Tuesday, October 10

Vyombo vya usalama Kenya vyadaiwa kuuwa watu 30

Askari wa Kenya wa kuzuia fujo wakiwadhibiti waandamanaji.
Tume ya Haki za Binadamu ya Taifa nchini Kenya imevituhumu vyombo vya usalama vya nchi hiyo kwa kuwauwa watu zaidi ya 30 kufuatia uchaguzi wa Agosti 18.
Mwandishi wa VOA ameripoti kuwa kikundi hicho cha haki za binadamu ambacho kinapata ruzuku kutoka serikalini kimechapisha ripoti Jumatatu yenye kichwa cha habari “Mirage at Dusk” inayoelezea ukandamizaji wa haki za binadamu.
Kwa mujibu wa tume hiyo, watu 34 akiwemo mtoto wa miezi sita, waliuawa na polisi wakati wa vurugu ya siku tatu. Watu wengine watatu waliuawa wakati wa mapigano kati ya raia.
Mwanachama wa Tume ya Haki za Binadamu Jadidah Waruhiu amesema maadamano hayo yalisababishwa na Tume Huru ya Uchaguzi kutangaza kuwa Rais aliyekuwa madarakani Uhuru Kenyatta alikuwa amemshinda kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
“Kulikuwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo katika nchi hiyo yakipinga tangazo hilo la ushindi, na tulikuwa na maandamano Jijini Nairobi, na hasa katika makazi yasiyo rasmi kama vile Mathare, Dandora, Kibera. Kati ya hayo tulikuwa na maadamano Kisumu. Kwa bahati mbaya wakati wa maandamano hayo na masiku kadhaa baadae, tulikuwa na Wakenya wengi waliokuwa wamejeruhiwa, na pia tulikuwa na baadhi waliouawa, na hadi sasa katika kumbukumbu zetu Wakenya 37 walipoteza masha kwa sababu ya machafuko hayo.
Lakini Waziri wa Mambo ya Ndani Mwenda Njoka hakubaliani na ripoti ya tume hiyo.
“Vifo ambavyo vinaweza kufunganishwa moja kwa moja na vurugu vilikuwa ni chini ya watu 10. Lakini kwa Tume ya Haki za Binadamu ya Taifa ya Kenya kujitokeza na kusema kuwa watu 37 wameuawa na polisi, ni ripoti ambayo imepotoshwa. Lakini ilikuwa juu yao kutoa majina na sehemu ambapo watu hawa waliuawa na habari maalum inayo onyesha siku na wapi walipokufa na kilichosababisha vifo hivyo.”
Warihiu amesema idadi hiyo inawezekana ni kubwa zaidi, kwa sababu watu wengi wanaogopa kuzungumza juu ya vitendo vya unyanyasaji vya polisi.

“Kila kesi inahakikiwa na watu wetu kwa kwenda katika jamii, kuchukua taarifa za kila mtu aliyejeruhiwa au kutoka kwa familia ya marehemu. Kwa hiyo kesi hizi zimethibitishwa. Tulikuwa na ripoti zaidi ya hizi lakini idadi yake hatukuweza kuthibitisha na sifikirii kama tunaripoti zote kwa kuwa kulikuwa na hofu na vitisho baada ya matukio hayo.
Hali bado iko tete nchini Kenya wakati nchi ikijiandaa kurejea uchaguzi wa urais.
Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo Agosti 8, ikisema kuwa kulikuwa na dosari upande wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka. Marejeo ya uchaguzi yamepangwa kufanyika Octoba 26.

No comments:

Post a Comment