Monday, November 27

Wanachama CUF waliovuliwa ubunge waliandikia barua Bunge



 Wanachama wanane wa CUF waliovuliwa ubunge wamemwandika barua Katibu wa Bunge ili amjulishe Spika Job Ndugai  kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu ili achukue hatua stahiki ikiwamo kuwafahamisha utaratibu utakaotumika kuwarejesha kwenye nafasi zao.
Wanachama hao ni Miza Haji, Saverina Mwijage, Salma Mwasa, Raisa Mussa, Riziki Mngwali, Hadija Al-Qassmy, Saumu Sakala na  Halima Mohamed.
Novemba 11 mwaka huu Mahakama Kuu ilitoa uamuzi wa kuizuia CUF kujadili kwa namna yoyote ile uanachama wabunge hao na ikatengua utekelezwaji wa kuwafukuzwa kwao.
Akizungumza  na waandishi wa habari leo, Jumatatu Novemba 27, 2017 kwa niaba ya wenzake Mngwali amesema barua hiyo iliandikwa Novemba  20 mwaka huu na tayari imeshawasilishwa katika ofisi ya Bunge.
"Tumemwandikia ili kujua utaratibu utakaotumika kuturejesha bungeni kwa spidi ile ile aliyoitumia kutuengua  katika chombo hicho Julai 25 mwaka huu," amesema Mngwali .
Katika mkutano huo, Mngwali ambaye  aliambatana na Mwijage ambapo amesema wameona ni vyema kuwajulisha wanachama wa CUF na Watanzania kwa ujumla hatua walizochukua baada ya uamuzi wa Mahakama.
Mngwali ambaye anamuunga mkono katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif amesema wana imani Spika Ndugai kwamba atatenda haki katika jambo hilo.

No comments:

Post a Comment