Saturday, September 2

Odinga ataka mabadiliko IEBC kabla ya uchaguzi


Mgombea urais wa Kenya kupitia Muungano wa Nasa, Raila Odinga amesema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni lazima ifanyiwe mabadiliko ili kurudia  uchaguzi.
Mahakama ya Juu ya Kenya leo Septemba Mosi imefuta matokeo ya urais yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.
Kwa uamuzi uliotolewa na mahakama, uchaguzi mwingine unapaswa kufanyika katika kipindi cha siku 60. Iwapo ushindi wa Kenyatta ungeidhinishwa angeapishwa Septemba 12.
Odinga amesema ni lazima waliosababisha dosari kwenye uchaguzi wa Agosti 8 waondolewe.
“Tume ya uchaguzi ni lazima isafishwe ili turejee kwenye uchaguzi mwingine na nina uhakika tutashinda,” amesema Odinga katika mkutano na waandishi wa habari ambao pia uliwashirikisha viongozi wengine wakuu wa Nasa.
Amesema ni lazima viongozi waliohusika wawajibishwe akisisitiza mitambo ya Tume ya Uchaguzi ni lazima iwe wazi kwa ukaguzi.
Odinga amesema hawana imani na IEBC inayoongozwa na Wafula Chebukati kwa kuwa haikuwatendea haki kwenye uchaguzi huo.
“Leo tunasherehekea sikukuu ya Eid lakini tuna sherehe nyingine ambayo Mahakama imetupatia tunaisherehekea,” amesema.
Amesema uamuzi wa Mahakama umeipa heshima Kenya katika ujenzi wa demokrasia. Ameipongeza kwa umakini uliozingatia uamuzi wa Wakenya wa kutaka uchaguzi huru na wa haki.
 “Uamuzi wa Mahakama umetoa sura mpya na umetuma ujumbe kwa Afrika namna demokrasia yetu ilivyokomaa. Kulikuwa hakuna haja ya kurudia uchaguzi kama tume ingeonyesha matokeo katika mitambo yake,” amesema.
Odinga amesema majaji wameonyesha Mahakama zinaweza kuwa na uhuru na kusimama dhidi ya nguvu za marais Afrika.
“Mahakama imeashiria mwanzo wa Kenya mpya na daima ni kwamba, ukweli ndiyo msingi wa yote na jina na Jaji Maranga litaendelea kukumbukwa katika historia ya Kenya,” amesema. David Maranga ndiye Jaji Mkuu wa Kenya.

No comments:

Post a Comment