Sunday, April 1

Wabunge waishauri Serikali kupunguza mrabaha wa madini


Dodoma. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, imeitaka Serikali kupunguza mirabaha inayotoza katika biashara ya madini ili kuepusha utoroshaji rasilimali hizo nje ya nchi ambazo zimekuwa zikitozwa kiwango kidogo.
Sheria ya madini iliyopitishwa na Bunge mwaka jana inawataka wawekezaji kulipa asilimia sita ya mirabaha, ikiwa ni ongezeko la asilimia tatu iliyokuwa ikitozwa awali.
Akizungumza jana wakati kamati hiyo iliyochambua bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2018/19, mwenyekiti wa kikao hicho, Vedasto Mathayo alisema kuna nchi za jirani ambazo zimekuwa zikitoza mrahaba wa asilimia moja.
Mathayo ambaye pia ni mbunge wa Musuma Mjini (CCM), alisema kutokana na mrabaha kuwa mkubwa wachimbaji wadogo wamekuwa wakitumia mwanya huo kutorosha madini kwenda nje ya nchi ambako wanatozwa kidogo.
Alijibu hoja hiyo, naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko alikiri Tanzania kutoza mrabaha zaidi ya nchi jirani lakini ukweli athari zinazopatikana baada ya wajichambaji kuondoka ni kubwa.
“Lazima kupata mrabaha mkubwa kuziba pengo la hasara hizo zinazopatikana baada ya wawekezaji kuondoka nchini,” alisema Biteko.
Pia, Biteko alikiri kuwa hata Benki ya Dunia (WB) ilitaka nchi itoze mrabaha pungufu ya asilimia tatu, lakini Serikali imeona ni vyema ikatoza kiwango hicho ili kizazi kijacho kione matunda baada ya wawekezaji kuondoka.
Hata hivyo, Biteko alisema kutokana na ongezeko la mrabaha huo, makusanyo yameongezeka katika sekta ya madini ambalo limeanza kutumika mwaka mmoja uliopita.
“Kwa mwaka mmoja tangu imeanza kutumika, sekta ya madini inakua vizuri na imechangia kuongeza mapato,” alisema.
Kuhusu ukuta uliojengwa Mererani kwa takriban Sh4 bilioni, Biteko alisema unalenga kudhibiti vitendo vya wizi wa madini ya Tanzanite na kwamba utafunguliwa rasmi Aprili 6.
Naye katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema takwimu za makusanyo ya maduhuli zinaonyesha hadi Februari 28 yamefikia asilimia 103.
Kamati hiyo iliidhinisha na kuipitisha bajeti ya wizara ya zaidi ya Sh58 bilioni ambazo wabunge walidai ni kidogo na kwamba ilipaswa kutengewa Sh100 bilioni.

No comments:

Post a Comment