Kwa wanakijiji waishio katika vijiji vilivyopo katika visiwa vya Lamu mpakani mwa Kenya na Somalia, upatikanaji wa huduma nyingi za jamii za msingi ni changamoto kubwa.
Mashirika mengi ya misaada yamekoma kuhudumia wanakijiji katika visiwa hivyo na miundombinu yake mingi imeharibika kutokana na kuongezeka kwa mapigano kati ya wanajeshi na wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab.
Barabara hazipitiki, shule zimefungwa, na hakuna huduma muhimu za afya.
Visiwa sita vinategemea madaktari wa kujitolea maarufu kama 'Safari Doctors' ambao hufunga safari mara moja kwa mwezi kwa kutumia mashua na kutoa huduma za afya bure kwa mamia ya wakazi.
Hakuna vituo rasmi vya afya vya serikali hivyo wakazi wanategemea madakatri wa kujitolea.
Ni safari ya usiku kucha ndani ya mashua iliyobeba dawa, madaktari, wauguzi na wasaidizi wengine wa kujitolea.
Aisha Omari ni mkazi wa kijiji cha Kiangwe. Hivi karibuni, alipata tatizo la kuharibika kwa mimba.
"Nilikuwa na mimba ya miezi mitatu, siku moja nilienda kuchota maji kisimani, mbali sana na nyumbani, niliporudi, nilipoweka tu chini mtungi wangu wa maji, nilianza kuvuja damu. Usiku wote nilikuwa nasikia uchungu, mgongo uliniuma, nilipiga mayowe. Huku watu wakiniangalia wakisubiri nife na hapo ndipo madaktari hawa wa kujitolea walipokuja, wakanipeleka hospitalini, nikasafishwa na sasa nimepona''.
Madaktari hawa huandaa kambi za matibabu katika visiwa hivi. Muuguzi Mkuu Harisson Kalu, anasema wakazi wengi hujitokeza wakiwa na mahitaji mbalimbali.
"Tunaleta huduma ya chanjo, tunahudumia wajawazito, tunapima ukimwi na malaria na magonjwa mengine madogo madogo, na tunapopata wale wagonjwa tunawatibu na kufuatlilia''
Mmoja baada ya mwingine, wanatibiwa ama kuangaliwa na daktari, wanapewa chati za matibabu, na wengine dawa kuimarisha afya zao hadi pale msafara huu wa madaktari utakaporejea kwa matibabu zaidi baada ya muda wa mwezi mmoja.
Mashua hufanya ziara za matibabu katika visiwa sita na kuhudumia maelfu ya wanakijiji. Safari nzima huchukua siku tatu.
Hali ya gharama za uzazi Kenya ikoje?
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO, takriban wanawake 830 hufariki dunia kutokana na sababu zinazohusiana na ujauzito na kujifungua ikiwemo gharama za kupokea hudumu za afya. WHO linasema nyingi ya sababu za vifo hivi zingeweza kuzuilika.
Asilimia 99 ya vifo vyote hutokea katika mataifa yanayoendelea.
Kenya imekuwa ikishuhudia kiwango kikubwa cha vifo vya akina mama wajawazito. Kutokana na hilo, serikali iliidhinisha sera ya utoaji huduma za bure kwa kina mama wanaojifungua katika taasisi za umma tangu mwezi Juni 2013.
Sera hii imekuwa ikiwawezesha mamia ya wanawake wajawazito kupata huduma za bure wakati wa kujifungua katika vituo vya afya vya umma.
Utaratibu ni kwamba vituo hivyo vya afya hutoa huduma ya bure na baadaye serikali inavilipa kupitia wizara ya afya kulingana na idadi ya akina mama waliozalishwa.
Pia hakuna malipo yanayotolewa kwa huduma za kabla na baada ya kujifungua kwa akina mama na watoto kwa hadi wiki sita.
Licha ya huduma hiyo ya bure, kiwango cha hudumu zinazotolewa bado kinazusha maswali mengi huku baadhi ya wazazi katika hospitali hizo za umma wakiishia kujifungua katika hali duni na wengine hata kuishia kulala kitanda kimoja na wazazi wenzao.
Sio wengi wanaoweza kumudu gharama za hospitali za kibinafsi nchini.
No comments:
Post a Comment