WACHIMBAJI wadogo wa dhahabu Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, wameunga mkono msimamo wa Rais, Dk. John Magufuli wa kutaka madini yawanufaishe Watanzania.
Pamoja na hayo, wanasema kuna haja ya baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na wawekezaji wa Kampuni ya Acacia, yatambulike kisheria kwa ajili ya kuwanufaisha zaidi Watanzania.
Wakizungumza jana wilayani hapa, baadhi ya wachimbaji hao walisema Rais Dk. Magufuli ameonyesha njia ya kuwasaidia wananchi tofauti na ilivyokuwa zamani.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini, Mkoa wa Mbeya (Mberema), Reonard Manyesha, alisema msimamo uliowekwa na Rais Dk. Magufuli wa kugawana faida ya madini unaonyesha ni kwa kiasi gani anavyoguswa na maisha ya wananchi.
“Lakini, yale makubaliano ya kugawana hamsini kwa hamsini katika ukatwaji wa kodi kutoka kwenye makampuni ya uchimbaji wa madini, yanatakiwa yaandikwe kisheria.
“Kama hilo halitaandikwa kisheria na kusimamiwa na wataalamu wa sheria, itakuwa ni sawa na bure kwani rais muda wake ukifika mwisho, ataondoka madarakani na yatajirudia yaliyokuwa yakifanyika siku zilizopita,” alisema Manyesha.
Naye mchimbaji Edson Kibusu, aliiambia MTANZANIA, kwamba msimamo uliowekwa na Serikali katika sekta ya madini utawasaidia kwa kuwa walikuwa wakifanya biashara hiyo kwa hasara kutokana na mazingira mabovu yaliyokuwapo.
Kibusu ambaye ni mchimbaji kutoka Kijiji cha Itumbi, alisema wamekuwa wakifanya shughuli hiyo kwa shida, lakini kwa sasa wameanza kuona mafanikio kupitia biashara hiyo.
Mchimbaji mwingine, Joshua Mwakyusa, mkazi wa Chunya Mjini, alisema wachimbaji wamekuwa na nguvu ya kuendelea kufanya kazi baada msimamo unaoonyeshwa na Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment