Friday, October 27

Mvua yazua balaa Dar

Wananchi wakiangalia maji ya mvua yaliyofurika
Wananchi wakiangalia maji ya mvua yaliyofurika katika Barabara ya Morogoro ambayo yalifunika daraja la Mpakani linalounganisha mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kufuatia mvua iliyonyesha kwa siku mbili. Picha na Salim Shao 
Dar es Salaam. Mvua ni baraka, lakini kwa wakazi wa jijiji la Dar es Salaam mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jana, iligeuka kuwa balaa baada ya kusababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na watu sita kutojulikana walipo na zaidi ya nyumba kubomoka eneo la Mbezi.
Kama ilivyo kawaida jijini Dar es Salaam, mvua hiyo iliharibu miundombinu ya usafiri ya maeneo kadhaa, ikisababisha baadhi ya barabara kutopitika na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Kasi (Udart) kulazimika kusimamisha shughuli zake.
Udart imesema jana kuwa ilisitisha huduma kutokana na eneo la Jangwani, ambako kuna ofisi zake, kujaa maji hivyo kuathiri shughuli zake.
“Tumesitisha huduma za mabasi yote kutokana na eneo la Jangwani kujaa maji,” alisema mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Udart, Deus Bugaywa.
Barabara kadhaa zilikuwa hazipitiki magari na watembeao kwa mguu, huku mitaa kadhaa ya maeneo ya Jangwani ikiwa imefurika maji na kusababisha wakazi kukimbilia Barabara ya Kigogo-Mabibo kushuhudia maji hayo, ambayo pia yalifurika hadi juu ya daraja la Kigogo Mwisho.
Wakazi wa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam walikumbwa na mshangao jana alfajiri wakati walipokuta maeneo yao yamefurika maji kutokana na mvua hiyo iliyonyesha kuanzia juzi jioni na kuendelea usiku kuamika jana. Baadhi walishuhudia nyumba zao zikibomka na madaraja kukatika.
“Hali ni mbaya. Mimi mwenyewe ukuta wa nyumba yangu umebomoka na nyumba za wananchi wangu zipatazo 11 zimebomoka,” alisema mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi kwa Yusuph, Josephat Mbuya.
Mwenyekiti huyo alisema nyumba sita zipo eneo la mtaa huo na tano ziko Mbezi Inn.
Mvua hizo zilisababisha daraja eneo la Mbezi kuvunjika na hivyo basi la daladala lililokuwa limebeba abiria kutoka Segerea kuelekea Mbezi Mwisho lilikwama daraja baada ya kuzidiwa na kasi ya maji yaliyofunika daraja hilo.
Abiria waliokuwa ndani ya daladala hilo waliokolewa wote huku mmoja wao akizimia na kupelekwa hospitali.
Mvua hiyo pia ilisimamisha shughuli za kijamii, wananchi walishindwa kwenda kazini wakiwamo wanafunzi ambapo walishindwa kufika shuleni kutokana.
Maji yalijaa barabarani huku shughuli za usafiri zikisimama , maduka na vibanda vya biashara vilifungwa na vingine vikisombwa na maji.
Pia mwenyeki wa Mtaa wa Kiluvya kwa Komba, Julius Mgini alisema watu sita wanasadikiwa kusombwa na maji eneo hilo akiwamo mtoto mmoja na nyumba za familia tatu zimebomoka.
“Katika eneo langu kuna daraja limekatika na watu sita wanasadikiwa kusombwa na maji. Waliosombwa ni pamoja na mtoto mdogo ambaye bado hatujajua umri wake,” alisema.
Hata hivyo, kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Jumanne Muliro alisema bado wanakusanya taarifa za mafuriko hayo na baadaye kuzipeleka kwa kamanda wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.
Kamanda Mambosasa pia alisema wanafanya tathimini ili kujua athari za mafuriko.
Hali halisi
Hali ilikuwa mbaya pia katika daraja la Mpakani, Kiluvya ambako mafuriko yalisababisha magari kushindwa kupita saa kadhaa.
Mwananchi ilifika eneo hilo na kushuhudia baadhi ya abiria ambao walikuwa wakiingia au kutoka nje ya Dar es Salaam kwa kutumia Barabara ya Morogoro.
“Tangu saa 6:00 daraja hili lilianza kujaa maji taratibu na kadri muda unavyokwenda likaonyesha mtikisiko kwa watu wa mwisho kuvuka daraja hili. Baadaye madereva waliogopa kuvuka kwa kuwa maji yaliongezeka. Tangu hapo mpaka sasa saa 9:00 usiku hakuna gari lililokuwa linavuka,” alisema mkazi wa eneo hilo, Jackson Lyimo.
Diwani wa Kiluvya, Aidan Kitare alisema bado hajapata taarifa kamili kuhusu watu waliosombwa na mafuriko eneo hilo na akaomba atafutwe mwenyekiti wa mtaa huo ambaye alisema ni watu sita.
Katika eneo la Tegeta Nyaishozi, mvua hizo zimesababisha baadhi ya nyumba na vituo vya mafuta kufunikwa na maji huku vitu vikisombwa na maji.
Wakati maji yakiwa yamejaa, wananchi walisimama nje ya nyumba zao na wengine wakijaribu kutoa maji na kuokoa mali zao.
“Tumekaa tu maji yameingia hadi ndani magari yanaelea kwenye maji,” alisema mkazi wa eneo hilo, Abuu Magetta.
Mkazi mwingine, Said Juma alisema wakazi walishindwa kuokoa mali zao.
Eneo la Kigogo pia halikusalimika.
Maji yalijaa katika daraja lililopo eneo hilo na kukwamisha magari kupita huku watu wengi wakikimbia kujinusuru na wingi wa maji uliokuwa ukiongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukienda.
Katika maeneo ya Tabata Relini, maji yalijaa hadi kwenye reli kiasi cha kufanya isionekane huku vibanda vya wauza chakula vikizingirwa na maji kila kona na kusababisha shughuli zao kusimama.

No comments:

Post a Comment