Wednesday, October 18

Watumishi wa umma wapewa mbinu ushindani wa ajira


Watumishi wa umma wametakiwa kujiendeleza kielimu ili kuingia katika ushindani wa ajira wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).
Wametakiwa wasisome kwa mazoea ya kujiendeleza kielimu kwa ajili ya kupanda madaraja, bali ili kuingia katika ushindani wa ajira.
Akizungumza na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma, jijini Dar es Salaam jana Jumanne Oktoba 17,2017, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alisema mbali ya kusoma pia wajifunze lugha ya Kiingereza. Amesema ni ukweli usiopingika kuwa Kiingereza ndiyo Kiswahili cha dunia.
Amesema hakuna awamu hata moja kati ya tano za Serikali iliyowahi kukataza watumishi kujifunza, hivyo wajizatiti katika elimu.
“Wakenya wanatushinda kwa hata Kiswahili tunachodhani tunakifahamu ambacho pia hatukijui, wao wanazungumza Kiswahili fasaha walichosoma darasani, sisi tunazungumza cha mtaani,” amesema Mkuchika.
Amewataka waajiri kuhakikisha wanawasilisha vielelezo vya watumishi wa umma waliohukumiwa na kukataa rufaa katika tume hiyo kwa wakati.
Mkuchika amesema imeonekana hiyo ni moja ya changamoto za watendaji wa tume, hivyo atakayekaidi atachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwemo kupelekwa kwa waziri au kwa Rais kulingana na aliyemteua.
“Inatakiwa ushahidi uwasilishwe ndani ya siku 14, baada ya mtumishi kukata rufaa, kesi hazitakiwi kuchukua muda mrefu, zikizidi hapo nahitaji taarifa kwa ajili ya kuchukua sheria inayostahiki,” amesema.
Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Richard Odongo amesema tume inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa bajeti ya kutosha kukamilisha majukumu yake.
“Kama hakuna fedha za kwenda kufanya ukaguzi wa utendaji, watumishi na waajiri wanajifanyia wanavyotaka kwa sababu hakuna wa kuwakagua, ” amesema Odongo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment