Kumekuwa na wasiwasi nchini Kenya kuhusu namna gharama ya mahari inavyopandishwa kadiri siku zinavyosonga katika jamii mbalimbali.
Hivi majuzi kiongozi wa kisiasa wa serikali katika Bunge la Kenya alishutumu gharama kubwa ya mahari katika jamii ya Wasomali.
Kiongozi wa wengi bungeni, Aden Duale anasema hicho ndicho chanzo kikuu kinachowavunja moyo vijana na kuwafanya wasusie ndoa.
Amelalamika kwamba gharama kubwa zinazotozwa zimeugeuza utamaduni huo kuishia kuwa kama ''kitega uchumi cha mamilioni ya dola''.
- Walio kwenye ndoa za 'njoo tuishi' kuadhibiwa Burundi
- Mwanamke ataka mahari kufutiliwa mbali Zimbabwe
Lakini sio tatizo linaloshuhudiwa kwa Wasomali tu. Vijana wanataja kukwama kupiga hatua ya kufunga ndoa kutokana na gharama hizo kubwa za mahari wanazoshindwa kuzimudu.
Mahari inavyotozwa katika baadhi ya nchi za Afrika:
Somalia:
Idadi ya ngamia au pesa taslimu mwanamume anazoahidi kumlipa mkewe kama mahari huitwa Meher.
Sio lazima Meher ilipwe moja kwa moja lakini huwa ni kama ahadi wameandikiwa, na mume hana budi kulipa katika kipindi cha ndoa.
Zamani ngamia ndio waliotumika kulipa mahari hayo lakini siku hizi mtindo umebadilika na pesa taslimu ndio zinazothaminiwa zaidi katika jamii hii.
Kijana anaweza kutakiwa kulipa hadi dola elfu kumi za Marekani kwa bibi harusi. Na kila thamani ya mahari inapokuwa kubwa ndio huonekana kuwa fahari kubwa kwa bibi harusi na familia yake na pia hudhihirisha ukubwa wa thamani ya mke anayeolewa.
Lakini tatizo kubwa ni kwamba vijana wengi hawawezi kugharimia mahari inayoitishwa na baadhi yao huishia kuwa na deni la maisha.
Tanzania:
Tanzania, ni nchi nyingine inayotajwa kushuhudia viwango vikubwa vya mahari katika baadhi ya jamii.
Huenda ndio moja ya sababu inayowafanya baadhi ya vijana kutooa kwa njia rasmi.
Vigezo ni vingi vinavyobaini kiwango cha mahari atkachotozwa kijana, mfano katika baadhi ya jamii - weupe wa msichana humaanisha mahari zaidi, lakini pia kiwango cha elimu cha msichana anyechumbiwa.
Kwa kukadiria kijana huitishwa ng'ombe au pesa zenye thamani ya kati ya shilingi milioni 5 hadi milioni 20 za Tanzania.
Uganda:
Utamaduni huu ni wa kawaida nchini Uganda, zaidi kwa jamii zilizopo katika maeneo ya mashinani, lakini pia hutolewa katika maeneo ya mijini.
Mahari nchini humu hufuata msingi ambao umekuwepo - kutoa kitu ili upewe mke.
Lakini sasa kuna mtindo kwa baadhi ya familia kuandikishana mikataba na bwana harusi kama ithibati ya kulipa mahari anayoitishwa.
Inaaminika kuwa iwapo mke amemtoroka mumewe baada ya kuteta na akarudi kwao, familia yake haina budi ila kurudisha mahari yote aliyolipiwa.
Mnamo 2010 mahakama nchini humo iliamua kuwa utoaji mahari ni halali, lakini majaji walipiga marufuku mtindo huo wa kurudishwa mahari wakati ndoa inapovunjika.
Kenya:
Katiba nchini Kenya haishurutishi ulipaji wa mahari, lakini ni jambo linalofahamika kuwa mahari hulipwa katika jamii tofuati nchini.
Baadhi ya jamii kwa mfano kwa wafugaji husisitiza mahari ya mifugo, huku kwa jamii nyingine mali, pesa taslimu na hata madini hupokewa kama mahari.
Huwepo hisia kwamba kuna malipo aliyotolewa mke kwenda kwa mume.
Afrika Kusini:
Mahari hapa huitwa "lobola", ambapo mwanamume hukabidhi ima mali au ng'ombe kwa familia ya mke au kwa mara nyingine vyote - kama ishara kwamba yuko tayari kumuoa.
Malipo ya lobola ni ishara ya uwajibikaji wa mwanamume kumhudumia mkewe na huonekana kama ishara muhimu na inayohitajika katika kuendeleza utamaduni, na sio kana kwamba amemnunua mwanamke.
Mahari ni nini?
Utamaduni wa kutoa mahari upo katika nchi nyingi ulimwenguni zikiwemo barani Asia, mashariki ya kati sehemu kadhaa za Afrika na pia katika baadhi ya visiwa vya pasifiki.
Kiwango kinachotolewa hutofautiana kuanzia zawadi ndogo tu za kuendeleza utamaduni huo hadi maelfu ya dola za Marekani kwa mfano kama inavyoshuhudiwa katika ndoa za baadhi ya jamii.
Tangu jadi, utoaji mahari umekuwa ni utamaduni unaoheshimiwa na kuenziwa pakubwa hata miongoni mwa jamii za watu waliosoma na kuishi maisha ya kisasa.
- Mwanamume alazimika kumlipia mahari mfu Msumbiji
- Kisiwa ambacho wanawake huwabeba wanaume Rwanda
- Mwanamke adai mumewe alimuibia figo
- Harusi za kifahari zapigwa marufuku Somalia
Kwa kawaida mahari huwa ni kama mkataba wa makubaliano kabla ya ndoa ambapo mali kama ng'ombe, ngamia, mbuzi au hata pesa taslimu hulipwa na bwana harusi kwa familia ya bibi harusi ili apewe mke.
Iwapo mume hatotimiza mahari iliyokubaliwa kwa muda uliotolewa, kuna jamii ambao humrudisha mke nyumbani mpaka mume akamilishe kulipa mahari.
Na kwa namna ambavyo mambo yamekuwa yakibadilika na gharama kuongezeka, baadhi ya wadadisi wanasema utamaduni huu wa kutoa mahari unageuzwa kuwa njia ya kujinufaisha na kujigamba kwa mali badala ya kuwa utamaduni wa kuonyesha upendo na shukrani.
Mchambuzi wa masuala ya kijamii kutoka Tanzania Betty Masanja anasema, "Suala zima limegeuzwa na kumfanya mwanamke kuwa chombo au bidhaa tu."
''Hali inazidi kuwa mbaya kutokana na kuwa, watu wana shida za kiuchumi, umaskini umekithiri hasa kwa familia ambazo hazikusoma."
Ndio maana unaona hata jamii zinawaozesha watoto wao wakiwa na umri mdogo ili mahari ilipwe kuitajirisha familia.
Lakini sio suala la kujitajirisha tu, Betty anasema kuna kutothaminiwa kwa mtoto wa kike ambapo wengi huozeshwa ili mali ipatikane kusaidia kumuelimisha mtoto wa kiume.
Ameeleza: ''suala zima limegeuzwa na kumfanya mwanamke kuwa chombo au bidhaa tu''.
No comments:
Post a Comment