Sunday, November 5

China yabadili itikadi, CCM yakwama kwa miaka 40


Unaweza kujiuliza kwa nini chama tawala cha CCM kimeendelea kushikilia itikadi ya siasa za ujamaa na kujitegemea? Pia unaweza kujiuliza itikadi hiyo ilitokea wapi na nani aliileta nchini? Jibu ni rahisi tu urafiki wa Tanzania na China unatokana na itikadi hiyo.
Historia inaonyesha ziara ya kwanza ya Mwalimu Nyerere aliyoifanya nchini China 1966, wakati huo akiwa Rais wa Tanganyika ndiyo iliyompa somo la siasa za ujamaa na kujitegemea na aliporejea nchini alianzisha vijiji vya ujamaa.
Urafiki wa nchi hizo, uliojengwa kwa msingi wa itikadi hiyo, umedumu tangu zama za kina Mao Tse Tung, Chou Enlai, Deng Xiaoping, Hu Jintao hadi wakati huu wa Xi Jinping.
Lakini, China ambayo ndiyo waasisi wa itikadi ya siasa hizo, wameshabadili itikadi hiyo mara kadhaa na kwenye mkutano wake wa mwezi uliopita wamefanya maboresho mengine kulingana na hali ya sasa ya mabadiliko ya kiuchumi duniani.
Baada ya kifo cha muasisi wake, Mao Zedong, nchi hiyo ilibadili itikadi yake na kuja na ujamaa wenye sifa za China, wakimaanisha utajiri siyo dhambi na kuruhusu Wachina kuwa matajiri, lakini wakitakiwa kuheshimu mihimili mikuu inayoongoza uchumi wa taifa hilo.
Kwenye mkutano wa CPC wa mwezi uliopita, Rais Xi Jinping amekuja na itikadi mpya kwa kuboresha ya zamani na kuwa ujamaa wenye sifa za China kwa zama mpya. Hapa China imelenga katika kujiimarisha kiuchumi, biashara, ulinzi, usalama sambamba na uhusiano wa kimataifa.
Rwenye mkutano huo uliofanyika jijini Beijing, Rais Jinping alisema katika miaka mitano iliyopita CPC ilitekeleza mawazo na mikakati mingi mipya ya utawala.
Alisema hivi sasa China inachangia asilimia 30 ya ongezeko la uchumi wa dunia, na kufanikiwa kuwasaidia watu zaidi ya milioni 60 kuondokana na umaskini.
CPC ambayo imekuwa ikifanya maboresho ya itikadi kila inapobidi, kwenye mkutano wake mkuu wa 12 uliofanyika zaidi ya miaka 30 iliyopita, ulitoa uamuzi wa kujenga Ujamaa wenye umaalumu wa China baada ya utekelezaji wa sera ya mageuzi na ufunguaji milango.
Rais Jinping anasema mkutano huu wa 19, umerithi nia ya awali ya kuendeleza na kufanya uvumbuzi kwa kutangaza Ujamaa wenye umaalumu wa China katika kipindi kipya.
“Nia ya Ujamaa wenye umaalumu wa China katika kipindi kipya imedhihirisha umuhimu wa kushikilia na kuendeleza Ujamaa wenye umaalumu wa China, na jukumu kuu ni kutimiza mambo ya kisasa ya kijamaa na kustawisha upya Taifa la China, baada ya kumaliza kazi ya kujenga jamii yenye maisha bora kwa pande zote, China itaendelezwa na kuwa nchi nzuri ya kisasa ya kijamaa yenye utajiri, nguvu, demokrasia, ustaarabu na masikilizano kwa hatua mbili ifikapo katikati ya karne hii.
“Pia, imedhihirisha kuwa katika kipindi kipya, changamoto kuu inayoikabili jamii yetu ni pengo kati ya mahitaji ya watu ya kuwa na maisha bora na kutokuwa na uwiano wa maendeleo ya kutosha,” alisema Jinping katika hotuba yake.
