Friday, July 28

Seif amjia juu Ndugai



Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif
Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad 
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwamba hatua ya Spika kuwavua ubunge , udiwani na kuteua wengine wapya  inalenga kudhoofisha kambi ya wabunge wa  CUF na Ukawa.
Amesema Watanzania wanapaswa wajikumbushe kwamba hata kama hicho kinachoitwa ‘kuwafukuza uanachama’ wabunge halali wa CUF kingekuwa kiko sawa, hatua kama hiyo hufuata taratibu zote za kisheria na kikanuni za Bunge kujiridhisha kwanza.
“ Spika Job Ndugai anadhani Watanzania ni vichaa wamuamini kuwa alishachukua hatua ya kujiridhisha kuwa wabunge wanane wa Chama cha Wananchi (CUF) wamefukuzwa uanachama kulingana na taratibu za chama hicho na hivyo wamekosa sifa za kuendelea na Ubunge. Ndani ya siku moja?” amehoji Maalim.
Amesema Spika amejiridhisha vipi ikiwa hata hakuwasiliana na Katibu Mkuu wa Chama ambaye kwa mujibu wa Katiba ya CUF ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za chama na pia kwa nafasi hiyo ndiye katibu wa vikao vya Mkutano Mkuu wa Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama?
Amesema yeye kama katibu, alimuandikia Spika Ndugai barua, Jumanne, Julai 25  akimueleza kwamba hilo lililoitwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF halikuundwa na wajumbe halali wa Baraza Kuu.
“Angekuwa na nia ya kweli ya kutaka kujiridhisha si hapo ndipo pangekuwa pa kuanzia kwa kuwepo kile wanasheria wanachokiita shaka inayoweza kuingia akilini yaani ‘reasonable doubt’?’’ amehoji.
Amesema  Spika Ndugai aliyapuuza yote hayo kwa sababu ni kinyume na mkakati wa Dola wa kuihujumu CUF na kuua demokrasia Tanzania. Hapo ndipo Spika Job Ndugai alipolifikisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe waanza kuingia kwenye mkutano wa baraza kuu


Zanzibar. Wajumbe wa Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF) wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, wameanza kuuingia makao makuu kwa ajili ya kikao cha baraza hilo kinachofanyika leo Vuga, Zanzibar.
Kikao hicho, ambacho mwenyekiti wa taifa anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kuwa hakitambui, kinatarajiwa kuendeshwa na Maalim Seif.
Baraza hilo kuu linatarajiwa kujadili mambo mbalimbali na kuweka msimamo  kuhusiana na kufukuzwa kwa wabunge wanane wa viti maalum hivi karibuni.
Imedaiwa kwamba kikao hicho kimeitishwa kwa kufuata masharti ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 (Toleo la 2014), kifungu cha 80 (1), ambacho kinaipa uwezo Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama kuitisha kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

Mawaziri watano wafanya ziara mpaka wa Tanzania na Uganda


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi 
Kagera. Mawaziri watano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametembelea mpaka wa Tanzania na Uganda ili kutatua changamoto zinazoukabili mpaka huo na kuuboresha.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleman Jaffo.
Pia alikuwapo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Suzan Kolimba na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe.
Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa na mawaziri hao leo Alhamisi, Julai 27 ni eneo la mpaka ya Tanzania na Uganda kwa upande unapopita Mto Kagera na eneo la kivuko cha mpaka wa Tanzania na Uganda kilichopo Mtukula mkoani Kagera.
Katika ziara hii mawaziri hao wameweza kujionea hali halisi ya maisha ya wakazi wa mipakani na jinsi wanavyohusiana na wenzao wa nchi ya jirani ya Uganda ambapo wamekuwa wakishirikiana na kuishi kwa amani katika shughuli zao za kila siku.
Aidha, ziara hii ni maandalizi ya mkutano wa ujirani mwema kati ya mawaziri wa Serikali ya Uganda na mawaziri kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao unatarajiwa kufanyika Julai  29 , Bukoba mkoani Kagera.

40 wauawa na Boko Haram Nigeria


Nigeria. Zaidi ya watu 40 wameuawa wakati wa jaribio la kuwaokoa watu waliotekwa na kundi la wanamgambo wa Boko Haram nchini Nigeria.
Takriban watu watano wa kampuni ya kuchimba mafuta waliuawa, kwa mujibu wa taarifa kutoka Chuo cha Maiduguri. Wanajeshi pia waliuawa wakati wa uvamizi huo.
Idadi hiyo kubwa ya vifo ni pigo kwa Serikali ambayo inasisitiza kuwa kundi la Boko Haram limeshindwa.
Takriban watu 20,000 wameuawa na maelfu ya wengine kutekwa tangu Boko Haram ianzishe harakati zake mwaka 2009.
Katika kisa kibaya zaidi Boko Haram waliteka wasichana 276 kutoka shule ya wasichana Kaskazini Mashariki mwa Nigeria katika mji wa Chibok mwaka 2014.
Ripoti za awali kutoka kwa jeshi nchini humo zimesema kuwa waliotekwa walikuwa wakifanya kazi katika Chuo cha Maiduguri lakini baadaye waliachiwa.
Siku ya Jumanne jeshi lilisema kuwa miili ya wanajeshi tisa na raia mmoja ilipatikana.

