Muleba. Polisi wanamshikiliwa mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Kagoma wilayani Muleba, kwa kosa la kuwaua pacha wake.
Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Augustino Olomi alisema tukio hilo lilitokea Novemba 14 baada ya mwanamke huyo kuwanyonga watoto wake na kusingizia kuwa wamefariki dunia. “Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mauaji ya watoto hao, itakapojulikana hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisema Olomi.
Naye mwenyekiti msaidizi wa kijiji hicho, Patrick Luhosho alieleza mwanamke huyo aliwaua watoto wake hao wenye mwezi mmoja na kuzika miili yao Kitongoji cha Nundu kilichopo katikati ya kijiji jirani cha Buhaya.
Luhosho alisema taarifa za tukio hilo zilipatikana baada ya ndugu kuanza kuhoji walipowekwa watoto hao na kwamba, aliwaeleza kuwa wamefariki.
“Taarifa hizo ziliwashtua wananchi kwani hivi karibuni alikuwa akidai anakosa huduma ya kuwatunza pacha hao kutokana na ugumu wa maisha,” alisema.
Alisema baada ya polisi kuwasili kijijini hapo kufanya uchunguzi, aliwaeleza kuwa watoto walifariki na kuzikwa Kijiji cha Nshamba lakini walipofuatilia walibaini ni uongo. “Wananchi wanaendelea kutafuta miili hiyo kwa kutumia mbwa,” alisema Luhosho.
Mwanamke huyo ambaye ni uzazi wake wa tano, anadaiwa kuwaua watoto wake hao ambao amezaa na mwanaume ambaye hajafahamiki baada ya kuachika kwenye ndoa yake ambako alizaa watoto wanne.
No comments:
Post a Comment