Monday, November 6

Mrithi wa Kabila kupatikana Desemba 2018


Hatimaye Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (CENI) imetangaza kwamba uchaguzi mkuu wa rais unaosubiriwa sana utafanyika Desemba 23, 2018 na siyo Aprili 2019 kama ilivyotangazwa awali.
Tarehe hiyo imetangazwa baada ya ukosoaji mkubwa kwamba Rais Joseph Kabila amekuwa akiahirisha uchaguzi mara kwa mara ili abaki anang’ang’ania madaraka.
Vilevile, CENI imetangaza tarehe hiyo siku chache baada ya balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley kuonya uwezekano wa kuzuka vurugu ikiwa uchaguzi huo hautafayika haraka.
Hata hivyo, upinzani umesema haukubaliani na tarehe hiyo huku ukimtaka Rais Kabila kuondoka madarakani. Uchaguzi mkuu ulipaswa kufanyika Desemba 2016 baada ya mihula miwili ya uongozi wa Kabila kumalizika, lakini umekuwa ukiahirishwa na alikataa kujiuzulu hali iliyoibua mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo.
"Tunaikataa ratiba ya CENI... tunachohitaji sisi kwa sasa ni Kabila kufungasha virago ifikapo Desemba 31, 2017," alisema Augustin Kabuya, msemaji wa chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS). "Utawala huu wa kinyang’anyi unataka tu kuendeleza hali ya ukosefu wa utulivu na majonzi kwa watu."
Baada ya muhula wake kumalizika yalifanyika majadiliano na yakapitishwa makubaliano ya Saint- Sylvestre ukaongezwa muda hadi Desemba 2017 lakini hivi tume ilitangaza kwamba utafanyika Aprili 2019.
Wachanganuzi wa masuala ya siasa wanasema tume ya uchaguzi imechelewa kuandaa uchaguzi, hivyo kuwa na hofu ya kutokea vurugu nchini humo.
Wapigakura watapata fursa ya kumchagua rais, wabunge na viongozi wa serikali za majimbo na kwamba matokeo yatatangazwa katika kipindi cha wiki moja – Desemba 30 – baada ya kupiga kura, lakini matokeo kamili yatatangazwa Januari 9, 2019.

No comments:

Post a Comment