Wednesday, October 18

Maajabu wa msitu wa uamuzi Serengeti-2




Mvutano uliokuwapo kwa muda mrefu kati ya Serikali na wazee wa mila mkoani Mara kuhusu kusimamishwa kwa ukeketaji wa watoto wa kike, huenda ukabaki historia baada ya wazee wa mila wa ukoo wa Inchungu wilayani Serengeti kutangaza kusimamisha vitendo hivyo.
Katika sehemu ya kwanza ya makala haya mwandishi alishiriki katika kikao cha kutoa uamuzi wa kusitisha vitendo hivyo kilichofanywa na wazee hao ndani ya msitu wa uamuzi uliopo katika Kijiji cha Nyamakendo wilayani humo. Endelea.
Ngariba kulishwa yamini
Mwenyekiti wa wazee wa mila wa ukoo wa Inchugu nchi za Tanzania na Kenya, Masonoro Marwa  anasema kabla ya ukeketaji baadhi ya wazee hupata njozi za kujua kama kipindi hicho kutatokea balaa na namna ya kuliepusha kisha hutengeneza dawa ikiwemo kuzuia damu kuvuja ama watoto kufariki dunia, kukinga eneo husika na ngariba wanayekuwa wamemchagua. Anasema ngariba wote wa ukoo huo watalishwa yamini na atakayekiuka na kuendelea na kazi hiyo atapata madhara.
“Baada ya mzunguko wa kuwatangazia jamii yetu tutawaita ngariba wote na kuwalisha yamini (kehore) kupitia fuvu la mtu na kuwaharibu haribu kwa njia tunayojua sisi,” anasema na kuongeza:
“Atakayekaidi na kuamua kwenda kukeketa atakufa kabla ya kufika eneo husika, maana nasema ukeketaji unaanzia kwa wazee wa mila na sasa wameamua kuumaliza. Kwa kuwa tumebarikiwa na ‘wazee’ wetu katika msitu wa uamuzi lazima tushughulike na anayetaka kutukwamisha.”
Mwenyekiti huyo anayeongea taratibu kwa tahadhari kubwa anasema kuwa wataharibu madawa na vifaa vya ngariba kwa kutumia dawa ikiwa ni ishara ya kukomesha ukeketaji na kwamba kazi iliyobaki kwao ni kuhakikisha wanahimiza elimu kwa mtoto wa kike.
“Tutachagua (njia) nyingine mbadala ya kumvusha rika mtoto wa kike kama jando bila ukeketaji kwa wanaopenda, wasiokuwa tayari wataendelea…na kwa kuwa tunatambua kulikuwa na unyanyapaa kwa wasiokeketwa hilo tutalidhibiti kwa mifumo yetu wenyewe,” anabainisha.
Fimbo huonyesha ukuu wao
Mwenyekiti wa wazee wa mila Kata ya Machochwe, Nyandonge Chacha (72) anainuka na kuchukua fimbo, kisha anaanza kuongea kwa sauti kali kwa lugha ya Kikurya akimaanisha:
“Wazee umri wetu umekwenda kusumbuana na Serikali si vizuri, kama mambo mengi ya mila ya kutoboa masikio, kuvaa bangili, kupasua meno tumeacha kwanini hili litushinde?” anahoji.
 “Wazee wa mila tumelaumiwa sana kuwa sisi ndiyo tunakumbatia ukeketaji, tumechangia kudumaa kielimu kwa watoto wa kike…sasa tumefika wakati wa kwenda hadharani kusema ukeketaji basi, mtoto wa kike asome kama atakuwepo anayepinga huyo ndiye adui wetu sote,” anasema.

Chakula cha Pamoja
Katibu wa wazee wa mila, Peter Waitacho kabla ya kikao kufungwa anasimama na kusema:
“Wageni wetu baada ya kutoka hapa tutaongozana kwenda kwa mmoja wa wazee wa mila kwa ajili ya chakula cha pamoja, huo ndiyo utaratibu wetu,”anasisitiza.
Mwaliko huo ni jaribu jingine kwetu kutokana na mambo tuliyoshuhudia ndani ya msitu wa uamuzi na mambo waliyokuwa wanasema yote yanaonyesha wanaamini katika nguvu zisizo za kawaida, tukatazamana kwa muda, kisha nikasema tuko tayari.
Tulitembea kwa mguu kwa zaidi ya kilomita mbili hadi Kitongoji cha Isaboka, Kijiji cha Nyamakendo kwa Wambura Maswi, tukapokewa na kundi la wazee waliotangulia kwa gari wakatukaribisha kinywaji aina ya togwa (bhusara).
Tunakaribishwa na kupewa vikombe vitupu kisha wanaleta togwa, ingawa situmii kinywaji hicho nalazimika kushiriki ili nisiende tofauti na taratibu zao. Kabla hatujaanza kunywa mzee Maswi anachukua vikombe vyetu wageni, anaonja kidogo kisha anaturudishia na kuturuhusu tuendelee kunywa.
“Ninyi ni mara ya kwanza kufika kwangu ndiyo maana nimeanza kuonja msifikiri nimeweka kitu kisicho cha kawaida…huo ni utamaduni wetu, karibu sana na endeleeni kwa amani,”anasema.
Tukaendelea na kinywaji hicho kama tulivyoambiwa kisha kikafuata chakula cha pamoja tukihudumiwa na wazee wa mila huku akina mama wakiwa mbali wakisubiri kuja kuchukua sahani za nyama zilizobaki ili waende kula.

