Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amewataka watu kuwapuuza wale wote wanaojaribu kupotosha ukweli wa waraka wa maskofu kwa kuupaka matope.
Askofu Shoo ametoa kauli hiyo Jumapili katika Usharika wa Moshi Mjini Dayosisi ya kaskazini, mkoani Kilimanjaro katika salamu za Pasaka wakati wa ibada maalumu ya kuadhimisha siku hiyo.
Amesema baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kupotosha waraka wa maaskofu.
Wengine wamejaribu kulipaka kanisa matope kwa malengo yao binafsi jambo ambalo halipendezi na kwamba watu hao ni wajinga. Lakini pamoja na hilo nataka wakayatafakari na kama wanaona kuna hatua zinapaswa wachukue basi wafanye hivyo.
“Kanisa limekuwa linapata kejeli za aina mbalimbali kutoka kwa watu hao na kuwatuhumu kuwa maskofu walifikia maamuzi ya kuandika waraka huo kutokana na sababu za kimaslahi kwa maana ya sadaka makanisani kupungua jambo ambalo si la kweli.
“Kanisa linasitikika sana, tunaposema jambo la kweli na jambo linalohusu maisha ya Watanzania wote, halafu kunatokea watu chache ambao naweza kuwaita wajinga wanakebehi na kusema eti kwa sababu sadaka zimepungua kanisani sisi sadaka hazijapungua kwani wakristo wanajitoa sana na hatujapungukiwa na kitu ila tunasema yale tunayoyaamini,” amesema.
Askofu Shoo amesema anafahamu kuwa kupitia waraka ule maaskofu wa kanisa hilo watabatizwa majina ya aina mbalimbali.
Ameongeza: "Hizo ni jitihada za kujaribu kuuzima ukweli ulipo katika wataka huo na wao hawajali kuhusu hilo bali watasimamia ukweli zaidi."
No comments:
Post a Comment