Wakazi wa eneo lililojitenga na taifa la Somalia, Somaliland, leo wanapiga kura ya kumchagua rais wao katika awamu ya tatu. Wamefanya uchaguzi huo wakidhamiria kudhihirisha kuwa na sifa za kidemokrasia
Pia wanafanya uchaguzi huo wakisisitiza zaidi kupata uhuru wao na kutambulika kimataifa.
Eneo hilo lililo Kaskazini mwa nchi hiyo, lenye kabila zenye kujitukuza na imara ukiliganisha na maeneo mengine ya Somalia, lilijitenga mnamo mwaka 1991 na tangu wakati huo linasisitiza kutambuliwa kimataifa.
Wagombea watatu, wanawania nafasi hiyo ya urais, akiwamo mwanasiasa, Muse Bihi, wa chama tawala cha Kulmiye na mpinzani Abdirahman Iro na Faysal Ali Warabe, ambaye aliangushwa katika uchaguzi uliopita wa 2010.
Mchakato wa upigaji kura ulianza kwa amani asubuhi ya leo, na tuna imani kuwa uchaguzi huu utakuwa wa kipekee na muhimu kwa nchi nzima,`` amesema Iro wakati akipiga kura.
Uchaguzi katika eneo hilo hufanywa kila baada ya miaka mitano, hata hivyo, upigaji kura uliahirishwa kwa miaka miwili kutokana na ukame na masuala ya kiufundi. Rais wa sasa, Ahmed Mohamud Silaanyo, si mgombea katika uchaguzi huu.
Somaliland ina sifa tofauti na taifa la Somalia
Somaliland ina historia ya kuwa na amani, uchaguzi wenye sifa na mabadiliko makubwa ya kidemokrasia, ambayo yameifanya kuwa tofauti na taifa la Somalia, na hata nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Katika uchaguzi uliofanyika Somalia mwaka huu, Rais alichaguliwa katika mchakato ambapo viongozi maalum wa kimila walioteuliwa ndio walioruhusiwa kupiga kura.
Kabla ya uchaguzi huu wa Somaliland, wagombea wakuu wawili, walishiriki mjadala uliorushwa katikatelevisheni na kueleza ajenda zao za kisiasa, wakijikita zaidi katika uchumi, ajira na kutambulika kwa nchi hiyo kimataifa.
``Huu ni uchaguzi muhimu sana, kwa vijana, kwani wanahitaji kiongozi ambaye anaweza kuimarisha uchumi na kuleta ajira, ili kila mtu aishi nchini kwake akifurahia maisha,`` amesema mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Ismail Mohammed.
Upigaji kura unatajwa kuwa muhimu ambapo watu 700,00 walijisajiliwa kwa kutumia mfumo wa elektroniki wa Biometric .
Hata hivyo, uamuzi wa mamlaka za eneo hilo kufunga mitandao yote ya kijamii wakati upigaji kura hadi vituo vitakapofungwa saa 12 jioni kwa saa za Africa Mashariki, ulikosolewa na taasisi ya Human Right Watch wiki iliyopita.
Msemaji wa tume ya uchaguzi, Said Ali Muse alifafanua akisema hatua hiyo ya uzimwaji wa mitandao ya kijamii ni muhimu ili kuzuia muingiliano kutoka katika mipaka ya utawala wa Somalia na udadisi wa matokeo hayo.
Somaliland ambayo ni koloni la zamani la Uingereza, ilipata uhuru wake, mwaka 1960 na baadaye ikajiunga na Somalia . Mwaka 1991, baada ya miaka kadhaa ya vita na serikali kuu mjini Mogadishu, Somaliland ilijitangazia uhuru wake na kujitenga na Somalia.
No comments:
Post a Comment