NA BASHIR YAKUB -
Umenunua kiwanja au nyumba. Aliyekuuzia amekuhahakikishia kuwa kiwanja/nyumba hiyo iko salama na haina mgogoro wowote. Mbali na mgogoro pia amekuhakikishia kuwa kiwanja/nyumba hiyo hajaiweka rehani popote ili kuchukua mkopo.
Amekuhakikishia kuwa mpaka wakati unanunua kiwanja/nyumba hiyo, ni kuwa iko salama na haijashikiliwa na benki au taasisi yoyote ya fedha kwa ajili ya mkopo.
Au pengine hukuuliza kabisa kama kuna deni lolote, umejikuta tu umenunua bila kuuliza swali kama hilo. Baadae sasa ndio unagundua kuwa kiwanja/nyumba uliyonunua kuna taasisi moja ya fedha ambapo aliyekuuuzia alichukua mkopo na kuiweka dhamana/rehani na bado hajamalizia mkopo huo.
Taasisi hiyo inakuonesha nyaraka halali za kushikilia kiwanja/nyumba hiyo kama dhamana muda mrefu hata kabla wewe hujanunua. Na kwa bahati mbaya aliyekuuzia hujui tena alipo au bahati nzuri unajua alipo.
Lakini hata ukijua alipo, tayari umeishanunua na hela ulishampa na kila kitu kilikwishakamilika. Nini kinakusaidia kukutoa katika hali hii ambayo sasa unaelekea kuingia katika mgogoro mkubwa wenye sura ya hasara.
Sheria namba 4 ya 199, Sheria ya ardhi itatupatia majibu ya jambo hili.
1.UNUNUZI WA AINA HIYO UNAVYOTAMBULIKA KISHERIA.
Ununuzi wa aina hiyo unatambulika kama aina ya ununuzi ambao unaingilia haki ya mtoa mkopo. Kifungu cha 69(1) cha sheria hiyo kinauita ununuzi huo kama ununuzi unaolenga kupora/kuharibu(defeat) haki ya mtoa mkopo.
Mtoa mkopo hapa ni benki au taasisi nyingine ya fedha iliyotoa mkopo.
Kwahiyo kujikuta umenunua eneo lenye mazingira ya namna hiyo hadhi yake ni kama ilivyoelezwa hapa juu.
2. HAKI ALIZONAZO MTOA MKOPO DHIDI YAKO MNUNUZI.
Kifungu cha 7(1)( cha sheria tajwa kinasema kuwa ikiwa mtoa mkopo atagundua kuwa rehani aliyoshikilia imeuzwa bila taarifa/kuhusishwa, basi atakuwa na haki ya kwenda mahakamani na kudai kutenguliwa(set aside) kwa ununuzi huo. Ununuzi wako wa eneo husika utatenguliwa na mahakama.
Kwenda mahakamani ni baada ya kukutaka mnunuzi uondoke au uachie hiyo ardhi kwakuwa ilikuwa rehani na pengine ukakataa. Ikiwa utakubali kuachia kirahisi na kukubali hasara basi haitakuwepo haja ya mtoa mkopo kwenda mahakamani.
Lakini ikiwa utakaidi basi ataiomba mahakama itengue ununuzi wako kwakuwa umeuziwa wakati akiwa ameshikilia eneo hilo kama dhamana/rehani.
3. JE WEWE MNUNUZI UNA HAKI GANI.
Kifungu cha 71 ( 1) kinaeleza jambo moja ambalo linaweza kukusaidia kama mnunuzi katika mazingira kama haya. Ni kuwa utatakiwa kuthibitisha kuwa wakati unanunua haukujua kabisa kama nyumba/kiwanja hicho kiliwekwa rehani sehemu. Ni kazi yako kuhakikisha unathibitisha kutokufahamu kabisa lolote kuhusu kuwekwa kwake rehani wakati ukinunua.
Ikiwa utaweza kulithibitisha hilo basi kifungu hicho kinaeleza kuwa mahakama haitatoa amri ya kutengua ununuzi wako. Hilo ndilo linaloweza kukuokoa na kadhia hii.
Hata hivyo kuthibitisha jambo hili kuwa hukujua kuna misingi yake. Kifungu cha 71(2) kimetaja msingi mkuu wa kuthibitisha kuwa hukujua ni kuonesha kwa ushahidi kuwa kabla ya kununua ulifanya utafiti wa kutosha(due diligence/actual and constructive notice), na unaokidhi viwango vya kisheria ili kujiridhisha kuwa eneo unalonunua halina tatizo/mgogoro.
Moja ya hatua unayotakiwa kuthibitisha ni kuonesha kuwa ulifanya “official search” na taratibu nyingine ambazo zinakidhi viwango vya kisheria katika kujiridhisha kabla ya kununua.
Basi ukiweza kuthibitisha hayo ununuzi wako hautatenguliwa. Na hapo ndipo tunaposisitiza sana kuhusu kufuata taratibu za kisheria za manunuzi ya ardhi lengo likiwa kukuweka salama na hatari kama hizi mbeleni. Tujihadhari.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE. 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment