Baadhi ya mashirika yasiyo ya klserikali nchini Kenya yanaendelea kulalamika juu ya vitendo vya unyanyasaji vinavyotekelezwa na bodi ya kitaifa inayosimamia taasisi hizo.
Wamemshutumu mkurugenzi wa bodi ya mashirika yasiyo ya kiserikali Mohamed Fazul kwa kutumiwa vibaya na serikali kuwanyanyasa.
Kielelezo cha unyanyasaji huo umetokana na nakala kutoka kwa mkurugenzi wa bodi ya kitaifa ya mashirika hayo Mohamed Fazul kuwa mashirika hayo yalipokea dola 360,000 kutoka kwa wakfu wa George Soros kuendeleza shughuli za kisiasa nchini Kenya .
Fazul amedokeza katika nakala hiyo kwamba vyombo vya dola nchini Kenya vinachunguza suala hilo kwa minajili ya kuchukua hatua za kisheria baadae pamoja na kuangazia uhalali wa mashirika hayo kuwepo nchini.
Amedai kuwa mashirka hayo yamewaajiri raia wa kigeni na yanatekeleza shughuli zao kinyume na masharti ya taifa la kenya
Mashirika mengine ambayo pia yamehusishwa na uchunguzi huo ni pamoja na Tume ya haki za binadamu (Kenya human Rights Commision), Kituo cha Kimataifa cha Sera na kutatua migogoro (International Centre for Policy and Conflict) pamoja na Tume ya Kimataifa ya Majaji (International Commission of Jurist)
Wakati wa kesi ya kwanza kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017, mashirika kadhaa pia yalihangaishwa na bodi hiyo na pia maafisa wa polisi kwa madai ya kukosa kulipa ushuru na pia kuendeleza shughuli zao nchini Kenya bila ya kusajiliwa rasmi.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa malalamiko hayo yamekuja baada ya baadhi ya maafisa wa Shirika la Muhuri na Haki Yetu kutakiwa kufika katika makao makuu ya bodi hiyo jijini Nairobi kuweka wazi matumizi ya fedha zao.
Maafisa hao ni pamoja na Khelef Khalifa wa shirika la Muhuri pamoja na wenzake kutoka shirika la Kurangu Haki yangu.
Katika mkutano na wanahabari Jumatatu mshirikishi wa miradi katika shirika la Haki Yetu tawi la Mombasa Julias Wanyama amesema kuwa wanadhani harakati hizi zinalenga kuzuia mashirika hayo kuunga mkono kesi inayopinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika mahakama ya Juu.
Wamesisitiza kuwa wanaushahidi wa kutosha kuwa ingawa uchaguzi wa marudio ulifanyika kulingana na sheria kulikuwa na makosa mengi ikiwemo idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment