Monday, November 6

Kubadili Katiba Uganda ni kufuru, asema Askofu


Kampala, Uganda. Mhashamu Askofu wa jimbo la Fortpotal Robert Muhiirwa amesema kuwa kufanyia marekebisho Katiba kwa lengo la kuondoa ukomo wa umri wa rais ni sawa na kufuru.
Askofu Muhiirwa alisema hayo jana katika mahubiri yake kwenye makaburi ya Wafia dini wa Uganda yaliyopo Namugongo kwamba viongozi wanaojihusisha na mchakato wa kubadili Katiba lazima wakumbuke kwamba walishika Biblia walipoapa kuitetea katiba.
“Neno la Mungu lisichezewe. Viongozi wa nchi hii wasiifanyie sitizai Biblia. Kwa hiyo basi, kwa mamlaka niliyonayo kama Askofu wa Kanisa Katoliki, Katiba isibadilishwe kwa ajili ya kumridhisha mtu mmoja,” alisema Askofu Muhiirwa.Soma: Rais Museveni aandaliwa mazingira ya kuwania urais
“Viongozi lazima waitetea Katiba bila maswali kwa sababu walitumia neno la Mungu kula kiapo,” aliongeza.
Mashabiki wa marekebisho ya katiba wanatafsiri kwamba kuilinda Katiba kunahusisha pia kuirekebisha kwa kuwa kipengele hicho pia kimo ndani ya Katiba.
Muswada uliowasilishwa Septemba kwenye Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Bunge unataka Ibara ya 102 (b) ya Katiba irekebishwe ili kuondoa ukomo wa umri wa rais.
Katiba ya sasa inamzuia mtu yeyote mwenye umri wa miaka zaidi ya 75 kuwania urais. Rais Yoweri Museveni sasa ana umri wa miaka 73 hivyo hataweza kugombea nafasi hiyo mwaka 2021 kwani atakuwa na miaka 77.
Wapinzani wa mabadiliko ya Katiba wanadai juhudi zote zinafanywa kumwezesha Museveni kugombea na hivyo kuwa rais wa maisha akiwa amedumu madarakani sasa tangu mwaka 1986. Wapinzani wa hoja hiyo wanakamatwa, wanawekwa mahabusu, wanatolewa bungeni na mikutano yao ya kuomba ushauri kwa wananchi inavurugwa.

No comments:

Post a Comment