BARAZA LA MADIWANI KISHAPU MKOANI SHINYANGA WAPONGEZWA KWA HATUA YA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO KWA UFANISI PAMOJA NA CHANGAMOTO ZA UHABA WA FEDHA



Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Boniphace Butondo akizungumza wakati akifungua kikao cha Baraza la Madiwani la kupokea na kujadili tarifa za kata za robo ya nne ya mwaka. Wengine pichani kushoto ni Makamu mwenyekiti wa halmashauri, Edward Shigela na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Stephen Magoiga.

Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akizungumza wakati wa kikao hicho. Wengine pichani kuanzia kushoto ni Katibu Tawala Wilaya, Shadrack Kangese, Makamu mwenyekiti wa halmshauri, Edward Shigela na Mwenyekiti Boniphace Butondo.

Madiwani na wataalamu kutoka halmashauri hiyo wakifuatilia kikao hicho cha kupokea na kujadili tarifa za maendeleo ya kata.

Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kangese akizungumza neno wakati wa kikao hicho.

Makamu mwenyekiti wa halmshauri, Edward Shigela akizungumza wakati akifunga kikao hicho.

Madiwani na wataalamu kutoka halmashauri hiyo wakifuatilia kikao hicho cha kupokea na kujadili tarifa za maendeleo ya kata.


………………………………


Na Robert Hokororo

Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imepongezwa kwa hatua yake ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ufanisi pamoja na changamoto za uhaba wa fedha.

Pongezi hizo zimetolewa leo na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Boniphace Butondo wakati akifungua kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kupokea taarifa za kata kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka.Butondo alisema miradi hiyo imetekelezwa kwa kiwango kizuri pamoja na changamoto ya uhaba wa fedha iliyoikabili halmashauri hiyo kwa kipindi hicho.

Alisema ushirikianoa baina ya madiwani na wataalamu kutoka halmashauri hiyo ndiyo siri ya mafanikio hayo ambayo ni tija kwa wananchi wanaowahudumia.Aidha, aliwapongeza wataalamu hao kutoka idara mbalimbali kwa kuwa na usimamizi mzuri ikiwemo wa fedha na maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa na kuwataka waendelee kushikamana.

“Naomba niwapongeze wote kwa ushirikiano mkubwa mnaounesha najua kuna changamoto ya kuwa na mapato kidogo kutokana na hali ya hewa na hivyo kuchangia kutopata pamba kwa wingi ambayo inaingiza mapato halmashauri,” alisema.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya lagana aliishukuru ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ushirikiano mkubwa kwa halmashauri na hivyo kuchangia mafanikio hayo.

Tayari miradi mbalilimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, zahanati, barabara na maji imetekelezwa katika kata mbalimbali za halmashauri ya wilaya hiyo.

DKT. PHILIP MPANGO ABAINI BAADHI YA WAFANYABIASHARA DODOMA HAWATUMII IPASAVYO EFDs


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akikagua mashine ya EFD na risiti ya kieletroniki aliyopewa baada ya kununua bidhaa kwenye moja ya maduka mjini Dodoma, alipofanya ziara ya kushitukiza kukagua kama wafanyabiashara wa mji huo wanatumia ipasavyo mashine hizo.
Kiongozi wa Timu Maalumu ya Ukaguzi wa Mashine za EFD’s kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Dodoma, Bw. Godfrey Patrick (wa pili kushoto) akifafanua jambo wakati wa ziara ya kushitukiza iliyofanywa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), kwenye maduka mjini Dodoma.
Mfanyabiashara wa duka la rejareja mjini Dodoma, Bw. Donald Chami, akimwonesha mashine ya kieletroniki ambayo imeharibika, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), baada ya kufanyaziara ya kushitukiza kwenye duka lake na kubaini kuwa hatoi risiti za kielektroniki kwa wateja wake.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akipitia kwa makini fomu ya makadirio ya kodi iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika moja ya duka la vipodozi mjini Dodoma wakati alipofanya ukaguzi wa matumizi ya mashine za EFD’s katika baadhi ya maduka yaliyopo mjini humo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akimuonya mfanyabishara wa mjini Dodoma, Bw. Isdori Shirima, baada ya kukuta akiuza bidhaa bila kutoa risiti za kielektroniki kwa wateja wake inavyotakiwa na kuagiza Mamlaka ya Mapato mkoani humo kufanya ukaguzi wa kina ili kubaini kiwango cha ukwepaji kodi cha mfanyabiashara huyo na kumchukulia hatua za kisheria.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akikagua risiti ya mteja aliyenunua tanki la kuhifadhia maji katika moja ya duka linalouza vifaa vya ujenzi mjini Dodoma, na kutoa wito kwa wananchi kukagua risiti zao ili kubaini kama kiwango kilichoandikwa kinalingana na kiasi kilichoandikwa kwenye risiti.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akimwelekeza mwananke mmoja aliyemkuta dukani akague risiti yake baada ya kufanya manunuzi kwenye duka moja la vifaa vya ujenzi mjini Dodoma, alipofanyaziara ya kushitukiza ili kubaini namna wafanyabiashara wa maduka mjini humo wanavyotumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akimuagiza Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Dodoma, Bw. Ngaka Magere, kumkutanisha na mawakala wanaosambaza mashine za kieletroniki za kutolea risiti mkoani humo baada ya kutoridhishwa na huduma zao.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), akisikiliza maelezo ya matumizi ya mashine za kielektroniki kutoka kwa mfanyakazi wa Kituo kimoja cha Mafuta mjini Dodoma, alipofanyaziara ya kushitukiza kituoni hapo kuangalia matumizi ya mashine hizo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akikagua risiti na kupata maelezo kutoka kwa mhudumu wa Kituo cha Mafuta cha ORYX mjini Dodoma, Bi. Hanifa Shaldin, alipofanya ziara ya kushitukiza kuangalia kama vituo vya mafuta mjini humo vimefungwa mashine za kielektroniki za kutolea risiti kwa wateja wao. (Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM).