“Hivyo, tunapaswa kushikilia wazo la kujiendeleza kwa ajili ya wananchi wetu, kuhimiza maendeleo ya watu katika kila upande na kupata maisha bora kwa wananchi wote.”
Alisema miaka mitano iliyopita, mkutano mkuu wa 18 ulidhihirisha malengo mawili ya miaka 100, ambayo ni kukamilisha kazi ya kujenga jamii yenye maisha bora hadi kufikia mwaka 2021 wakati itakapotimia miaka 100 tangu CPC ianzishwe na kuijenga China iwe nchi ya kisasa ya kijamaa mwaka 2049 wakati itakapotimia miaka 100 tangu Jamhuri ya Watu wa China ianzishwe.
INAENDELEA UK 26
INATOKA UK 25
“Kwa kuchambua hali za ndani na duniani na mazingira ya maendeleo ya nchi yetu, tunaweza kupanga kazi katika vipindi viwili kati ya mwaka 2020 na katikati ya karne hii. Kipindi cha kwanza ni kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2035, baada ya kumaliza kazi ya kujenga jamii yenye maisha bora kwa pande zote, tutaijenga China kuwa nchi ya kisasa ya kijamaa kwa kutumia miaka 15.
“Kipindi cha pili ni kuanzia mwaka 2035 hadi katikati ya karne hii, baada ya kuijenga China kuwa nchi ya kisasa ya kijamaa, tutaendelea kuiendeleza kuwa nchi nzuri ya kisasa ya kijamaa yenye utajiri, nguvu, demokrasia, ustaarabu na masikilizano,” anasema Rais Jinping.
Ukilinganishwa na mpango wa zamani, ripoti iliyotolewa kwenye mkutano wa 19 imerekebisha lengo litakalotimizwa ifikapo katikati ya karne hii kwaq nguvu na vizuri zaidi, hali ambayo inamaanisha kuwa chama cha Kikomunisti kinatilia maanani uhifadhi wa mazingira.
Rais Jinping anasema China itashikilia njia ya kujiendeleza kwa amani, kuhimiza kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja, kutekeleza sera za kidiplomasi za amani za kujitawala, ujiamulia na kuendeleza uhusiano kote duniani.
CCM na itikadi ya Ujamaa
Wakati chama CPC ikifanya maboresho ya mara kwa mara ya itikadi yake, CCM iliyochukua itikadi hiyo kutoka China na kuiingiza kwenye katiba yake mwaka 1977, bado inaendelea na itikadi hiyo bila kuifanyia maboresho.
Itikadi hiyo kwa mara ya kwanza ilipewa nguvu za kisera mwaka 1967, lilipotangazwa Azimio la Arusha ambapo uchumi uliwekwa mikononi mwa umma. Itikadi hiyo pia ilisisitiza umuhimu wa kuishi pamoja hasa katika vijiji vya Ujamaa.
Nyerere alitumia Ujamaa kama msingi wa mradi wa maendeleo ya Taifa. Aliitafsiri dhana ya Ujamaa kuwa mfumo wa usimamizi wa kisiasa na wa kiuchumi kwa namna mbalimbali:
Kuweko kwa mfumo wa chama kimoja chini ya uongozi wa CCM ili kusaidia katika kuimarisha mshikamano wa kujitegemea kwa Tanzania iliyokuwa tu imejipatia uhuru.
Ustawishaji wa usawa kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kuweko kwa demokrasia kuu; kukomesha ubaguzi kwa misingi ya hali ya mtu; na kuzifanya sekta muhimu za uchumi kufikia Taifa zima.
Pia, aliutumia kupeleka uzalishaji katika vijiji, ambapo ilifanya uwezo wa uzalishaji wa aina zote kufanyika kwa pamoja. Kukuza kujitegemea kwa Tanzania kwa njia mbili: mabadiliko ya kiuchumi na mitazamo ya kiutamaduni. Kiuchumi, kila mtu angekifanyia kikundi chote kazi na kujifanyia yeye mwenyewe; kiutamaduni, ni lazima Watanzania wajifunze kujikomboa kutoka kwa utegemezi wa nchi za Ulaya.