Ngariba asalimu amri
Mmoja wa mangariba maarufu wa ukoo huo, Matinde Kinyunyi wa Kijiji cha Ngarawani, Kata ya Uwanja wa ndege anaamua kujisalimisha kwa wazee wa mila na kuweka sahihi ya kuachana na ukeketaji, licha ya kumkubalia wanasema muda ukifika watamwita rasmi ili awasilishe mikoba yake na kula yamini.

Wazee wamkuna mchungaji
Mchungaji wa Kanisa la Wasabato Matare, Nicodemas Nyahonyo anasema uamzi wa wazee wa mila kuacha ukeketaji ni wokovu mkubwa kwa watoto wa kike na jamii ya Wakurya.
“Mwalimu (Juliusi) Nyerere aliwahi kusema wakati mataifa mengine yaliyoendelea yanatembea sisi tunatakiwa kukimbia, sasa jamii ya Wakurya inatakiwa kukimbia kwa kuwasomesha watoto wa kike ili kuyafikia makabila mengine, hii itatusaidia kupata wataalamu kutoka miongoni mwetu, maana tuliishia kuwaoza,” anasema.
Anasema kitaalamu ukeketaji una madhara makubwa kiafya na kisaikolojia kwa wanaofanyiwa na wanapata shida wakati wa kujifungua.
“Wazee wa mila nguvu yenu kwenye jamii itumike kuleta maendeleo si madhara kama mlivyokuwa mnafanya, himizeni elimu na maendeleo ili mwishoni muweze kukumbukwa, kwa sasa mlikuwa mmefikia hatua ya kuogopwa kwa kusimamia vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike,” anasema.

Nini kifanyike?
Meneja wa Mradi wa Tokomeza Ukeketaji Serengeti, unaotekelezwa na Amref Health Africa, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Halmashauri na wadau wengine kwa ufadhili wa UN WOMEN, Godfrey Matumu  anasema njia mbadala watakayosimamia wazee wa mila ni unyago bila ukeketaji.
“Kwa kuwa wamekubaliana kuacha ukeketaji wataelimishwa namna ya kuendesha unyago bila ukeketaji, ambao watoto wa kike watavushwa rika bila kukeketwa, lakini watafanyiwa matambiko mengine yote na hawatakatwa sehemu zao za siri,”anasema.
Anasema jando bila ukeketaji imefanikiwa katika eneo la Samburu nchini Kenya, Kiteto mkoani Manyara  na Kilindi mkoani Tanga na kwamba hakuna mtoto wa kike anayekimbia kwao kwa kuwa hafanyiwi ukatili, badala yake wanafundishwa mambo mengi ya maisha, utii kwa wazazi na uzalendo kwa nchi yao.
“Kwa kuwa kuna koo sita wilayani hapa zinazojihusisha na ukeketaji, kila moja itachagua njia ambayo wataitumia kuwatoa watoto jandoni, wapo wanaowapaka unga, wengine kuwavika bangili na namna nyingine kama ishara ya mtoto kuvuka rika. Tunataka utu wa mtoto wa kike ulindwe si kutwezwa kwa kukatwa sehemu zake za siri kama ilivyokuwa,” anabainisha.
Matumu anasema hiyo ni njia pekee inayowaacha watoto salama na kubakia kwenye familia zao.
“Mwaka jana watoto wengi wamekimbia kwao na kutunzwa maeneo mbalimbali kutokana na hofu ya kufanyiwa ukatili…mila inakuwa na faida gani inapofika wakati familia inasambaratika?” anahoji.
Anasema moja ya sifa kubwa ya wazee wa mila ni kuhakikisha wanalinda jamii isisambaratike, familia zibaki na umoja, lakini kwa vitendo vya ukeketaji vimechangia faraka ndani ya ndoa, watoto wamekimbia na kuishi ughaibuni kama yatima, hiyo si sifa njema ya wazee wa mila ambao ni kimbilio kubwa.
Katibu wa wazee wa mila wa ukoo wa Inchugu, Ngarawani Nyandonge anasema wazee wa mila wamekubaliana na unyago bila ukeketaji na kuwa wanasubiri muongozo ili waweze kuutumia kuvusha watoto rika.
“Hiyo itatumika mwaka kesho maana ni mwaka unaogawanyika kwa mbili ambao ukeketaji ungefanyika, sasa tutafanya unyago bila ukeketaji,”anasema.
Mkurugenzi wa kituo cha Nyumba Salama kinachotunza watoto wanaokimbia kukeketwa Mugumu Serengeti, Apaisaria Kiwori anasema wana watoto 77 miongoni mwao ni wanafunzi wa sekondari, shule ya msingi na wengine wanajifunza ufundi ambao wamefika hapo wakikimbia kukeketwa.
“Hata watoto wakiwaona wazee wa mila wanajificha, hivyo hatuwezi kutengeneza taifa zuri kama watoto wanakua wakiogopa wazee ambao walipaswa kuenzi mambo mazuri kwao, wanajenga tabia ya kuwachukia wazee wao, kwa uamuzi wao wa kuachana na ukeketaji sasa watajenga mshikamano na jamii kwa masuala ya kijamii na kiuchumi,” anadai.
Anasema kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha watoto wa kike wanaendelezwa kielimu ili waweze kuharakisha maendeleo ya jamii na Taifa na kuimarisha mfumo wa usawa katika malezi na uamuzi.
Baadhi ya watoto waliohifadhiwa katika kituo cha Nyumba Salama wanaiomba Serikali kufuatilia kwa karibu uamuzi wa wazee wa mila kwa kuwa baadhi hugeuka na kurudia ukeketaji, huku wakibainisha kuwa kama watabaki na uamuzi huo utawasaidia watoto wa kike kuishi na kusoma kwa bidii.
Ofisa mradi huo, William Mtwazi ambaye kitaaluma ni mwanasheria anasema ukeketaji ni kosa la jinai na unaangukia katika makosa makubwa yanayosababisha madhara kwa wanaofanyiwa na adhabu yake ni kubwa.
“Sheria ya Mtoto Namba 21  ya mwaka 2009 na sheria nyingine zilizotungwa na Bunge na zile za kimataifa zinaharamisha vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike na jamii imepewa jukumu la kuhakikisha watoto wa kike chini ya miaka 18 hawafanyiwi ukatili, wazee kama wameong’oka ni wajibu wa jamii kusimamia msimamo huo kwa watakaokiuka,” anabainisha.

