Sunday, April 1

Wengi wanatarajia mahubiri ya Pasaka yagusie amani, upendo na umoja


Dar es Salaam. Wakati waumini wa dini ya Kikristo nchini wakiungana na wenzao duniani kote kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, wachambuzi wa masuala ya siasa, uchumi na jamii wanatarajia kusikia ujumbe kuhusu amani, upendo na mshikamano.
Kadhalika, baadhi yao wamesema wanatarajia viongozi wa dini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) kutoa ufafanuzi zaidi wa waraka waliotoa hivi karibuni kuhusu masuala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimaendeleo.
Akizungumza na Mwananchi, wakili wa kujitegemea kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Harold Sungusia alisema hivi karibuni viongozi wa KKKT na TEC, walitoa matamko yaliyozungumzia hali halisi ya nchi katika masuala ya demokrasia na maendeleo.
Alisema baada ya matamko hayo kumekuwa na mijadala mingi ya kupinga na kuunga mkono, hivyo watumie sikukuu hiyo kufafanua matamko hayo kama kuna jambo jipya wamelisikia baada ya kuyatoa.
Februari 10, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) lilitoa ujumbe wa Kwaresma wa mwaka 2018 ndani yake likitoa msimamo kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Ujumbe huo ulioandikwa na maaskofu wote 35 wa TEC wakiongozwa na rais wao, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa ulizungumzia hali ya kisiasa nchini kwa kuonya uamuzi wa Serikali kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni kwenda kinyume cha Katiba ya nchi.
Mbali na tamko la TEC, maaskofu wa KKKT nao pia walitoa waraka wa ujumbe wa Sikukuu ya Pasaka uliozungumzia masuala ya kiroho na kutaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini wake ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa.
Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa Letu, Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini, ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.
Akizungumzia anachotarajia kukisikia katika ujumbe wa viongozi wa dini katika Sikukuu ya Pasaka, Sungusia alisema kwa kawaida mahakamani huletewa malalamiko na mlalamikaji hujenga hoja kutetea malalamiko yake, kisha hupewa majibu ya kile alichokiwasilisha kabla ya mlalamikiwa kupewa nafasi ya mwisho ya kujibu hoja zilizojengwa kutokana na malalamiko dhidi yake.
“Kwa lugha ya kimahakama huitwa “rejoinder” ambapo mlalamikiwa baada ya kusikiliza malalamiko dhidi yake hupewa nafasi ya mwisho ya kujibu hoja, nategemea viongozi wa dini waliotoa waraka na matamko, watatumia sikukuu hii kufanya hivyo, ”alisema Sungusia.
Alisema anategemea pia kusikia viongozi wa dini wakizungumzia masuala ya demokrasia na maendeleo ikiwamo Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
“Kwa kuwa ni kipindi cha kukumbuka mateso ya Yesu Kristo, nategemea wazungumzie mateso ya watu wengine ikiwamo ya familia ya Tundu Lissu aliyepigwa risasi.
“Nategemea pia watazungumzia mateso inayopitia familia ya mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi, Azory Gwanda aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba mwaka jana.
“Lakini mateso ya familia za wanasiasa wanaotaabika kuhakikisha Tanzania inakuwa na siasa safi na uongozi bora na ambao wanasherehekea sikukuu hii wakiwa mahabusu, ”alisema Sungusia.
Wakili huyo alisema wananchi wangependa kusikia viongozi wa dini wakizungumzia hali ya maisha kuwa ngumu na kushuka kwa kipato “Mke wangu amefunga biashara zake, hakuna wateja, matumizi yameongezeka”.
“Tungetaka pia kusikia mateso ya Yesu yanatuasa nini sisi raia wa kawaida, ingawa maeneo mengi ya maandiko yanatuasa kuyashinda mateso ili kupanda daraja, tunahitaji kupata mwongozo wa hilo kutoka kwao,” alisema.
Lakini, Dk Jimson Sanga wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) alisema katika mahubiri ya sikukuu hiyo angependa kusikia wakihubiri kuhusu amani, kupendana na kuwa na mshikamano bila kuoneana.
Alisema kwa kuwa nchi ipo katika wakati mgumu wa masuala mbalimbali ipo haja ya kutafsiri Biblia kama maagizo ya Mungu mambo yanapokuwa na ukakasi.
“Maandiko ya Biblia ni yaleyale kwa sababu ni kitabu kitakatifu, lakini je, tunakitafsiri vipi katika wakati huu.
“Amri 10 za Mungu ziliamrisha upendo, tukifuate hicho kutatua kila gumu ili kama binadamu tuendelee na maisha kwa amani,” alisema Dk Sanga.
Profesa wa Uchumi katika Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), Damian Gabagambi alisema amri iliyo kuu ya Mungu ni upendo, hivyo katika mahubiri ya sikukuu hiyo yalenge masuala ya amani na upendo.
Alisema maisha ya Yesu Kristo yaliamrisha upendo na mshikamano, hayakuwa na mapambano.
“Maudhui ya hotuba zao yawe katika muktadha wa siku husika na maisha ya Yesu Kristo ambaye leo tunaadhimisha kufa na kufufuka kwake, ”alisema Profesa Gabagambi.
Mwanasiasa mkongwe, Njelu Kasaka alisema dini ni sehemu ya maisha ya mwanadamu ya kila siku, hivyo anatarajia mahubiri hayo yatahusu maisha ya kila siku ya mwanadamu.
Alisema kwa sababu hakuna anayeweza kuwa na dini na kuyakimbia maisha ya kila siku katika dunia, hivyo wahubiri watapita katika maeneo hayo.
“Hata ukimjua Mungu kupita kiasi huwezi kukwepa maisha ya kawaida kama mwanadamu, kwa sababu kukiwa na maafa, vita, njaa, kimbunga, ukame vitakuhusu kama mwanadamu uliye duniani.
“Hivyo viongozi wa dini naamini watazungumzia na kugusa kila kitu kinachomuhusu binadamu na mazingira yanayomzunguka ikiwamo dini, ”alisema Kasaka.
Akizungumzia anachotarajia kusikia kutoka kwa viongozi wa dini mkazi wa jijini Dar es Salaam, Emmanuel Zakayo alisema:
“Natamani kusikia wakizungumzia na kutafakuri kuhusu nchi inakokwenda na nini kinatakiwa kufanyika ili tuvuke hapa tulipo sasa kwa amani.”
Mkazi mwingine, Zawadi Mkilanya alisema anatamani kusikia viongozi wa dini wakizungumzia zaidi masuala ya kusamehe na kutendeana mema.
“Naamini mahubiri kama hayo yatahamasisha upatikanaji wa haki miongoni mwetu, badala ya kuchochea migongano, ”alisema Mkilanya.

No comments:

Post a Comment