Thursday, November 16

TAKUKURU KILIMANJARO YAMSHIKILIA DAKTARI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA,MAWENZI KWA TUHUMA ZA RUSHWA

Anaandika Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini. 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)mkoani Kilimanjaro,imemtia mbaroni Daktari wa Hospital ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi akituhumiwa kudai na kupokea rushwa ya shilingi 150,000.

Daktari huyo,Deogratias Godfrey Urio,alikamatwa jana katika mji mdogo wa Himo kwenye baa maarufu ya Mombasa High Way baada ya kuwekewa mtego na makachero wa takukuru mkoani Kilimanjaro.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro(RBC),Holle Makungu imesema kuwa kukamatwa kwa daktari huyo kunatokana na malalamiko ya ndugu wa mgonjwa aliyekuwa akipigwa dana dana kupatiwa huduma ya upasuaji katika hospital hiyo.

Makungu ameeleza katika taarifa yake kuwa,mgonjwa huyo alikuwa akihitaji kufanyiwa upasuaji wa uvimbe katika kizazi chake tangu oktoba mwaka huu baada ya kufanyiwa vipimo kwenye hospital hiyo na kubainika kuwepo kwa uvimbe.

Lakini licha ya kubainika kuwepo na uvimbe huo,mgonjwa huyo hakuweza kupata tiba haraka baada ya kuelezwa na daktari huyo kuwa hawezi kufanyiwa upasuaji huo hadi hapo atakapotoa fedha hizo.

Makungu ameeleza kuwa,baada ya taarifa hizo kuwafikia,mtego uliandaliwa na daktari huyo aliweza kutiwa mbaroni jana Novemba 15 akiwa kwenye baa hiyo ya Mombasa High Way.

“Tunaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na atafikishwa mahakamani mara tu uchunguzi utakapokamilika,takukuru inatoa rai kwa madaktari na wauguzi katika hospital ya Mawezi kuzingatia viapo vyao ili Mawenzi iwe hospital ya kuigwa kwa huduma bora”,amesema makungu.

Mkuu huyo wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro akahitimisha taarifa yake kwa kuonya kuwa kwa wale wachache watakaoendelea kutozingatia viapo vyao,watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria na pia kuwataka waajiri wao wachukue hatua kali za kinidhamu dhidi ya watumishi hao .

No comments:

Post a Comment