Madaktari nchini Uganda wamejiunga na waendesha mashtaka katika mgomo, kuishurutisha serikali kuwapa nyongeza ya mishahara na kuboresha maeneo yao ya kufanyia kazi.
Hatua ya madaktari kugoma imeafikiwa baada ya mkutano uliodumu zaidi ya saa 10 katika hospitali kuu ya rufaa ya Mulago.
Juhudi za Waziri wa Afya Sarah Opendi kuwaomba madaktari kusitisha mgomo huo wakati serikali ikishughulikia madai yao ziligonga ukuta.
Waziri Mkuu Dkt Ruhakana Rugunda aliitwa katika mkutano huo lakini akawa na wakati mgumu kuwahutubia madaktari na kuondoka kwa hasira.
Makamu wa Rais wa muungano wa madaktari nchini Uganda Profesa Pauline Byakika, ameeleza kwamba mgomo huo hauwezi kuepukika.
“Madaktari wanataka maeneo yao ya kazi yaboreshwe, pamoja na kuongezewa mishahara. Tunafanya kazi katika mazingira hatari, hatuna nyumba za kuishi, hatuna usafiri lakini mara nyingi tunahitajika kufika kazini hata usiku wa manane kuokoa maisha,” ameeleza Prof. Byakika.
Madaktari wanataka kulipwa shilingi milioni 48 kwa wale wa kiwango cha juu na shilingi milioni 6.5 kwa wale wa kiwango cha chini.
Pia, wanataka serikali kuwapa nyumba, magari ya usafiri wa binafsi, walinzi pamoja na wafanyakazi wa nyumbani.
Lakini serikali imesisitiza kwamba haina pesa kutimiza matakwa hayo, na kwamba madaktari, sawa na wafanyakazi wengine wa uma, wasubiri hadi serikali iweke sawa viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wa uma.
Madaktari wanajiunga na wasimamizi wa mashtaka ambao mgomo wao unaingia mwezi wa pili.
Muungano wa wanasheria nchini Uganda, umekuwa ukisaidia katika mazungumzo kati ya serikali na wasimamizi wa mashtaka kujaribu kutatua mgomo ambao sasa umeingia mwezi wa pili, wasimamizi wa mashtaka wakitaka nyongeza ya mishahara na mazingira salama ya kazi.
No comments:
Post a Comment