WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, amevionya vyama vya upinzani kuacha kuzungumzia suala la shambulio la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), katika kampeni za udiwani nchini.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati wa kampeni za kumnadi Mgombea Udiwani wa CCM wa Kata ya Chanikanguo, Cypria Mpetula, katika mkutano wa kampeni huku akivitaka vyama hivyo kunadi sera za wagombea wao badala ya shambulio la Lissu.
“Mimi nashangaa sana badala ya kunadi sera zao wamekazana kutangaza shambulio la Lissu, hivi shambulio la Lisssu linahusiana vipi na Kata ya Chanikangu.
“Haiwezekani kila siku wanashindwa kunadi sera zao, labda kuna jambo fulani wao walitarajia lifanyike ili wailaumu Serikali wanavyojifanya wana uchungu sana kuliko hata mimi ambaye Lissu ni ndugu yangu tunatoka wote Singida,” alisema Mwigulu.
Katika hatua nyingine, Mwigulu ameliomba Jeshi la Polisi Wilaya ya Masasi kulipitia upya jalada la kesi la mgombea wa udiwani Kata ya Chanikanguo kwa tiketi ya Chadema na kuchunguza upya kwa kuwa kesi za jinai huwa hazina ukomo.
Alisema mgombea huyo anatuhumiwa kuiba mabati 20,000 katika Halmashauri Mji wa Masasi alipokuwa Lindi kwenye kampuni moja ya ulinzi na magunia manne ya korosho alipokuwa mjumbe wa bodi ambazo baadaye alizirudisha baada ya kubanwa.
“Jeshi la Polisi pitieni upya kesi yake na kuichunguza juu tuhuma zinazomkabili mgombea huyo, mashahidi wapo haiwezekani tukawa na mgombea mwenye sifa mbaya ya wizi halafu aje kutuongozea kata yetu, kama ameshindwa kulinda mali za halmashauri ya mji alipokuwa ni askari, atawezaje kuwa na uaminifu wa kulinda mali za kata akiwa diwani?
“Ninaomba wale pia wanaoshiriki katika kunadi mambo hayo wachunguzwe pia,” alisema Mwigulu.
Kwa upande wake mgombea udiwani Kata ya Chanikanguo, Cypria Mpetula, aliwaomba wananchi wamchague kwa kuwa anaweza kuwaletea maendeleo kwani anao uzoefu wa uongozi kwa muda mrefu kama katibu wa kata hiyo.
No comments:
Post a Comment