Monday, November 6

Zitto: Tutafungua kesi kupinga vifungu vya sheria ya takwimu


Dar es Salaam. Kiongozi wa  ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema watafungua kesi mahakamani kupinga baadhi ya vifungu vilivyomo katika Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya kitengo cha upelelezi wa makosa ya kifedha kilichopo Kamata, Kariakoo jijini Dar es Salaam, Zitto amesema haiwezekani kukawa na mamlaka moja ya kutoa takwimu.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini amesema tangu kutungwa kwa sheria hiyo imekuwa ikipigiwa kelele kutokana na kuminya uhuru wa wananchi kuchambua takwimu.
"Tunataka kufungua kesi mahakamani kupinga sheria ya takwimu kuzuia watu kuchambua, huko ndiko ukweli utajulikana na wananchi watajua sheria hii ilivyo. Hii itakuwa kesi ya kwanza kwa sheria hii kupelekwa mahakamani," amesema Zitto.
Amesema, "Tuna taarifa ambazo hatukuzitoa, tukifika mahakamani tutazitoa na NBS- (Ofisi ya Taifa ya Takwimu) haiwezi kusema una hatia au la kwa kuwa wao si Mahakama. Sisi tulitumia takwimu zao kuchambua na tumewaeleza polisi kwamba tutawaeleza zaidi tukifika mahakamani."
Zitto ametoa kauli hiyo siku moja baada ya jana Jumapili Novemba 5,2017 Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa kusema mtu mwenye mamlaka ya kutoa takwimu ni ofisi hiyo pekee.
Dk Chuwa katika kipindi maalumu kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Azam kuhusu miaka miwili ya utawala wa Rais John Magufuli aliyeingia Ikulu Novemba 5,2015 alisema takwimu za Taifa ni lazima ziheshimiwe na si kila mtu anastahili kuzitoa.
Zitto akizungumzia tuhuma za uchochezi zinazomkabili amesema, “Nimeripoti leo kama nilivyotakiwa lakini nimeelezwa nirudi tena Ijumaa Novemba 17,2017 wanadai wanasubiri chaji kutoka kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) na baada ya hapo wataona kama watanipeleka mahakamani au la.''
"Lakini kesho, mimi nitakuja hapa (kitengo cha uhalifu wa makosa ya kifedha) saa tatu au saa nne kama nilivyotakiwa. Mtakumbuka natuhumiwa kwa kesi mbili ya sheria ya takwimu na makosa ya mitandao," amesema.
Zitto pia amezungumzia uamuzi wa Jeshi la Polisi la kuiita kamati kuu ya ACT- Wazalendo akisema haina uwezo huo na wao kama walivyoeleza jana katika mkutano na waandishi wa habari watawakilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja na Katibu Mkuu Doroth Semu.
"Polisi hawana uwezo wa kuihoji kamati kuu, ndiyo maana mwenyekiti na katibu mkuu wapo hapa wanaendelea na mahojiano... huwezi kuwaita wajumbe wote wa kamati kuu kwa kuwa mtendaji wa chama ni katibu mkuu na msemaji ni mwenyekiti na ndicho tumekifanya," amesema.

No comments:

Post a Comment