Wednesday, December 6

Mwanafunzi anaswa akiwa na sare za jeshi


Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Fahari iliyopo Goba kwa kosa la kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema leo Jumanne Desemba 5,2017 kuwa mwanafunzi huyo mwenye miaka 17 (jina linahifadhiwa) anayesoma kidato cha tatu alikamatwa jirani na Benki ya CRDB maeneo ya Mbezi jijini Dar es Salaam akiwa amevaa sare za JWTZ.
Amesema mwanafunzi huyo akiwa amevaa sare alikuwa akivuta sigara hadharani na kufanya vitendo visivyoendana na maadili ya askari.
Kamanda Mambosasa amesema katika mahojiano ya awali, kijana huyo alijitambulisha kuwa ni askari kutoka  501KJ Lugalo jijini Dar es Salaam.
Amesema baada ya kubanwa alikiri kupata sare hizo kwa rafiki zake na upekuzi ulipofanywa ndani ya begi alilokuwa nalo alikutwa na kofia nyingine moja ya jeshi hilo.
Pia, alikutwa na kitambulisho cha mtoto wa askari wa JWTZ Private Gabriel Kiwila wa 501 KJ.
Kamanda Mambosasa amesema kitambulisho hicho kilikuwa na picha ya mtoto wa askari huyo, Elia Gabriel.
"Mwanafunzi huyo alikuwa akilazimisha kupewa huduma bure, ikiwemo kupanda gari bila kulipa nauli akidai yeye ndiye  askari," amesema Mambosasa.
Amesema uchunguzi unaendelea ili kuwapata rafiki zake ambao inasadikiwa huwa wanashirikiana kufanya uhalifu.

No comments:

Post a Comment