Friday, November 17

MAONI YA MHARIRI: Viongozi Afrika wajifunze kutoka Zimbabwe


Unaweza ukawa ndio mwisho wa zama za utawala wa Rais Robert Mugabe, ambaye ameitawala Zimbabwe tangu mwaka 1980.
Mpaka jana jioni, Mugabe alikuwa kizuizini nyumbani kwake baada ya jeshi la nchi hiyo kuingia mitaani, huku likidai kuwa na dhamira ya kuwashughulikia linalowaita wahalifu wanaomzunguka rais huyo.
Kimsingi, hatua ya jeshi hilo inaonekana kuleta mjadala mkubwa kutoka kwa watu wengi ndani na hata nje ya bara la Afrika.
Kuna wanaounga mkono utawala wa Mugabe na kuna ambao wanapinga kwa madai kuwa ametawala muda mrefu.
Si Mugabe pekee, duniani kuna viongozi kadhaa ambao wamekaa madarakani kwa muda mrefu ama kwa sababu katiba zao hazijaweka ukomo au zimebadilishwa mara kwa mara kwa lengo la kuwabeba.
Kwa viongozi ving’ang’anizi kama Mugabe, kibaya zaidi kwao si tu kujimilikisha uongozi wa nchi, lakini wanaporuhusu watu wao wa karibu hususan wanafamilia kufanya wayatakayo. Wanafamilia hawa hawaguswi na vyombo vya dola, hakuna anayewanyooshea kidole hata kama wanayofanya yanazipeleka nchi zao shimoni. Ikumbuke kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho; viongozi wajifunze kukubali kuwapo kwa ukomo wa madaraka. Hakuna mwenye hakimiliki ya kuongoza nchi hata kama atakuwa ameifanyia makubwa nchi yake.
Tujifunze kutoka kwa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye kwa mchango aliotoa katika uhuru wa Tanzania, pengine mpaka sasa nchi hii ingeweza kuwa chini ya utawala wa kizazi chake. Harakati za kufa na kupona alizofanya na waasisi wenzake yeye akiwa kama kinara hazikumpa jeuri za kuona ana haki ya kutawala nchi milele; ndio maana aliamua kung’atuka na kuwapisha wengine kuongoza nchi.
Mwalimu Nyerere hakung’atuka kwa sababu alichokwa, ila alisukumwa na busara ya kuona kuwa kulikuwa na haja ya kumpisha mwingine kuongoza nchi. Kitendo cha aina hii pia kilifanywa na Nelson Mandela aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini.
Mugabe (93) licha ya kuongoza kwa muda mrefu wa miaka 37, alitaka kumuachia madaraka mkewe Grace jambo ambalo linaonekana kupingwa na watu wengi wakiwemo wanajeshi hao ambao wamemuweka kizuizini. Wanaompinga wanasema Zimbabwe ilihitaji mtu mpya mwenye maono mapya.
Kadhia ya Zimbabwe haina budi kuwa tanbihi kwa viongozi wengine barani Afrika; bara ambalo mpaka tunaandika maoni haya limegubikwa na viongozi wengi wabinafsi na wapenda madaraka.
Rai yetu kwa viongozi wa Afrika na dunia kwa ujumla, wakubali kuwapo kwa mfumo wa kubadilishana madaraka. Na hii ndiyo demokrasia kama anavyosema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) kuwa ni lazima serikali za Afrika ziweke sawa mazingira ya ushindani wa kisiasa katika kuongoza nchi.
Bara la Afrika linahitaji maendeleo stahimilivu ili kuwakomboa wananchi wake katika lindi la changamoto za kimaisha ukiwamo umasikini uliovuka ada. Ili tufike huko nchi zetu hazina budi kuheshimu na kutekeleza misingi ya demokrasia, utawala bora na utii wa sheria.
Hakuna popote anayeweza kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi, lakini ni busara kwa viongozi wanaotawala kuwa na busara na kufuata misingi ya Katiba ili kuepusha mambo kama hayo.

No comments:

Post a Comment