RAIS DKT. MAGUFULI AWASILI JIJINI DAR, AWAHUTUBIA WANANCHI WA TEGETA KWA NDEVU




Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es salaam, baada ya wananchi hao kusimamisha msafara wake alipokuwa safarini akirejea jijini Dar es salaam kutokea Mkoani Dodoma, Julai 27, 2017.
Sehemu ya wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es salaam, wakimsikiliza Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliposimama kuzungumza nao, alipokuwa safarini akirejea jijini Dar es salaam kutokea Mkoani Dodoma, Julai 27, 2017.
Sehemu ya wananchi wa eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es salaam, wakimshangilia Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliposimama kuzungumza nao, alipokuwa safarini akirejea jijini Dar es salaam kutokea Mkoani Dodoma, Julai 27, 2017. PICHA NA IKULU.

MNADA WA HADHARA WA MALI ZA UBALOZI DAR ES SALAAM


UNIVERSAL AUCTION CENTRE Kwa idhini waliyopewa na  OFISI YA UBALOZI watauza kwa mnada wa hadhara  Funicha za nyumbani na Generator  tarehe 29 Julai, 2017 Jumamosi saa 4:00 asubuhi. 
Mnada utafanyika Golden Resort Sinza,  
Lion Street, Dar es salaam.
Fanicha na Computer zitaanza kuuzwa kuanzia saa 4:00 asubuhi: 
Sofa sets, Recliner, Sofa Bed, Wing chairs, Chest drawers,  Dressers, Mirror, Credenza, Entertainment Centre, Coffee table, Book case, Meza za chakula / Viti, Meza za ofisi, Carpet, Vitanda ,Magodoro, Fridge, Freezer, Music system, TV, Jiko la umeme, Washer, Dryer,  Heavy duty Tread mill, Computer set, Photocopy m/c, File cabinet, safe,  A/c Split unit, Refrigerant Reclaim System  na vingine vingi.

Generator Zitaanza kuuzwa saa 6.00 mchana:
Idadi
Aina
Model
Mwaka
Ushuru
3
Generator 40 & 60 KVA
Perkins Diesel   Engine
2001/ 2004
Bado

Mali zote zinaweza kukaguliwa Golden Resort Sinza,Lion Street tarehe 26  hadi 28 Julai, 2017 kuanzia saa 4:00. asubuhi mpaka saa 11:00 jioni.

MASHARTI YA MNADA:
  1. Mnunuzi  wa Fanicha atatakiwa kulipa malipo yote kwa keshia (cashier). Na mnunuzi wa Generator  atatakiwa kulipa 25% pale pale na salio lilipwe ndani ya siku 4 za kazi  mwisho wa kulipa tarehe 3 August 2017, saa 10:00 jioni. Ukishindwa kulipa kwa muda huo generator litauzwa  kwa mshindi mwingine aliyefata  na dhamana haitarudishwa.
  1. Mali zote zitauzwa kama zilivyo bila dhamana.
  1. Mnunuzi atawajibika kulipa ushuru na kodi zingine zote.
  1. Mali yote iliyouzwa itatakiwa kuondolewa baada ya kulipa malipo yote pamoja na kodi 
  2. Kila mtu atatakiwa kuwa na bid namba itakayo patikana getini.
Kwa maelezo zaidi waone:
UNIVERSAL AUCTION CENTRE
PLOT NO. 5 “E” LION STREET SINZA
CELL NO:  0754 284 926, 0757 284 926                       
E-mail: universalauction@hotmail.com
DAR ES SALAAM.

