Friday, October 27

Zifahamu sababu za wazee wa baraza kumtia Lulu hatiani


Dar es Salaam. Wazee wa baraza wameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa mwigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu amehusika kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Wakitoa maoni yao jana baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, wazee hao walieleza kuwa Lulu ndiye aliyesababisha kifo cha mpenzi wake huyo wakati wa ugomvi baina yao usiku wa Aprili 7, 2012.
Wakizungumza mmoja baada ya mwingine, wazee Omary Panzi, Sarah Lugoma na Rajabu Mlawa, walihusisha tukio la Kanumba kujibamiza kichwa ukutani na kusukumwa na mshtakiwa.
“Kutokana na sababu na uainishi wa kesi (ushahidi) wa pande zote, mimi kwa upande wangu nimeridhika kuwa Elizabeth (Lulu) ameua bila kukusudia,” alisema mzee Mlawa na kuongeza: “Katika ugomvi, inawezekana hekaheka za kujinusuru, alitumia nguvu kumsukuma Kanumba na kuanguka ukutani. Hivyo, kwa maoni yangu kosa la kuua bila kukusudia kwa Elizabeth limethibitika.”
Akitoa maoni yake, Sarah Lugoma alisema Kanumba alifariki dunia kutokana na ugomvi baina yake na mpenzi wake (Lulu) kwa kuwa ndani kulikuwa giza, Kanumba aliteleza wakati wa ugomvi huo akaanguka.
“Hivyo mshtakiwa aliua bila kukusudia,” alisisitiza Lugoma wakati akihitimisha maoni yake.
Mzee mwingine, Panzi alisema Kanumba aliteleza na kuanguka wakati wa ugomvi huo, mshtakiwa ndiye aliyehusika na kifo chake kwa kuua bila kukusudia.
Hata hivyo, maoni ya wazee hao wa baraza siyo hukumu halisi ya Mahakama bali yanayotokana na mtazamo wao tu katika hali ya kawaida nje ya sheria kwa namna walivyousikiliza ushahidi wa pande zote.
Hivyo, kumtia hatiani mshtakiwa huyo hakumaanishi kuwa tayari ana hatia kwa kuwa maoni hayo hayamfungi jaji katika hukumu yake ambaye huongozwa na sheria husika.
Kwa hiyo, hatima ya msanii huyo kama ana hatia au la itabainishwa na Mahakama Novemba 13 wakati Jaji Sam Rumanyika anayesikiliza kesi hiyo atakapotoa hukumu.
Jaji awakumbusha wazee
Jaji Rumanyika aliwakumbusha wazee hao muhtasari wa ushahidi uliotolewa na pande zote kabla ya kutoa maoni yao.
Jaji Rumanyika akieleza kwa ufupi kilichozungumzwa na kila shahidi wa pande zote, alitoa mwongozo kwa wazee hao pamoja na mambo mengine, kutoa maoni yao bila kuongozwa na huruma wala kuogopa chochote.
“Mnalo jukumu la kutoa maoni yenu bila kuongozwa na huruma wala vitisho. Mnatakiwa kutoa maoni yenu kwa mujibu wa ushahidi mliousikia,” alisema Jaji Rumanyika.
Aliwaeleza kuwa kama walivyosikia ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa umejikita kwenye ushahidi wa kimazingira, mshtakiwa ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuwa na Kanumba.
Alisema ushahidi wa kimazingira lazima uwe ni vipande ambavyo ni mnyororo (muunganiko) unaomhusisha mshtakiwa kuwa ndiye ametenda kosa.
“Kama mkiona kuwa mshtakiwa ametoa maelezo ya kutosheleza basi mnaweza kusema hana hatia, lakini kama mna maoni tofauti pia mtaniambia,” alisema Jaji Rumanyika na kuongeza:
“Mkiona kuwa kifo hicho kilitokana na ugomvi, basi shtaka lake huwa ni la kuua bila kukusudia, mkishawishika kwa vyovyote na kwa namna yoyote ile mshtakiwa hakuhusika na kifo hiki msisite pia kunipa maoni yenu.”

No comments:

Post a Comment