Mahakama ya Uhispania inatarajiwa kutoa waranti wa kuitaka Ubelgiji kumrudisha Carles Puigdemont nchini Uhispania anakotakikana kujibu mashtaka
Waranti wa kukamatwa kwa kiongozi wa Catalonia aliyevuliwa madaraka, Carles Puigdemont, unatarajiwa kutolewa leo, huku Umoja wa Ulaya umekataa kuingilia kati kuhusu waranti hiyo, ukisema kuwa suala hilo ni la mahakama kuamua.
Mahakama ya Uhispania inatarajiwa kutoa waranti wa kuitaka Ubelgiji kumrudisha Carles Puigdemont nchini Uhispania anakotakikana kujibu mashtaka kuhusu madai ya uhaini, uasi na matumizi mabaya ya fedha za umma kuendesha shughuli ya kutaka jimbo lake kujitenga.
Haya yanatokea katika wakati ambapo majaji wamekataa rufaa ya kuwataka wanaharakati wawili wanaowania kujitenga kwa Catalonia, na ambao pia wanakabiliwa na kesi ya uhaini, kuachiliwa kwa dhamana.
Wito wa maandamano zaidi
Hayo yakijiri, shirika linalojiita Bunge la Taifa la Catalonia, ANC, linalounga mkono uhuru wa Catalonia limetoa wito wa maandamano katika jimbo hilo kupinga kuzuiliwa kwa maafisa wa serikali iliyovuliwa madaraka.
Mnamo Alhamisi, jaji katika mahakama kuu ya Uhispania aliwaweka kizuizini viongozi wanane wa serikali ya Puigdemont wakisubiri kesi yao kuanza, hali iliyosababisha maandamano ya takriban watu 20,000 mjini Barcelona.
Mmoja kati ya viongozi waliowekwa ndani, Santi Vila, aliachiliwa kwa dhamana. Villa ambaye alijiuzulu kutoka serikali ya Puidgemont kabla ya tangazo la uhuru, amekuwa akitaka kuwepo mazungumzo na serikali kuu ya Uhispania kama njia ya kupata suluhisho.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuachiliwa huru, Santi amesema "Wenzangu pamoja nami tuko salama, tumetulia, hali tete. Ninafikiri hatua zilizochukuliwa hazifai. Tuna imani kuwa mwishoni tutajitolea kumaliza hali hii mbaya ambayo ninaamini wanademokrasia ulimwenguni hawaelewi."
Ujerumani na EU zapinga Catalonia kujitenga
Juhudi za Catalonia kuufanya mzozo huo kuwa wa kimataifa zimegonga mwamba, baada ya Umoja wa Ulaya kuegemea moja kwa moja upande wa serikali kuu ya Uhispania, ikisema kuwa ni suala la ndani ya nchi hiyo.
Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ni kati ya nchi nyingi za Ulaya ambazo zimepinga wito wa Catalonia kutaka kujitenga, huku taasisi za Umoja wa Ulaya zikiamua kuiunga mkono serikali ya Waziri Mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy.
Punde baada ya tangazo la Catalonia kujitenga, Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker, alionya kuwa umoja huo wenye nchi 28 hauhitaji mianya na migawanyiko zaidi akiongeza kuwa hataki Umoja wa Ulaya kuwa na nchi 95.
Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanahofia suala la Catalonia linaweza kuathiri bara hilo lenye mavuguvugu kadhaa yanayotaka kujitenga ndani ya mataifa wanachama kama vile Uingereza, Ubelgiji na Romania, hali inayoweza kuwa kitisho kikubwa cha umoja wa muungano unaokabiliana sasa na athari za Brexit.
Puigdemont, ambaye Uhispania ilimpokonya madaraka wiki iliyopita kama rais wa jimbo la Catalonia baada ya bunge la Catalonia kutangaza uhuru, alienda Ubelgiji Jumatatu wiki hii na anasema yuko tayari kurejea endapo tu akihakikishiwa kesi dhidi yake zitaendeshwa kwa haki.
No comments:
Post a Comment