Thursday, July 27

Nilichosema Kupitia Sauti Ya America Kuhusu Sakata La Acacia Na Serikali Ya Tanzania

Image may contain: mountain, sky, outdoor and nature

Mbali ya mambo mengine..
- Acacia kwa namna yeyote hawawezi kulipa deni hilo. Itachukua karne nyingi.
- Acacia watapenda kulimaliza jambo hili haraka kwa mazungumzo kwa kutambua kuna makosa wameyafanya.
- Kiasi hicho kimekokotolewa na TRA kwa kufuata ripoti zile mbili na kinaipa nafasi Serikali kuingia kwenye meza ya majadiliano na nguvu ya kushinikiza kupata ( Si kiasi kilichokokotolewa) bali kipande kikubwa zaidi cha keki kwa maslahi ya Watanzania.
- Tutakachokiona hivi karibuni ni kuongezeka kwa spidi ya mazungumzo kati ya Acacia na Serikali.

Serikali: Bei ya karafuu haishuki

anzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesisitiza kuwa bei ya karafuu inayotolewa kwa wakulima haitashuka hata kama bei ya soko la nje itashuka.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi  Amina Salum Ali amesema  lengo la Serikali katika ni kuwanufaisha wakulima zaidi ili kuwajengea ari ya kulihudumia vyema zao hilo kwa manufaa yao na Taifa kwa jumla.
“Hakuna nchi yoyote duniani inayolipa wakulima bei ya asilimia 80 ya soko la nje kwa mazao ya biashara na wala hakuna zao lolote hapa Zanzibar linalofikia bei ya Sh14,000 kwa kilo zaidi ya karafuu, hivyo nawaahidi wakulima wetu kuwa Serikali haitothubutu kushusha bei ya zao hilo,” amesema Balozi Amina.
Amesema huu ni wakati kwa wakulima na wananchi kwa jumla kushirikiana na Serikali ili kuona zao hilo linaendelea kuimarishwa zaidi ili vizazi vijavyo navyo viweze kunufaika na urithi wa zao hilo ambalo ni mkombozi kwa wanyonge walio wengi.
 “Nawaombeni sana tuliendeleze na tulitunze hili zao letu la karafuu ili vizazi vijavyo visije tulaaumu kwa kutowaachia urithi huu ambao ndio mkombozi wetu katika maisha’’ amesema Balozi Amina.
Akizungumzia magendo ya karafuu, Balozi Amina amewataka wananchi kila mmoja kuwa askari dhidi ya watu wanaofanya magendo ya karafuu na wawe tayari kuwafichua kwa kuwa ni adui wa zao hilo.
Amesema suala la magendo ya karafuu halikubaliki na tayari Serikali imejizatiti kwa kutunga kanuni kwenye Sheria ya Maendeleo ya Karafuu na kuimarisha ulinzi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto katika uchumaji  karafuu.
Amesema uchumaji wa karafuu ni miongoni mwa kazi ngumu hivyo si busara kuwaajiri watoto kufanya kazi hiyo badala yake wawahimize kwenda shule.
 Amesema kuwatumia watoto katika kazi za uchumaji karafuu ni kwenda kinyume cha haki za watoto na wanapopata ajali hukosa haki ya kulipwa fidia kwa vile kwa mujibu wa masharti ya bima hawatambuliki.
Pia, amewaonya wafanyabiashara wanaopita vijijini kununua karafuu mbichi kinyume na uratibu kuwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwa vile kufanya hivyo ni kosa.

