Thursday, November 16

TUKIO LA LULU LITUFUMBUE MACHO WAZAZI, JAMII


HIVI majuzi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilimhukumu mwigizaji wa Filamu za Kibongo, Elizabeth Michael  maarufu kwa jina la Lulu, kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia Steven Kanumba. Tukio hili lililotokea Aprili 7, 2012 nyumbani kwa marehemu Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.
Kabla ya hukumu hiyo, wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala alipopewa nafasi ya kumtetea mteja wake na Jaji Sam Rumanyika aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alisema Lulu anategemewa na familia yake na kwamba wakati tukio hilo linatokea, alikuwa bado mdogo.
Jaji Rumanyika alisema kifo cha Kanumba kilitokana na ugomvi hivyo amejiridhisha kwamba mtuhumiwa aliua bila kukusudia. Akaongeza kuwa wivu wa mapenzi ni maangamizi.
Tukio hili la Lulu linatukumbusha wazazi kuwa makini na vijana wetu, siwezi kusema kuwa Mama Lulu alishindwa kumlea mwanawe katika maadili mema, la hasha! Lakini nathubutu kusema kuwa uhuru aliomuachia huenda ikawa ni sababu kubwa ya matatizo yote haya kwa mtoto wake.
Wakati Lulu ameanza kujihusisha na masuala ya mapenzi, umri wake ulikuwa bado hauruhusu, lakini jambo la kushangaza ni kwamba si wazazi wake wala jamii iliyomzunguka iliyothubutu kunyanyua mdomo na kumuasa juu mienendo yake huku mwenyewe akijua fika kwamba umri wake hauruhusu.
Licha ya kutumia vifungu mbalimbali vya sheria hadi Lulu kutiwa hatiani, Jaji Rumanyika pia alitoa hukumu hiyo akiamini kuwa msichana huyu alijiingiza kwenye mambo ya kikubwa akiwa bado mdogo naye kuona kuwa ni mambo ya kawaida.
Hakika, Lulu alikosa ulinzi wa kutosha kutoka kwa wazazi wake, ambao hata hawakushtuka wakati mtoto wao amegeuzwa mke wa mtu.
Hawakushtuka hata mtoto wao alipoamua kuzunguka ovyo usiku wa manane na kwenda kwa ‘mvulana wake’.
Hata wanaharakati, waandishi wa habari na jamii iliyomzunguka walidiriki kukaa kimya – hawakuthubutu hata kukemea tabia ya mtoto huyu, hata pale alipoandikwa kwenye vyombo vya habari akituhumiwa kutembea na huyu na yule.
Sifurahii tukia lililomkuta kijana huyu, bali nawaasa wazazi kutumia fursa hii kubadili tabia, kuzungumza na watoto wetu juu ya mienendo yao.
Watoto nao wanapaswa kusikiliza wanayoambiwa na wakubwa wao, wasidharau ule usemi usemao: “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.”

No comments:

Post a Comment