Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amesema raia wote wa Nigeria ambao wamekwama Libya watarejeshwa nyumbani na kusaidiwa kurejelea maisha ya kawaida.
Akizungumzia video za karibuni ambazo zimekuwa zikiwaonesha Waafrika wakiuzwa kwenye mnada wa watumwa nchini Libya, Rais Buhari amesema inasikitisha sana kwamba "baadhi ya raia wa Nigeria wanauzwa kama mbuzi - dola kadha Libya".
Ameonekana pia kushangaa iwapo raia wa Libya walijifunza lolote la maana tangu kuondolewa madarakani kwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.
''Walichojifunza pekee ni kuwapiga watu risasi na kuua. Hawakujifunza kuwa mafundi wa umeme, mafundi wa mabomba au ufundi wowote ule," amesema.
Kwenye video iliyotolewa na CNN mapema mwezi huu, vijana kutoka mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara walionekana wakiuzwa kama wafanyakazi wa mashambani kwa wanunuzi.
Walikuwa wanauzwa $400 (£300) katika eneo ambalo halikufichuliwa Libya.
Rais huyo wa Nigeria ameapa kupunguza idadi ya raia wa Nigeria wanaolazimika kufunga safari ndefu na hatari kupitia jangwa la Sahara na bahari ya
Mediterranean kufika Ulaya.
Amesema hilo litatimizwa kwa kutoa huduma bora ya elimu, afya na chakula nchini Niugeria.
Bw Buhari amesema hayo katika kikao na raia wa Nigeria wanaoishi nje ya nchi pambizoni mwa kongamano kuu ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya mjini Abidjan, Ivory Coast.
No comments:
Post a Comment