Shirikisho la Riadha nchini Tanzania limepata pigo kubwa kwa kumpoteza mwanariadha Ismail Juma Gallet ambaye alikuwa akikimbia zaidi mbio za nusu marathon na kufanya vyema katika mashindano ya Nje ya Nchi.
Ismail Juma alikuwa kati ya wanariadha 19 ambao majina yao yameshawasilishwa ofisi za Kamati ya Olympic Tanzania (TOC) tayari kwa kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Madola (2018 Gold Coast Commonwealth Games) yatakayofanyika mwakani huko nchini Australia na alitegemewa kuingia kambi mwezi huu pamoja na wenzake.
Mwanariadha huyo aliyekuwa anachipukia katika mbio za nusu Marathon, Gallet alifariki Alhamisi katika ajali ya pikipiki iliyotokea wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara.
Vyanzo vya habari Arusha vimesema taarifa hiyo imewachanganya viongozi wa riadha na wanariadha wenzake kutokana na umahiri aliokuwa nao katika mbio za riadha.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania, Wilhelm Gidabuday imesema kuwa Ismail alifariki Alhamisi saa kumi jioni kwa ajali ya pikipiki aliyokuwa akiendesha baada ya kugongana uso kwa uso na Fusso kisha kufariki papo hapo.
No comments:
Post a Comment