Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamin Sitta amefungua semina ya mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa mtaa, kata na wenyeviti wa mtaa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo yao kabla hayajafika ngazi za juu.
Akizungumza mara baada kuzindua mafunzo hayo mstahiki meya Benjamin Sitta amesema kuwa kuna kero nyingi sana katika manispaa ya Kinondoni hivyo kupitia semina hiyo watakumbushwa wajibu wao katika kuwahudumia wananchi na hatimae kero hizi zitaishia ngazi ya chini kwani zipo ndani ya uwezo wao.
"Tumeshuhudia viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na Rais John Pombe Magufuli wakisimamishwa na wananchi na wakiambiwa kero ambazo zipo chini ya uwezo wa viongozi wa kata jambo ambalo si sahihi" Alisem Meya Sitta.
Katika hatua nyingine Mstahiki Meya Sitta ameahidi kutowafumbia macho watendaji wazembe kwani wanarudisha nyuma kasi ya maendeleo inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli.
"Tutawachukulia hatua kali watendaji wazembe ikiwemo kuwasimamisha tumeisha anza na mmoja na wengine watafuata kwani manispaa imelipa fidia ya zaidi ya bilioni 10 kutokana na watendaji wasio tambua majukumu yao, ila wale wenye kufanya vyema tutawapongeza kwa kutambua mchango wao" Alisema Meya Sitta.
Kwa upande wake Marry Asei Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema mafunzo hayo ni matunda ya ziara ya Dar Mpya chini ya Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta akizungumza katika semina ya mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa mtaa, kata na wenyeviti wa mtaa lengo ni kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali, leo jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya watendaji wa mtaa, kata na wenyeviti wa mtaa wakimsikiliza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta. (Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii)
No comments:
Post a Comment