Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kwamba uchaguzi mkuu nchini humo sasa utafanyika Desemba 2018.
Hatua hiyo hata hivyo haijaufurahisha upinzani ambao unataka Rais Joseph Kabila aondoke madarakani.
Uchaguzi ulipangiwa kufanyika mwaka huu chini ya makubaliano yaliyoafikiwa mwaka jana, lakini tume ya uchaguzi imechelewa kuandaa uchaguzi.
Awali, ilikuwa imetangaza kwamba uchaguzi unaweza tu kufanyika mwaka 2019.
Lakini sasa tume hiyo imetangaza kwamba uchaguzi wa rais, wabunge na viongozi wa serikali za majimbo utafanyika mnamo 23 Desemba, 2018.
Lakini upinzani umepinga tarehe hiyo na kusema haikubaliki.
Upinzani umesisitiza kwamba ni sharti Rais Kabila aonondoke madarakani kufikia mwisho wa mwaka huu.
"Tunaikataa kalenda iliyotolewa ya uchaguzi...tunachokitaka kwa sasa hivi ni Kabila kuondoka madarakani kufikia 31 Desemba, 2017," alisema Augustin Kabuya, msemaji wa chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS).
Afisa wa tume ya uchaguzi Jean-Pierre Kalamba amesema matokeo ya muda yatatangazwa katika kipindi cha wiki moja baada ya upigaji kura kufanyika, mnamo tarehe 30 Desemba, lakini matokeo kamili yatatangazwa tarehe 9 januari, 2019.
Rais mpya anatarajiwa kuapishwa 12 Januari, 2019.
Kiongozi wa upinzani Moise Katumbi amepuuzilia mbali mpango huo wa uchaguzi.
"Utawala huu dhalimu unataka kuendeleza ukosefu wa uthabiti na dhiki dhidi ya wananchi," Katumbi amesema.
"Hatutakubali kalenda hii. Kabila sharti aondoke," aliandika kwenye Twitter.
Hali ya wasiwasi imekuwepo nchini humo tangu Kabila alipokosa kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka jana baada ya kumalizika kwa muhula wake wa pili na wa mwisho.
Tume ya uchaguzi ilikuwa imesema haiwezekani kuandaa uchaguzi kwa wakati kutokana na matatizo ya kuandaa sajili ya wapiga kura, hasa eneo lenye misukosuko la Kasai katikati mwa nchi hiyo.
Tangazo la Jumapili limetolewa siku kumi baada ya ziara ya balzoi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa
Nikki Haley ambaye aliitaka DR Congo kufanya uchaguzi mwaka ujao.
Uingereza, Ufaransa, Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa wale ambao walitaka tarehe mpya ya uchaguzi itangazwe.
No comments:
Post a Comment