuzi wa aliowaita watu sita umebadilisha mambo.
“Hawa watu sijui watano ...sijui sita wameamua kubadilisha uamuzi uliofanywa na Wakenya... naomba msife moyo, mimi na mwenzangu tuko tayari kurejea tena kwenye uchaguzi na tutarudi na ajenda yetu ileile,” amesema Kenyatta katika hotuba yake kwa Taifa.
Amewataka wananchi wa Kenya kuendelea kuwa wamoja na kutokaribisha tofauti zao, akisema umoja ndiyo nguzo muhimu kwa Wakenya.
“ Naomba tuendelee kuwa wamoja, jirani yako ni ndugu yako,” amesema Kenyatta huku akisisitiza kwa kusema, “amani, amani, amani.
Mahakama ya Juu imetengua matokeo ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8 ambao ulimpa ushindi Rais Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.

No comments:

Post a Comment