Walisema wanatumia njia za kienyeji kuangamiza wadudu hao kwa kuwa dawa za dukani gharama zake ni kubwa na pia haziwezi kuangamiza wadudu vizuri.
Mmoja wa wakulima hao, Ryoba Marwa alisema huchukua mkojo na kuuchanganya kwenye majivu na maji, kisha kumwagilia kwenye mashina ya mahindi.
“Mkojo umeonekana kuua wadudu wanaoshambulia maua ila changamoto iliyopo ni kuukusanya wa kutosha kwa kuwa huwezi kuomba kwa majirani, wanaweza kuhisi unautumia kwa njia za kishirikina, hivyo kinachofanyika ni familia kujisaidia kwenye makopo kisha unakusanywa,” alisema Marwa mkazi wa Kijiji cha Ring’wani.
Ofisa kilimo wilayani Serengeti, Simon Warioba alisema funza hao wanaoshambulia mahindi ni hatari.
“Changamoto iliyopo Serikali haina dawa za kuua hao wadudu na hata wanaotumia njia za asili, wanaangamiza wadudu pekee huku mayai wakiyaacha yakiwa salama,” alisema Warioba.
Alifafanua kuwa kwa kiasi fulani wanasaidia kutoa ushauri kwa wakulima waweze kununua dawa ili kuwaangamiza wadudu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Porini aliwataka wataalamu kwenda vijijini kwa wakulima kuwasaidia kudhibiti wadudu hao kwa kuwa wilaya itakabiliwa na upungufu wa chakula.
No comments:
Post a Comment