Thursday, November 16

SHULE 10 ZAFUNGIWA KWA KUTOKAMILISHA USAJILI

 


HALMASHAURI ya Mji wa Bariadi   imezifungia shule 10 zinazodaiwa kujiendesha kinyemela.
Shule hizo zinadaiwa kutoa mafunzo kwa watoto bila ya kukamilisha taratibu za usajili kama inavyotakiwa.
Hatua ya kuzifungia shule hizo inatokana na halmashauri  kupata malalamiko   kutoka kwa wazazi na walezi wa watoto waliokuwa wakisoma katika shule hizo na kukwama kwa watoto wao kufanya mitihani ya  taifa.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Merkzedeck Humbe, alikuwa akizungumza juzi wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi za vyeti na ngao kwa shule za msingi zilizofanya vizuri kwenye mtihani wa  ttaifa wa darasa la saba mwaka 2016.
Alisema shule hizo zimefungiwa na kupigwa marufuku kuendelea kutoa huduma ya mafunzo kwa watoto na  baadhi zimepewa miezi sita kukamilisha taratibu ili kupatiwa usajili rasmi.
Humbe alisema   baadhi ya shule hizo zimekuwa zikitoa mafunzo kinyume na mitaala ya elimu  na hazina walimu wenye uwezo,.
“Moja ya shule hizo imefundisha watoto hadi darasa la nne, kwenye mtihani wa taifa watoto hao hawakufanya mitihani kutokana na kutotambulika na serikali.
“Wazazi walilalamika huku fedha walizotumia kulipia ada zikipotea bure na walipokuja  ofisini kwetu tuliwaambia ukweli,” alisema Humbe.
Mkurugenzi huyo alizitaja shule hizo kuwa ni Prophetic English Mediam School, Emmanuel English Mediam School, Free Pentecoste School, Gosheni English Mediam School, Aziza English Mediam School, Sakwi English Mediam School.
Nyingine ni Baptist English Mediam School, Sinane English Mediam School, Kenest English Mediam School, pamoja na Kaliwa English Mediam School, zote zikiwa za Mjini Bariadi.
Mkurugenzi   alitoa onyo kali kwa watakaokiuka maagizo ya serikali kwa kuendelea kuendesha shule hizo bila ya kufuata utaratibu.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa ikiwa shule hizo zitaendelea kufundisha ili hatua kali zaidi zichukuliwe kwa wamiliki.
Awali,   Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo, Juma Mnyeti, alisema   halmashauri imemaliza tatizo la watoto wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kutoka wanafunzi 2869 mwaka 2015 hadi wanafunzi 0 mwaka 2017.

No comments:

Post a Comment