Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametuma ujumbe wa Sikukuu ya Pasaka, akiwahakikishia wananchi kuwa "tuko imara na wala msiwe na huzuni".
Wakati huohuo viongozi wa chama hicho, wabunge na madiwani leo watawatembelea viongozi wao na ‘kusherehekea’ nao kwa dakika kadhaa mahabusu.
Mjumbe wa kamati kuu Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema hatua ya baadhi ya viongozi, wanachama na wabunge kwenda kumuona Mbowe na wenzake ni njema na inawapa faraja kubwa viongozi hao waliopo gerezani.
Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema ujumbe wa mwenyekiti huyo ambaye pia ni mbunge wa Hai ulitolewa jana na mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Anatropia Theonist aliyekwenda Gereza la Segerea kumjulia hali na kubainisha kuwa viongozi zaidi watakwenda ‘kula’ Pasaka na Mbowe na wenzake mahabusu leo.
Mbowe na viongozi wengine watano wa chama hicho wapo Gereza la Segerea tangu Alhamisi iliyopita. Wanasiasa hao watatakiwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jumanne ijayo kila mmoja akiwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh20 milioni na kuwa na barua kutoka kwa viongozi wao ama wa vijiji au mtaa.
Uamuzi wa mahakama kuwapa dhamana viongozi hao wa Chadema ulitolewa Alhamisi huku washtakiwa wakiwa hawapo mahakamani ikielezwa kuwa gari lililopaswa kuwapeleka mahakamani limeharibika jambo ambalo limewafanya waendelee kukaa mahabusu mpaka Sikukuu za Pasaka zitakapomalizika.
Kadhalika zoezi hilo litafanyika kwa viongozi wengine wa Chadema walio mahabusu ya Segerea, pia watafanya hivyo kwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anayetumikia kifungo cha miezi mitano jela na katibu wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga.
Mbowe na wenzake wanakabiliwa na jumla ya makosa manane, likiwamo la kuhamasisha uasi, chuki na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Mbali na Mbowe, viongozi wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, manaibu katibu wakuu John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko.
Chadema imesema lengo la kwenda kuwaona ni kuwapa moyo na mshikamano viongozi wao. Pia hii itakuwa historia kwa wafungwa na mahabusu wa Segerea.
Naye mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi alisema "nitaongoza msafara wa viongozi wa baraza hilo watakaokwenda kuwatembelea viongozi waliopo Segerea."
“Tunataka viongozi wetu wafahamu kuwa kuwekwa magereza ni kusudi jingine la kukipeleka chama chetu mbele, kule kuna watu watapata fursa ya kuzijua siasa za chama chetu, naweza kusema wameendelea kutusaidia kueneza chama chetu katika mazingira yoyote yawe magumu au rahisi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu ujio wa viongozi wa Chadema, Mkuu wa Gereza la Segerea, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Mwanangwa Mandarasi aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa milango ipo wazi.
Alisema utaratibu wa kutembelea wafungwa na mahabusu haujabadilika kikubwa wahusika wafuate utaratibu uliowekwa ili wasivunje sheria.
“Kama kuna watu wengi huwa wanaingia kwa awamu ili wote wapate fursa ya kuwaona wanaowahitaji. Sitarajii kama hao viongozi wa Chadema watakuwa wengi kesho (leo) kwa sababu baadhi yao walishaanza kwenda tangu Ijumaa (juzi) na Jumamosi (jana)” alisema Mandarasi.
No comments:
Post a Comment