Kwa Nyerere, hii ilijumuisha Watanzania kujifunza kujifanyia mambo wao wenyewe na kujifunza kuridhika na kile ambacho wangeweza kufikia kama nchi huru. Utekelezaji wa elimu bila malipo na ya lazima kwa Watanzania wote ili kuwahamasisha wananchi kuhusu kanuni za Ujamaa.
Hata hivyo, Ujamaa (kama vile mipango mingine ya uzalishaji wa pamoja) ulipunguza uzalishaji hata kutia shaka juu ya uwezo wake wa kustawisha uchumi.
Ujamaa kushindwa
Hatimaye sababu mbalimbali zilifanya Ujamaa uonekane umeshindikana kiuchumi. Kati ya hizo, tatizo la kimataifa la mafuta miaka ya 1970, anguko la bei ya bidhaa zilizozalishwa nchini (hasa kahawa na katani), utovu wa uwekezaji kutoka nje ya nchi na vita vya Uganda na Tanzania miaka 1978-1979 vilivyofyonza mtaji muhimu, na miaka miwili mfululizo ya ukame.
Kufikia mwaka 1985 ilikuwa wazi kwamba Ujamaa ulishindwa kutoa Tanzania nje ya ufukara wake. Hata hivyo, 1985 wakati Nyerere alipomwachia mamlaka Ali Hassan Mwinyi.
Mwinyi baada ya kuchukua madaraka alitangaza utaratibu wa soko huria na kuanzia hapo CCM imekuwa ikiimba majukwani na kwenye katiba yake kwamba inafuata siasa za Ujamaa na Kujitegemea, lakini kila kiongozi aliyeshika madaraka ya nchi hakuna aliyetekeleza itikadi hiyo kwa vitendo wala kuiboresha iendane na wakati, licha ya kufanyika maboresho mengine ya muundo wa chama.
Wasemavyo wachambuzi
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa wa Benson Bana anasema CPC ni tofauti sana na CCM na wala haifanani kwa aina yoyote ile.
Anasema katika Bara la Afrika hakuna chama chenye itikadi kwani itikadi iliondoka mara tu baada ya kuruhusu itikadi ya uchumi na siasa na kwa CCM ambayo inashambuliwa kila kona haiwezi kuwa na itikadi.
“Huwezi kusema CCM ina itikadi ya ujamaa, ujamaa gani ambao upo CCM, wanasema tu lakini Afrika hii hakuna chama chenye itikadi na wala hatuwezi kuifananisha CCM na Chama cha Kikomunist, havifanani kwa lolote,” anasema Profesa Bana na kuongeza
“Wanajaribu kuwaeleza tu wananchi lakini CCM inayoshambuliwa mbele, nyuma, kushoto, kulia na vyama vya upinzani huwezi kusema ina itikadi, CCM iliyojaa mabwanyenye…kama nilivyosema tusikifananishe chama hicho na CCM.”
Mtaalamu wa masuasa ya kisiasa na mahusiano ya kimataifa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Hamad Salim anasema suala la itikadi lilitoweka hata kabla ya kifo cha Mwalimu Jiulus Nyerere.
“Chama na Serikali kwa sasa hakuna itikadi ya ujamaa ingawa msingi mkuu wa chama ni kuwatetea wanyonge lakini tukiangalia uongozi wa chama hawafanani na itikadi ya ujamaa wanayoisema,” anasema Dk Salim.
“Tumebakiza ujamaa katika maandiko lakini kivitendo hakuna, ujamaa wa mtu kupata mshahara milioni 40 huku mwingine anapata laki tatu? Ndio manaa nasema CCM na Serikali ilikwisha kuondoka huko na Rais anajaribu kurudisha katika ujamaa ila ni ngumu,” anaongeza
Mchambuzi huyo anatolea mfano risasi, kuwa ikishatoka ndani ya silaha kuirudisha ni kazi kweli kweli.

No comments:

Post a Comment