Lowassa afunguka miaka miwili nje ya CCM

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa gazeti la Mwananchi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis. 
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa leo ametimiza miaka miwili tangu aweke historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu serikalini kuihama CCM na anasema hajutii uamuzi wake, yuko imara na licha ya kuzuiwa kufanya mikutano, kura zake zinazidi kuongezeka.
Lowassa alichomoka CCM Julai 27, 2015 ikiwa ni siku chache baada ya Kamati Kuu ya CCM kuondoa jina lake na mengine katika kinyang’anyiro cha urais, uamuzi ambao ulizua mtafaruku mkubwa uliosababisha wajumbe wa Halmashauri Kuu kuimba wimbo wa kuonyesha kuwa na imani naye wakati mwenyekiti wa wakati huo, Jakaya Kikwete akiingia mkutanoni.
Siku moja baada ya kujiengua CCM, Lowassa alitangaza kujiunga na Chadema, chama ambacho kilimpa fursa ya kuendeleza “Safari ya Matumaini” aliyoianzisha CCM, kwa kushirikiana na vyama vingine vitatu vilivyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akihojiwa na Mwananchi jana kuhusu miaka yake miwili nje ya CCM, Lowassa alisema pamoja na kupata kura zaidi ya milioni sita za urais, yeye na wapinzani wenzake wanasononeshwa na kunyimwa haki ya kufanya mikutano na kukutana wanachama wao.
Hata hivyo, alipoulizwa ni kwa kiwango gani kunyimwa fursa ya mikutano kumemuathiri, alisema: “Kura zangu zimeongezeka sana, tena sana. Ile tu kutoniona kunaniongezea (kura).
“Nataka kwenda kuwaona (wananchi) lakini siruhusiwi. Nataka kufanya mikutano ya hadhara, siruhusiwi. Sio mimi tu, ni pamoja na wenzangu wote kwenye vyama vya upinzani, hii ndiyo kauli yao.
“Waeleze wananchi na wanachama wa Chadema, nawapenda sana. Natamani kwenda kwao, kuzungumza nao, lakini sipati nafasi.”
Alikuwa akizungumzia amri ya kuzuia mikutano ya hadhara ya wanasiasa hadi mwaka 2020 iliyowekwa na Serikali. Zuio hilo halihusu mikutano ya wabunge na wananchi wao, lakini hawaruhusiwi kualika wanasiasa kutoka maeneo mengine.
Hana lolote la kujutia
Lowassa, ambaye sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema pamoja na hali hiyo wanayokumbana nayo, hana cha kujutia kutokana na uamuzi wake wa kujiunga na upinzani.
“Sina cha kujutia hata kidogo,” alisema katika mahojiano hayo yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
“Nadhani ulikuwa uamuzi sahihi. Baada ya kuutafakari wakati ule na sasa, bado naamini ulikuwa uamuzi sahihi.”
Pamoja na hayo, Lowassa aliyewania urais na kupata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97 dhidi ya Rais Magufuli aliyepata kura milioni 8.8 (asilimia 58.46), alisema kuna tofauti kubwa kufanya siasa ukiwa CCM na ukiwa upinzani.
Alisema hali ni tofauti kwa sababu kuna changamoto nyingi zaidi kwenye chama cha upinzani ukilinganisha na CCM.
Alisema kuna maswali mengi ambayo yanajitokeza na CCM ilikuwa na muundo na miundombinu ya kukabili mambo hayo, tofauti na ilivyo kwenye vyama vya upinzani kutokana na uchanga wake.
“Hivi vyama bado ni vichanga, havina capacity (uwezo) kama ilivyo CCM. Kweli kuna changamoto nyingi, leo kuna changamoto hii, kesho kuna hii, lakini kubwa ni kuwahusisha wananchi, tupate nafasi ya kuzungumza na wanachama, kujadiliana nao na kufanya nao kazi kutatua changamoto zilizopo,” alisema Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 alipoachia ngazi.
Kuhusu Chadema, alisema chama hicho kikuu cha upinzani kinakua haraka, kinaongeza idadi ya wanachama na viongozi wengi, hivyo akasema kinachotakiwa ni kujenga uwezo wao.
Alisema uzoefu huo hauwezi kuja kwa siku moja, bali kwa muda mrefu kama ilivyo kwa CCM.
“CCM ni moja ya vyama vikongwe Afrika na ina uzoefu mkubwa. Ukitulinganisha sisi (utaona) tuko nyuma yao, lakini tunayo majukumu makubwa na makali zaidi mbele yetu kuliko wao,” alisema.
Kuzuiwa mikutano
Akizungumzia changamoto zinazoukabili upinzani katika uendeshaji siasa kwa sasa, Lowassa alisema Watanzania wanajua, wanaona na wanasikia kwamba vyama vya upinzani vinanyimwa haki hiyo.
“Pamoja na kura milioni sita tulizozipata za urais, hatuna haki. Haturuhusiwi kufanya mikutano ya hadhara. Hili ni jambo gumu sana kulielewa. Ni jambo baya sana katika demokrasia,” alisema Lowassa ambaye mikutano yake ya kampeni ilikuwa ikifurika watu kila alipoenda.
“Ni jambo lisilokubalika katika jamii ya kimataifa, lakini imewekwa kwamba ukifanya mkutano wa hadhara unakamatwa unapelekwa mahakamani.