Polisi wanena
Inspekta wa Polisi, Alfred Malimi anasema Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 ambayo  ilifanyiwa mabadiliko mwaka 2002 na inajulikana kama Kanuni ya adhabu sura ya 16 katika kifungu cha 169(A)  inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 5 na kisichozidi miaka 15 na faini ya fedha kwa anayetiwa hatiani kwa kumkeketa mtoto wa kike.
“Sisi tunaheshimu sana uamuzi wa wazee wa mila kuachana na ukeketaji kwa kuwa wanaacha kutenda kosa la jinai, lakini kama wataenda kinyume na kauli na misimamo yao hawataweza kukwepa mkono wa sheria,” anasema.

DC asema Serikali haitalala
Mkuu wa wilaya hiyo, Nurdin Babu anasema Mei 16 mwaka huu wazee wa mila wa koo sita za Wainchage, Wainchugu, Wakenye, Watatoga, Warenchoka na Wangoreme walisaini mbele yake, polisi na Mradi wa Tokomeza Ukeketaji kuwa wameacha vitendo hivyo.
“Julai wamekuja kwangu wakasema wanahitaji kuzunguka kwa wazee kwenye ukoo wao kuzungumza na jamii zao kwenye mikutano ya hadhara, tumewaruhusu wanaenda na vikao vya wazee wa mila vinaendelea kwa kuwa wamefikia hatua hiyo sisi kazi yetu ni ufuatiliaji,” anasema.
Anasema wanatakiwa kusimamiana wao kwa wao kutokana na makubaliano yao kwa kuadhibiana kwa mila na desturi, lakini wanaposhindwa kazi ya polisi ni kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Mwaka 2014 watoto  wa kike 14,121  wilayani Serengeti waliandikishwa na makatibu wa mila wa koo za Inchugu, Inchage, Warenchoka na Wakenye kwa ajili ya kukeketwa.
Mwaka  2016 jumla ya watoto 5,621 waliandikishwa kukeketwa kati yao 2,313 sawa na asilimia 41 walikeketwa,762 sawa na asilimia 14 walikataa na kukimbia kwenye vituo maalumu na kuhifadhiwa na ukoo uliobainika kuongoza ni Inchugu kwa kukeketa asilimia 56 ya walioandikishwa.
Watatoga walikeketa kwa asilimia 22, Warenchoka asilimia 12.4, Inchage asilimia 13, Wakenye asilimia 11 na Wangoreme asilimia 6.3, takwimu zinazoonyesha kuwa mwaka jana ukeketaji ulipungua kwa asilimia 40.
Mwaka 2016 ngariba saba walikamatwa, mzee wa mila mmoja, ngariba wawili na wazazi wawili walihukumiwa vifungo kati ya miaka mitatu hadi mitano na ngariba mmoja anakabiliwa na kesi tano zinaendelea.
Mikoa ya Manyara, Singida na Mara inatajwa kwa kushamiri kwa vitendo vya ukeketaji, kwa mkoa wa Mara wilaya za Serengeti na Tarime zinadawa kuwa vinara.

No comments:

Post a Comment