Friday, March 16

Lissu kukaa hospitali siku 14


Arusha. Alute Mughwai, kaka wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema ndugu yake atakaa kwa wiki mbili katika hospitali ya Leuven Gasthuisberg ya nchini Ubelgiji baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kulia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2018 Mughwai amesema kutokana na operesheni hiyo, Lissu ambaye alikuwa akipatiwa matibabu hospitali na kurejea kwenye makazi yake, sasa atakaa hospitali kati ya siku saba hadi 10.
Amesema upasuaji katika mguu huo, ambao awali ulionekana kutounga vizuri, ulikwenda vizuri na madaktari wa hospitali hiyo wamemtaka alazwe ili kupata matibabu zaidi.
Wakili Mughwai ambaye ndiye msemaji wa familia ya Lissu, amesema baada ya siku 10, Madaktari watatoa taarifa juu ya maendeleo ya afya yake na mazoezi ya viungo ambayo alikuwa anaendelea nayo.
"Kutokana na maelekezo ya madaktari kwa sasa, hatuwezi kusema Lissu atarudi lini nchini, kwani upasuaji wa jana umesababisha alazwe tena hospitali"alisema.
Amewaomba Watanzania na watu wengine, kuendelea kumuombea Lissu ili apone haraka na arejee nchini.
Akizungumzia matibabu ya Lissu, amesema wanaomba watanzania na wasamaria wema, kuendelea kumchangia Lissu kupitia akaunti iliyotolewa na Chadema.
“Bado tunafanya mazungumzo kujua kama itawezekana awe na akauti nyingine Ubelgiji ili kusaidia matibabu kwani hadi sasa anatibiwa kwa misaada wa watanzania na watu wengine kutoka nje ya Tanzania,” amesema.

No comments:

Post a Comment