“Sasa hiyo inatunyima nafasi ya kuwasiliana na wanachama wetu. Lakini Katiba ya nchi hii imeruhusu vyama vya siasa vishindane bila kupigana. Tupingane bila kupigana. Vyama vimeruhusiwa kufanya hivyo. Serikali kuzuia mikutano ya hadhara ni blow (pigo) kubwa kuliko zote tulizopata katika uongozi wa vyama vya upinzani.”
Alisema kuzuia mikutano ni kukwaza wananchi.
“Kama hatupati nafasi ya kushindanisha sera zenu, mtakuwa mnawakwaza wananchi na mtakuwa mnakwaza demokrasia katika nchi,” alisema.
Atajwa uchaguzi Kenya
Wakati Lowassa na wenzake wakiwa wamezuiwa kufanya mikutano ya hadhara, jina lake limeibuka kuwa gumzo nchini Kenya ambako kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 8, zinaendelea.
Baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Nkaissery, Lowassa alifanya mahojiano na vyombo tofauti vya habari, na tangu hapo amekuwa akitajwa kila mara kwenye majukwaa ya kisiasa.
“Sijisikii lolote jina langu kutajwa Kenya, ila hiyo ndiyo siasa. Mimi ni mwenyekiti wa Malaigwanani (viongozi wa kabila la Wamasai) wa Afrika Mashariki. Kwa nafasi hiyo nina nafasi ya kwenda Kenya kuzungumza na Malaigwanani wenzangu umasaini juu ya nafasi za kisiasa,” alisema Lowassa ambaye anatuhumiwa na wapinzani wa Nasa kumfanyia kampeni Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee.
“Na kule sikuzungumza siasa. Chama changu kilikaa, tukasema kati ya wagombea wote, anayefaa kuliko wenzake ni Uhuru Kenyatta. Ni bora kuliko wengine wote. Baraza Kuu lilitoa kauli ya kumuunga mkono. Kwa hivyo chama kilitoa uamuzi huo na mimi nautekeleza kumuunga mkono Uhuru Kenyatta.”
Upinzani wa Simba, Yanga
Akizungumzia sababu za kufikia uamuzi huo, Lowassa alisema: “Na nieleze, hatukufikia uamuzi huo hivihivi, sisi tuna vigezo vyetu. Tunamwona Kenyatta kama mtu anayependa ushirikiano wa Afrika Mashariki. Pale mpakani Wamasai wanapita kwenda na kurudi kila siku ya maisha yao. Usipompata mtu anayependa ushirikiano huo, mtakuwa mmenoa sana.
“La pili, tunaona katika utawala wake, Kenyatta anapenda, anaheshimu sana wapinzani. Anauona upinzani kama ushindani. Na hiyo ni vizuri, ushindani unatakiwa uwe kama wa Simba na Yanga, sio chuki za kisiasa au chuki za kuuana na kupigana.
“Kwa hiyo nilipokwenda kumzika marehemu Nkaissery, walinialika niseme kidogo, na mimi nikasema ‘msirudi mlikotoka maana ni aibu, nikasema mchague mtu atakayesimamia masilahi ya Afrika Mashariki, mtu ambaye ataheshimu upinzani, mtu ambaye mtakubaliana kufanya kazi naye pamoja na nchi zetu zikawa na amani na utulivu.
“Hayo ndiyo niliyasema, nafurahi yamesikika, najua wamenijibujibu lakini ukweli utabaki palepale. Nawatakia wote kila la heri na uchaguzi uende kwa amani. Amani ya nchi ile ni muhimu sana, amani ikiwapo Kenya, pia itakuwapo Tanzania.”
Lowassa alirudia kauli yake kuwa katika Uchaguzi Mkuu 2020 atashinda kwa kishindo na atakuwa tayari kwa uchaguzi huo, lakini kwa sasa wamwachie Rais Magufuli afanye kazi yake.
“Yapo mambo mazuri anayofanya Rais Magufuli, aungwe mkono. Na kwa kiasi kikubwa anafanya mazuri, lakini haya hayajatoka mbinguni, bali ni wajibu wake,” alisema Lowassa.
“Isionekane kama ni salamu kutoka mbinguni, ni wajibu wake kama Rais. Kazi ya Serikali ni kutoa huduma, ni kujenga shule, ni kujenga hospitali. Ndiyo kazi ya Serikali, kwa hiyo watu wasihesabu kuwa ni hisani.
“Wamefanya kazi yao, kwa kweli nawapongeza, lakini wasionekane wamefanya hisani. Kazi za Serikali zote duniani ni kuleta maendeleo kwa watu au kuandaa mazingira ya kuleta maendeleo.”
Mbunge huyo wa zamani wa Monduli alitoa angalizo dhidi ya siasa za chuki alizosema zimeanza kujitokeza nchini, akisema zisipokomeshwa zitaiingiza nchi pabaya.
Alisema vitendo vya wakuu wa wilaya kushindana kukamata viongozi, wanachama na wafuasi wa upinzani kama njia ya kuwakomoa ni vibaya na havikubali.
Alisema sheria hiyo ya kuweka watu ndani kwa saa 48 iliwekwa kwa ajili ya watu wanaofanya fujo kama kwenye mkutano, lakini si kuwakomoa.
Aliwapongeza viongozi walioamua kuwashtaki wakuu wilaya binafsi waliochukua uamuzi huo, akisema mahakama zina uhuru, zitarekebisha hali hiyo.
Kuhusu wimbi la madiwani wa Chadema kujiuzulu mkoani Arusha na sasa Kilimanjaro, Lowassa alisema ingawa kuhama ni haki yao, inasikitisha kusikia kuna watu wanashawishiwa kwa fedha.
“Wale wanaosema wanapenda sera za Rais Mafuguli, nawatakia heri, lakini si wangesubiri hadi 2020, kuhama ni haki yao lakini waeleze sababu halisi,” alisema

