Wednesday, October 11

VIGOGO WAWILI CHUO CHA UHASIBU (TIA) WAPANDISHWA MAHAKAMA YA KISUTU JIJINI DAR LEO.

Na Karama Kenyunko, blogu ya Jamii.

Vigogo wawili wa chuo cha uhasibu (TIA) jijini Dar es Salaam, leo wamepandishwa katika kizimba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili, la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya bilioni moja.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa serikali kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa, Leornad Swai amewataja watuhumiwa hao kuwa ni, Shaha Mussa Hanzuruni na Onesphory Ambangile Luhungu.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba imedaiwa, kati ya January Mosi 2012 na Desemba 30 2014, katika chuo hicho cha TIA kilichopo katika wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam washtakiwa hao walitenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Imedaiwa, washtakiwa, walitumia vibaya madaraka yao kwa kutofuata taratibu za manunuzi katika ununuzi wa ardhi wa chuo hicho (TIA) kampasi uya Mwanza na kimsababishia Vedasto Lupungo kupata manufaa ya Sh.1,097,681,107./-

Katika shtaka la pili imedaiwa siku na mahali hapo washtakiwa hao kwa ridhaa zao na matendo yao waliisababishia TIA Hasara ya Sh. 1,097,681,107/- kwa kutokifuata sheria za manunuzi wakati wa kusaini mkataba wa ardhi Wa eneo la TIA kampasi ya Mwanza.

Kwa kuwa DPP ameipa mamlaka mahakama ya Kisutu kisikiloza kesi hiyo ya uhujumu uchumi, washtakiwa walipata nafasi ya kijibu juu ya tuhuma hizo ambapo wote wamekana kutenda makosa hayo na mahakama ikawasomea masharti ya dhamana kwa kuwa kesi hiyo inadhaminika

Akisoma masharti ya dhamana, Hakimu Simba amewata washtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaoweka bondi ya milioni 250 kila mmoja, pia amemtaka mdhamini mmoja kati ya hao kuweka mahakamani pesa taslimu, milioni 250 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha ambayo Ipo ndani ya mkoa wa DSM.

Pia wametakiwa kuwasilisha Pasi zao za kusafiria vilevile hawaruhusiwi kusafiri nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ruhusa ya maandishi kutoka mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment