Monday, November 27

Waziri asimamia utekelezaji agizo la Magufuli


Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema ametoka Dodoma kuja Dar es Salaam kusimamia ubomoaji wa majengo ya ofisi za wizara kupisha upanuzi wa barabara.
Kamwelwe amesema leo Jumatatu Novemba 27,2017 kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli na kupisha ujenzi wa barabara pana inayokwenda Chalinze mkoani Pwani.
Amesema atahakikisha majengo yote yaliyo ndani ya hifadhi ya barabara yanabomolewa leo.
Waziri amesema watendaji wake wamejipanga na ofisi yake tayari ilishahamia Dodoma.
"Nimekuja juzi kutoka Dodoma kuja kusimamia ubomoaji wa majengo haya ya Serikali. Jana tumekaa mpaka saa mbili usiku na kukubaliana kwamba leo lazima tubomoe," amesema waziri.
Amesema tayari wananchi wameshabomolewa nyumba kupisha ujenzi wa barabara, hivyo Serikali nayo ni lazima itimize wajibu wake kwa kubomoa majengo yake kama inavyotakiwa.
"Sitaondoka mpaka majengo yote yabomolewe. Ninachotaka leo lazima majengo yawe chini," amesema Kamwelwe.

No comments:

Post a Comment