Ukawa ilivyoendeleza Safari ya Matumaini


Dar es Salaam. Lilikuwa ni jambo lisilotarajiwa kwamba mmoja wa wagombea urais ndani ya CCM aliyeonekana kuwa na ushawishi mkubwa, angekihama chama tawala.
Mbali na hilo, hakuna aliyeweza kufikiria kuwa mtu aliyewahi kushika nafasi ya juu kama ya uwaziri mkuu, angeweza kuchukua uamuzi mzito kama huo katika nchi ambayo chama tawala ni ‘chama dola’.
Lakini Edward Lowassa alithubutu kufanya hivyo mwaka 2015 alipotangaza kuihama CCM siku kama ya leo na kujiunga na upinzani, ambao hapo awali ulimrushia kila aina ya kombora ukimhusisha na kashfa ya Richmond.
Huo ulikuwa ni mwanzo mpya wa kisiasa kwa Lowassa, mbunge wa zamani wa Monduli, aliyekulia ndani ya CCM na kufanya shughuli zake zote ndani ya chama hicho tawala. Alikuwa na kazi nzito ya kuanza kazi ya kuendeleza “Safari ya Matumaini” nje ya CCM.
Wengi waliamini kuwa uamuzi wake wa kujiondoa CCM na kwenda upinzani ulikuwa ni wa hasira na kama ilivyo kwa wanasiasa wengi, angerejea chama tawala baada ya hasira kutulia licha ya kupewa nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine vitatu.
Lakini leo, anapotimiza miaka miwili tangu ajiondoe CCM, Lowassa bado hafikirii wala kuwaza kurejea chama hicho na zaidi ya yote hajilaumu kujiunga upinzani.
“Sijutii kujiunga upinzani,” alisema Lowassa jana katika mahojiano na Mwananchi kuhusu mtazamo wake wa kisiasa katika kipindi cha miaka miwili alichokuwa nje ya chama tawala hadi sasa.
Aliingia kwenye mtihani mkubwa wa kuwania urais akipambana na chama ambacho alikitumikia kwa muda mrefu na kuanzisha “Safari ya Matumaini” ya kuwa Rais, lakini iliyokatishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Lakini matokeo ya Uchaguzi Mkuu yalimpa mwanga. Alishika nafasi ya pili katika mbio za urais, akipata kura 6.072,848, ambazo ni zaidi ya mara mbili ya kura ambazo wapinzani walikuwa wakipata tangu mwaka 1995 wakati Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi ulipofanyika kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.
Kura hizo ni sawa na asilimia 39.97 dhidi ya Rais Magufuli aliyepata kura 8,882,935 (asilimia 58.46), kiwango ambacho ni kidogo kwa mgombea urais wa CCM tangu mwaka 1995.
Haikuwa rahisi Lowassa kukubaliwa na kupewa dhamana hiyo ya kugombea urais akiungwa mkono na vyama vinne, baada ya CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kuamua kutosimamisha mgombea kwa makubaliano ya Ukawa.
Julai 26, 2015 ikiwa ni siku moja kabla ya kuondoka CCM, mwandishi wetu alimshuhudia Lowassa akihudhuria kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema. Aliwasili lango la Hoteli ya Ledger Bahari Beach, Dar es Salaam saa 3:02 usiku na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe. Baada ya hapo aliongozwa kuelekea chumba cha Watu Mashuhuri (VIP) na kukutana na viongozi wachache wa chama hicho akiwamo makamu mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohammed. Mazungumzo hayo yalidumu kwa takribani dakika 18 na ilipofika saa 3:20 usiku, walitoka na kuingia ukumbini kwenye kwa ajili ya kikao cha Kamati Kuu.
Lowassa alishiriki kikao hicho kwa takriban dakika 98 na ilipofika saa 4:58 usiku, alitoka akisindikizwa na Mbowe, Willibrod Slaa (katibu mkuu wakati huo), Profesa Abdallah Safari (makamu mwenyekiti) na Salum Mwalimu (naibu katibu mkuu, Zanzibar).
Saa 18 baada ya Lowassa kutambulishwa Kamati Kuu ya Chadema, Julai 28 viongozi wengine wa Ukawa waliitisha mkutano wa wanahabari mchana na kumkaribisha.
Waliokuwapo katika mkutano huo ni wenyeviti wa Ukawa; James Mbatia (mwenyekiti NCCR – Mageuzi), Emmanuel Makaidi (mwenyekiti wa NLD - sasa ni marehemu), Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba (mwenyekiti CUF).
Walitumia mkutano huo kuzungumzia tuhuma dhidi ya Lowassa walizoshiriki kuzitoa, hasa sakata la mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura baina ya Tanesco na kampuni ya Richmond Development ya Marekani.
“Sisi tunaponda ufisadi na mfumo wa kifisadi. Chanzo kikubwa cha ufisadi ni mfumo ndani ya CCM. Kwanza tuing’oe CCM, hapo ndipo tutakapoweza kuondoa ufisadi na kujenga msingi wa kupambana na ufisadi na rushwa iliyopo,” alisema Profesa Lipumba.
“Lowassa alikumbwa na tuhuma za ufisadi mwaka 2008, leo ni 2015. Ufisadi umeongezeka au umepungua? Lowassa hayupo serikalini, akaunti ya Tegeta Escrow imetokea wakati gani? Lowassa alikuwapo? Tatizo ni mfumo na jambo la kwanza ni kuing’oa CCM.”
Kuhusu kushirikiana naye wakati walikuwa wanamtuhumu kwa ufisadi, makamu mwenyekiti wa CUF wa wakati huo, Juma Duni Haji alihoji: “Mbona CUF iliwahi kupigana na kuuana na CCM mwaka 2000 lakini leo wameunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa?”
Dk Makaidi alisema kama Lowassa angekuwa mbaya kiasi hicho, angekuwa ameshashtakiwa kama ilivyo kwa viongozi wengine ambao tayari wameshahukumiwa vifungo kwa matumizi mabaya ya madaraka au rushwa.
Mbatia alisema Ukawa inamwalika kila Mtanzania aliye tayari kuuondoa mfumo kandamizi na dhalimu wa CCM na watashirikiana naye kujenga Taifa imara na kwamba Lowassa ni miongoni mwa wanaokaribishwa.
Siku moja baadaye, Lowassa alitangaza rasmi kujiunga na Chadema akisema, “Sasa basi, imetosha”.
Alisema amejiunga na chama hicho ili kutekeleza azma yake ya kuwakomboa Watanzania na kuendeleza Safari ya Matumaini kupitia Ukawa.
“CCM imepotoka, imepoteza mwelekeo na sifa za kuendelea kuiongoza Tanzania,” alisema Lowassa katika mkutano wa kumkaribisha Chadema uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Ledger Bahari Beach na kurushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni na redio.
Lowassa alitumia dakika 13 kueleza sababu za kujiunga na Chadema, mbele ya wenyeviti wenza wa Ukawa katika mkutano huo, ambao haukuhudhuriwa na Dk Slaa, naibu wake (Bara), John Mnyika na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.
Wakati Lowassa akizungumza, wanachama wa Chadema walikuwa wakiitikia ‘peoples power’, na alipomaliza hotuba yake waliimba wimbo maalumu wa “Tuna Imani na Lowaasaa”, ambao ni wa kuonyesha mshikamano na ambao uliimbwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupinga jina la Lowassa kutopitishwa kuwania urais.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa misukosuko ya kisiasa inayohusisha kupambana na vyombo vya dola ambayo hakuwahi kukutana nayo wakati akiwa CCM.
Agosti 29, 2016, akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na wabunge, walikamatwa na polisi wakiwa katika kikao cha ndani jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi ambako walihojiwa na kuachiwa huru.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema: “Tulikuwa kwenye msafara wa kumpokea, lakini tulipofika hapa stendi wananchi walitaka kuongea na Lowassa. Kabla hata hajashuka kwenye gari, askari walituvamia wakasema tuondoke moja kwa moja twende kituoni.”
Ilikuwa ni wakati Lowassa alipofanya ziara kwenye maeneo ya wananchi kuzungumza nao kama sokoni, vituo vya mabasi na hospitali.
Agosti 12, 2015 msafara wake na viongozi wengine wa upinzani waliounda Ukawa ulizuiwa wilayani Mwanga, Kilimanjaro wakati wakielekea kuhudhuria mazishi ya kada wa CCM, Peter Kisumo.
Polisi walitaka Lowassa pekee ndiye aende na viongozi wengine warudi, pendekezo ambalo alilikataa.
Si hilo tu, Januari 16, 2017 polisi mkoani Geita walimkamata Lowassa akiwa anakwenda kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Kata ya Nkome na baadaye aliachiwa, huku taarifa za polisi zikidai kuwa walimzuia kwa sababu za kiusalama.
Tukio jingine lilimkuta Agosti 23, mwaka jana wakati msafara wake ulipouiwa kwenda mikoa ya Rukwa na Katavi baada ya polisi kuhofu kuwa ungeweza kuingilia ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Na Juni 27, 2017 Lowassa aliitwa polisi kuhojiwa kuhusu kauli zake za kutaka kesi masheikh wa Uamsho wanaoshikiliwa na polisi ziharakishwe na wapewe dhamana. Hadi sasa anaripoti Makao Makuu ya Polisi upelelezi ukiendelea.
Pamoja na misukosuko hiyo, jina la mwanasiasa huyo limeibuka kwenye siasa za nchi jirani ya Kenya, hasa baada ya chama chake kutangaza hadharani kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta anayepambana na mwanasiasa mkongwe, Raila Odinga.